Mhandisi Seff akagua ubovu wa miundombinu ya barabara ya Lengai-Lemkuna-Msitu wa Tembo wilayani Simanjiro

MANYARA-Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amefanya ziara ya kukagua barabara ya Lengai-Lemkuna-Msitu wa Tembo yenye urefu wa Km. 89 wilayani Simanjiro.
Katika ziara hiyo,Mhandisi Seff aliambatana na Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Mhe. Christopher Ole Sendeka na kujionea uharibifu wa barabara hiyo uliosababishwa na mafuriko.

Aidha, Mhandisi Seff amemwagiza Meneja wa TARURA Mkoa wa Manyara kumwelekeza Mkandarasi Afritrust kurudi eneo la kazi ili kuendelea kutekeleza mkataba wake kama alivyoingia.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Mhe. Christopher Ole Sendeka amesema,barabara hizo ni kiungo muhimu kati ya Makao Makuu ya Wilaya ya Simanjiro na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na pia barabara hiyo ni ya kiuchumi na imekua ikiingizia Halmashauri hiyo mapato makubwa kutokana na kusafirisha madini ya mchanga ambapo asilimia kubwa hutumika na wananchi wa wilaya ya Moshi katika ujenzi wa nyumba.
Hata hivyo, Mbunge huyo alimuomba Mtendaji Mkuu kuangalia uwezekano wa TARURA kufanya ujenzi wa barabara tatu za Msitu wa Tembo-Lemkinai-Langai Km. 25, Nabelela-Landanai-Lemkunae pamoja na ufunguzi wa barabara ya Msitu wa Tembo-Naisinyai Km. 20 ili kuweza kuchochea shughuli za kijamii.

Awali Diwani wa Kata ya Msitu wa Tembo Mhe. Keliya Mollel alieleza kwamba eneo hilo lilishakumbwa na mafuriko mengine mwaka 1998 yaliyofika hadi kwenye makazi hivyo aliomba Makalavati zaidi yaongezwe kwenye barabara hiyo ili maji yaweze kutoka kwa urahisi.
Wakati huo huo Meneja wa TARURA Wilaya ya Simanjiro Mhandisi Naftal Chaula ametaja sababu kubwa za kuchelewa kukamilika kwa mradi huo ni kutokana na mafuriko yaliyoharibu kazi zilizokuwa zikifanyika na Mkandarasi na kupelekea kufanya mapitio ya usanifu na kuonekana kuna ongezeko la Makalavati manne(4) ili kuweza kudhibiti maji katika eneo la mradi.

Utekelezaji wa mradi huo ulianza mwaka wa fedha 2023/2024 kwa bajeti kutoka Serikali kuu na utekelezaji wake umefikia asilimia 60.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news