KKKT Mufindi:Viongozi wa dini waombwa kuweka mkazo katika kusimamia maadili

IRINGA-Viongozi wa dini wameombwa kuendelea kusimamia imara na kukemea matendo maovu yanayopelekea mmomonyoko wa maadili hususan kwa vijana hasa katika mazingira ya yanayoendeshwa zaidi na ulimwengu wa kidijitali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akipokea kwa niaba zawadi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Mhashamu Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo, mara baada ya ibada ya Kuwekwa Wakfu Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mufindi.

Hayo yamesemwa Januari 7,2024 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama wakati akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan katika Ibada Maalum ya Kuwekwa Wakfu Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mufindi mkoani Iringa.

Waziri amehimiza malezi bora kwa watoto na ikiwezekana jamii kurejea utamaduni wa kitanzania wa mtoto kulelewa na kuonywa na jamii nzima inayomzunguka.
Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego (Katikati) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakiwa katika mazungumzo na Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Mhandisi Robert Jitundu (kulia) kabla ya ibada ya kuwekwa Wakfu Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mufindi, Mhashamu Baba Askofu Dkt. Anthony Kipangula.

“Serikali inatambua kuwa Viongozi wa dini wana mchango mkubwa katika kuwahimiza wananchi maadili mema na maisha ya uadilifu,”alifafanua.

Waziri amenukuu maandiko Matakatifu kutoka Waraka wa Mtume Paul kwa Wagalatia Sura ya 6: 1-3 yanayosihi kuonya na pale inapobainika mmoja katika jamii amekwenda kinyume kwa kutenda kosa lolote.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na Askofu wa Jimbo la Mufindi Mhashamu Askofu Dkt. Anthony Kipangula mara baada ya ibada ya kuwekwa wakfu.

Amewaomba viongozi hao kueendelea kutekeleza jukumu hilo ipasavyo ili kulilinda Taifa dhidi ya janga la mmomonyoko wa maadili.

“Tunaamini kwa kupitia Imani yetu na kukua kwa kanisa, ni kukua kwa Imani ya dini, hivyo kutachochea maadili na kusaidia kupambana na vitendo vibaya vya rushwa na kuimarisha utawala bora,”alibainisha.

Aliendelea kusema kuwa, Mambo mazuri yatakayofanywa na washirika wa Dayosisi hiyo yataleta ari na chachu kwa watu wengine ambao sio wanashirika Dayosisi.

Waziri amesema kwamba licha ya Nchi ya Tanzania kutoegemea upande wowote katika masuala ya dini (Secular State) sehemu kubwa ya wananchi wanaamini katika Mungu kupitia dini na madhehebu mbalimbali.
Waumini mbalimbali katika picha wakifuatilia ibada ya kuwekwa wakfu Askofu wa Jimbo la Mufindi Mhashamu Baba Askofu Dkt. Anthony Kipangula na Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Mufindi, Mchungaji Kete Ulula iliyofanyika katika ushirika wa Mafinga.

Aidha, alifafanua kuwa Serikali inaendelea kutambua uwepo wa dini nchini na umuhimu wake katika kulinda tunu za amani na utulivu pamoja na mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za dini katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Waziri ametumia nafasi hiyo kupongeza na kushukuru Kanisa la Kilutheri Tanzania hasa kwa wale waliopata Dayosisi mpya na Mhashamu Askofu Mpya, kuwana matarajio makubwa sana kwa Dayosisi hiyo Mpya.

Kwa upande wake Askofu wa Jimbo la Mufindi, Muhasham Baba Askofu Dkt. Anthony Kipangula, amesema kanisa linahitaji kushirikiana na Serikali kutoa elimu ya kujitegemea ili kusaidia vijana kupata ujuzi.
Mhashamu Askofu wa Jimbo la Mufindi Mhe. Baba Askofu Dkt. Anthony Kipangula akiwa na Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Mufindi, Mchungaji Kete Ulula, katika picha ya pamoja mara baada ya ibada ya kuwekwa wakfu Askofu wa Dayosisi hiyo.

Alisema, Elimu ya Ufundi ni muhimu sana kwa vijana hasa wanaomaliza elimu ya msingi bila kwenda sekondari na wanaomaliza elimu ya sekondari bila kwenda juu zaidi.

“Kanisa linajipanga kuendeleza elimu ya ufundi katika chuo chetu cha Mafinga Lutheran vocation centre ikiwezekana kuanza mchepuo ufundi kama tawi la chuo kikuu kisaidizi cha Iringa,”alisema Baba Askofu.
Mhashamu Baba Askotu Dr. Alex Gehazi Malasusa, Mkuu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania; akimpongeza Mhashamu Askofu wa Jimbo la Mufindi Baba Askofu Dkt. Anthony Kipangula mara baada ya ibada yake ya kuwekwa wakfu.

Akitoa neno la shukrani Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Mhashamu Askofu Dkt. Fredrick Shoo, ameomba Viongozi wanaomsaidia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumsaidia kwa dhati na kuepuka kuunda makundi ya kumkwamisha.

Tunamuombea Mhe. Rais Dkt, Samia Suluhu Hassani na tunamuunga mkono yeye pamoja na wengine wote wenye mamlaka na nafasi katika nchi yetu.
“Tunaomba kila mmoja asimame kikamilifu katika nafasi yake awatumikie watanzania wasasa na vizazi vijavyo,” alifafanua Mhashamu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news