Kamati ya Bunge yatembelea kazi ya uboreshaji Mfumo wa Sekta ya Ardhi

NA MUNIR SHEMWETA
WNMM ARUSHA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii imetembelea kazi ya uboreshaji Mfumo Unganishi wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi inayofanywa na timu ya wataalamu mkoani Arusha.
Mfumo huo unatarajiwa kuanza katika mikoa mitano ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Tanga na utarahisisha na kuharakisha upatikanaji huduma za sekta ya ardhi kwa kuwa wananchi watakuwa wakipata huduma kwa njia ya mtandao.

Akizungumza wakati wa kuikaribisha kamati hiyo jijini Arusha tarehe 8 Januari 2023 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mhe. Jerry Silaa amesema, mfumo unaoboreshwa na timu ya wataalamu mkoani Arusha asilimia mia moja utakuwa ni wa kidigitali.

‘’Baada ya kazi ya maboresho ya mfumo kukamilika, hatua zozote za ardhi zitakuwa zikifanyika kwenye mfumo na suala la mwananchi kwenda ofisi za ardhi kupata huduma ni uamuzi wake mwenyewe,’alisema Mhe. Silaa

Mkurugenzi wa Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Flateny Hassan ameeleza kuwa, uboreshaji wa mfumo unafuatia Wizara ya Ardhi kuwa na changamnoto kadhaa kwenye mifumo yake jambo alilolieleza kwamba limesababisha kuwepo uhitaji wa kuunganisha mifumo yote ili kuwa na mfumo mmoja utakaohusika na sekta ya ardhi.

‘’Kazi inayofanywa na timu ya wataalmu jijini Arusha kwa sasa imefikia asilimia 85 na matarajio ni kwamba ikifika Juni 2024 mikoa ya awali iliyopangwa itakuwa imefikiwa,’’alisema Flateny.

Maboresho yanayofanyika ni pamoja na mfumo unaoruhusu watumishi wa sekta ya ardhi kutekeleza majukumu yao ndani ya ofisi zao, mfumo unaoruhusu wananchi kuomba huduma kwa njia ya mtandao na huduma ya Mobile App ambao mwananchi anaweza kupata huduma kupitia njia ya mkononi.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuwa katika jitihada kubwa za kuhakikisha huduma za sekta ya ardhi zinapatikna kwa haraka na urahisi kupitia mifumo ya kidigitali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news