Jerry Cornel Muro awasilisha maoni yake mbele ya Kamati kuhusu miswada mitatu ya marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa,tume ya uchaguzi na sheria ya uchaguzi

DODOMA-Nimepata nafasi ya kutoa maoni mbele ya ya Kamati ya Bunge ya Kudumu Utawala, Katiba na Sheria iliyoanza kusikiliza maoni ya wadau na wananchi kuhusu miswada mitatu ya marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa, muswada wa sheria ya tume ya uchaguzi pamoja na muswada wa sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.
Miswada yote ni ya mwaka 2023, ambayo inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni kwa ajili ya kutoa nafasi kwa Bunge kujadili na wakiridhia kwa pamoja itaanza kuwa sheria.

Katika maoni yangu mosi, msingi wa miswada hii mitatu yenye kurasa 125 na vifungu 168 ni falsasa ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inayojulikana 'Four R' Reconsialiation, Rebuild, Reselience and Reform.

Falsafa ya R nne inamanisha katika taifa tunapaswa kupatana, kujenga, kubadilika na kuvumiliana katika msingi wa maendeleo ya taifa endelevu.

Ni falsafa ambayo ilisababisha kuundwa kwa kikosi kazi ambacho kilihusisha wadau mbalimbali walioleta maazimio ya kufanywa kwa mambo makubwa matatu ambayo ni kutazama masuala ya kisheria, kiutawala na katiba.

Katika maoni yangu nimemweleza mwenyekiti wa kamati kuwa ni msingi huu wa taarifa ya kikosi kazi alichounda Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ndio kilicholetelea kuandaliwa kwa miswada hii mitatu ikiwa ni takwa katika eneo la kisheria ambalo limezaa miswada hii mitatu ya kipekee kabisa nchini.

Nimemweleza pia, katika msingi wa falsafa ya R nne kupitia kikosi kazi pendekezo lingine lilikuwa ni suala la kiutawala ambalo tayari Mheshimiwa, Rais Dkt.Samia pamoja na wasaidizi wake wameshalifanyia kazi katika hatua za mwanzo na tumeona matokeo yake kuruhusiwa kwa mikutano ya vyama vya kisiasa, na shughuli nyingine za siasa katika ngazi na muktadha mbalimbali.

Katika miswada hii mitatu, sikutazama sana vifungu vya sheria maana vilishafafanuliwa na wabobezi nilijikita zaidi katika kuweka misingi itakayoweza vifungu vinavyojadiliwa kueleweka na kuridhiwa kwa pamoja pasipo kumuacha mtu pembeni na kutolea mfano wa majirani zetu ambao walitengeneza katiba mpya, wana tume huru ya uchaguzi na uhuru wa kutosha,lakini katika chaguzi zao tatu za Rais na wabunge na madiwani nachelea kusema hazikuwasaidia.

Maana waliingia katika machafuko yaliyosababisha mapigano watu kufariki na kuongeza kiwango cha uhasama mpaka leo pamoja na kuwa na mahakama huru, tume huru na katiba mpya hazijawasaidia kupunguza chuki na uhasama maana hata wao walikuwa na maridhiano yaliyohusisha pande mbili zinazohasimiana kisiasa na kusahau misingi mingine ambayo katika R-nne za Mheshimiwa Rais Samia imewekwa vizuri.

Katika maoni yangu nimesisitiza kwanza msingi wa dhamira ya dhati ya utekeleza wa R nne kwa pamoja hatua ambayo itatuleta pamoja kama taifa na kufungua njia sahihi ya majadiliano na makubaliano ya pamoja.

Katika maridhiano nimemweleza mwenyekiti kuwa maridhiano mbali na kuwa na taswira ya kisiasa, lakini yanakwenda mbali zaidi mpaka ndani ya vyama vyenyewe,wenyewe kwa wenyewe ndani, katika ngazi ya familia baba mama na watoto kuridhiana katika mambo ya msingi na hata viongozi wa dini kuridhiana.

Hatua itakayosakafia msingi wetu wa umoja mana MSINGI WA AMANI NI HAKI na haki sio serikalini pekee inakwenda mpaka katika ngazi ya Familia na shughuli zinazoathiria maisha yetu ya kila siku.

Katika masuala ya vifungu, kwanza nimekubaliana na umahiri na upekee wa weledi wa matayarisho ya miswada mitatu kama kianzio cha msingi wa kutafuta sheria mpya na kushauri mapungufu na changamoto za kimsingi zenye malengo ya kusaidia wananchi yafanyiwe marekebisho kadri yanavyopokelewa na hata sheria zitakapoanza kutumika mlango wa marekebisho usifungwe.

Maana tutakapokuwa tunazitumia ndivyo tutakopokuwa tunaona mapungufu yake kulingana na majira, matukio na nyakati.

Katika kifungu cha sita moja mpaka tatu limeibuliwa suala la wasimamizi wa uchaguzi huku rasimu ikiweka wazi kuwa tume inaweza kuwachagua wakurugenzi wa halmashauri au watumishi wa umma na itakapobidi tume inaweza kuchagua mtu yoyote yule kusimamia uchaguzi katika ngazi ya majimbo na kata.

Katika maoni yangu kuhusu kifungu hiki, nimemweleza mwenyekiti kuwa pamoja na sheria kutoa nafasi hiyo kwa makundi hayo ni muhimu pia uteuzi uzingatie weledi na ushirikishwaji wa makundi mbalimbali wakiwemo wanawake, walemavu, na vijana wenye sifa na sio kuteuliwa kwa cheo au nafasi tutazame sana sifa husika za kazi.

Katika kifungu hiki cha sita pia nimefafanua zaidi kuwa, msingi wa chaguzi kusimamiwa na wakurugenzi umeonyesha mafanikio katika chaguzi mbalimbali kuanzia mwaka 1992 vyama vingi vilivyoanzishwa japo kulikuwa na dosari kadhaa katika chaguzi za mwaka 2020 kutokana na baadhi ya wakurugenzi kutajwa kuwa makada ya baadhi ya vyama vya siasa na kuonyesha mashaka ya kutenda haki.

Nimemkumbusha Mwenyekiti kuwa cheo cha ukurugenzi wa halmashauri ni cheo cha kitaasisi ambapo katika taasisi hiyo kuna maafisa uchaguzi waliosomea na kupewa mafunzo ya ubobezi wa kusimamia uchaguzi.

Hivyo asitazamwe mkurugenzi kama cheo bali itazamwe taasisi yenye nyenzo na miundombinu wezeshi kuendesha na kusimamia uchaguzi mfano wataalamu waliopewa mafunzo kwa muda mrefu, ofisi zenye vifaa rejea ofisi ya maafisa uchaguzi halmashauri, magari.

Pia, halmashauri ndio yenye kujua na kutambua maeneo ya kiutawala ikiwemo vijiji, mitaa na shughuli nyinginezo hivyo wakati tunalijadili hili lazima tuweke mkazo wa endapo hawataruhusiwa tutapata wapi nyenzo wezeshi, wataalamu wenye mafunzo na walioandaliwa kusimamia uchaguzi katika kipindi hiki kifupi.

Katika maoni yangu nimeshauri changamoto ambazo zimebainika zilizoleta kasoro ya kutaka kuwaondoa wakurugenzi zitazamwe na kama zinaweza kufanyiwa kazi ingekuwa vyema zaidi kuliko kuanzisha jambo jipya linalohitaji gharama, muda na uundaji wake.

Nikashauri tunaweza kuboresha zaidi na kusonga mbele na mfumo wetu kwa hoja moja kubwa kuwa sheria iliyounda serikali za mitaa na tawala za mikoa zililenga katika ugatuaji wa madaraka kwenda kwa wananchi na kwa wasiofahamu niseme tu hizi halmashauri ni mali ya wananchi.

Maana zinaongozwa na wananchi kupitia uwakilishi wa madiwani na mwenyekiti wa halmashauri huku mkurugenzi mtendaji akibaki kuwa katibu wa vikao vya halmashauri na mtekelezaji mkuu wa maazimio ya vikao vya madiwani kwa kushirikiana na watalaamu huku akiwa na jukumu la kusimamia fedha za miradi mbalimbali inayopelekwa na serikali.

Katika kifungu hiki, nimuhimu sana kutambua tunapojaribu kuwaondoa wakurugenzi katika usimamizi wa chaguzi maana yake unaondoa wataalamu, unaondoa miundombinu wezeshi lakini pia unabeza na kutweza uwezo wao wa kusimamia chaguzi za serikali za mitaa na vijiji.

Chaguzi ambazo zimekuwa zikifanyika kwa mafanikio makubwa na pia tunaondoa hoja ya kutaka kuziunganisha chaguzi zote za Rais, wabunge na madiwani pamoja na chaguzi za serikali za mitaa pamoja mkakati ambao tunaweza kuuwaza katika miaka ijayo na ndipo tutaridhia basi wakurugenzi hawataepukika katika kusimamia chaguzi, katika hili cha msingi tupate wakurugenzi wenye sifa na weledi zaidi.

Nimehitimisha kwa kuwaambia wananchi miswada yote mitatu imezingatia kwa kiasi kikubwa katiba yetu na kwa jinsi nilivyoipitia miswada sijaona kama kuna ukinzani wa moja kwa moja kati ya katiba na miswada hii mitatu kama zipo changamoto wabobezi wanaweza kuendelea ninapoishia.

Nawashukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya utawala, katiba na sheria pia naishukuru Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,ninavishukuru vyama vya siasa vilivyojitokeza na kuwasilisha maoni yao kwa njia ya ubobezi mkubwa.

Pamoja na wadau kutoka asasi na taasisi mbalimbali na mwananchi mmoja mmoja kwa kujitokeza na kuitumia haki ya msingi ya kikatiba ya kutoa maoni.

Mungu ibariki Tanzania.
Mungu ibariki Africa

Naomba kuwasilisha.
Jerry Cornel Muro
Mwananchi.
06/01/2023

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news