Miaka 60 ya Mapinduzi, Mheshimiwa Luhaga Mpina asema


Luhaga Joelson Mpina (Mb) Mbunge wa Jimbo la Kisesa.

Salamu za Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina kwenye kilele cha sherehe za miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar alipozungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar tarehe 12 Januari, 2024

UTANGULIZI

Ndugu wanahabari, asanteni sana kwa nafasi mliyonipa kuzungumza machache kuhusu tukio hili muhimu la kitaifa.

Nimshukuru sana na kumpongeza Mhe.Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Serikali yake kwa salamu zake ambazo zimesisimua sana halaiki na maandalizi mazuri ya sherehe hizi ambazo zimefana sana.

Pia, niwapongeze waandaaji wa kauli mbiu ya Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 2024 inayosema “Tuimarishe Uchumi, Uzalendo, Amani kwa Maendeleo ya Taifa Letu”.

Kauli mbiu hii imekuja muda muafaka na imekonga mioyo ya Watanzania na ndiyo maana imeshangiliwa sana uwanjani.

Sote tumeshuhudia gwaride la kijeshi lilivyopigwa kwa uhodari mkubwa na majeshi yetu ikiwa ni kielelezo cha uimara na umahiri wa majeshi yetu na kwamba yako tayari kuendelea kulinda Uhuru na Mapinduzi ya nchi yetu na kukabiliana na adui wa aina yoyote wa ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu. HONGERA SANA MAJESHI YETU.

Pia, kwa namna ya kipekee nimshukuru na kumpongeza sana Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kulipa umuhimu mkubwa tukio hili na kutenga muda wa kutosha kushiriki kikamilifu licha ya majukumu makubwa aliyonayo ya kitaifa na kimataifa.

Pia, sherehe hii imekuwa ya kipekee, kwani imehudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi jirani za Uganda, Rwanda, Kenya na Burundi.

Umoja na mshikamano mnaotuonyesha viongozi wetu wa kitaifa na kikanda unatutia nguvu na matumaini zaidi katika kuwatumikia watanzania na wa Afrika kwa ujumla.

Ndugu wanahabari, kama mnavyofahamu leo tumekusanyika hapa katika viwanja vya New Amaan Complex visiwani Zanzibar kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ni siku muhimu sana kwa ndugu zetu Wazanzibar walijitwalia Uhuru wao baada ya kuuangusha utawala wa Sultan kwa njia ya Mapinduzi.

Mapinduzi yaliyoongozwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume na wazalendo wenzake 14 waliokuwa mstari wa mbele kudai Uhuru wa Zanzibar uliopatikana rasmi Januari 12, 1964.

Ndugu wanahabari, hatujasahau na hatutasahau namna Mwasisi wa Mapinduzi, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume na wenzake walivyopigania kuuondoa na kuung’oa ukoloni wa kila aina unaofahamika na usiofahamika na hatimaye kupatikana kwa uhuru wa wananchi wa Zanzibar ambapo pia ilienda pamoja na kukomeshwa kwa dhuluma na unyonge waliofanyiwa wananchi kwa kipindi kirefu.

Wazee wetu hao walijitoa mhanga hadi uhai wao kuhakikisha kuwa wanawakomboa wanyonge kutoka utumwani mwa Sultani na Serikali yake ya kidhalimu.

Hawakuwa na silaha za kisasa wala teknolojia ya kisasa zaidi walitumia silaha za jadi kama vile marungu, mapanga na mishale kufanya Mapinduzi.

Wengine walipoteza maisha, lakini haikuwarudisha nyuma wala kuwakatisha tamaa zaidi ilichochea hamasa ya kuendeleza mapambano. Daima tutaendelea kuenzi mchango wao mkubwa katika Taifa letu.

Hayati Sheikh Abeid Amani Karume mara tu baada ya Mapinduzi kesho yake asubuhi alisafiri kwenda Dar es Salaam kukutana na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Tanganyika wakati huo.

Hii inaonyesha kuwa, viongozi hawa walikuwa na ushirikiano mkubwa na nchi hizi mbili zilikuwa na uhusiano wa karibu hata kabla ya Muungano wa Aprili 1964.Vijana hawa wa kiafrika waliamini kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. 

Ndugu wanahabari, Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Karume mara tu baada ya nchi yetu kupata Uhuru na Mapinduzi kufanyika kwa nyakati tofauti tofauti walionesha kukerwa sana wakikumbuka dhuluma, ubaguzi, ukandamizaji, maonevu na manyanyaso waliyotufanyia wakoloni, wakikumbuka umiliki na uhamishaji wa raslimali za nchi, wakikumbuka namna walivyo wageuza watanzania kuwa watumwa ndani ya nchi yao na wakaligeuza taifa letu kuwa dampo la kuuzia bidhaa zao.

Hapa nanukuu maneno ya Mwalimu Julius Nyerere alisema, “Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha, unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na tupuuzwe. Sasa 4 tunataka Mapinduzi, Mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na tusipuuzwe tena” mwisho wa kunukuu.

Ndugu wanahabari, kwa ujumla waasisi wetu hawa walichukizwa sana utawala wa kikoloni ndiyo maana mara baada tu ya Uhuru walitangaza kutumia nguvu zao zote kukomesha aina zote za dhuluma, wizi, rushwa na ufisadi wa mali za umma.

Waasisi wetu hawa Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume waliamini kuwa kama mambo hayo maovu yataendelea kufanyika katika taifa letu hakutakuwa na maana na Uhuru na Mapinduzi.

Ndugu wanahabari, kutokana na msimamo huo wa waasisi wetu walitangaza maadui watatu wa Taifa letu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini na baadaye likatangazwa Azimio la Arusha mwaka 1967 ambapo pia iliwekwa Miiko ya Viongozi wa Umma ili kukataa dhuluma na kuhakikisha kuwa wizi, rushwa na ufisadi wa mali za umma unakomeshwa nchini. Pia njia kuu zote za uchumi zilirejeshwa mikononi mwa wananchi.


2. TATHMINI YA MAPINDUZI NA UHURU 

Ndugu wanahabari, 

Tunaposherehekea Mapinduzi ni muhimu kufanya tathmini kama Taifa tumeenzi na kulinda maono ya waasisi wetu ya kudai Uhuru na Mapinduzi kama ilivyokusudiwa au tumeenda nje ya malengo?

Ni muhimu kama taifa tufanye tathmini ya mafanikio na changamoto tulizopata katika kipindi cha miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Miaka 62 ya Uhuru wa Taifa letu ili 5 kuweka uelekeo sahihi kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu.

3. MAFANIKIO YALIYOPATIKANA TANGU MAPINDUZI NA UHURU

Ndugu Wanahabari, ni ukweli usiopingika kuwa nchi yetu imepiga hatua kubwa za kimaendeleo katika nyanja mbalimbali Tanzania bara na Zanzibar. Maendeleo na mageuzi makubwa ya Kiuchumi yanaonekana dhahiri, Tanzania inajua, Afrika inajua na Dunia inajua mafanikio tuliyopata.

Baadhi ya mifano ya maeneo machache ni pamoja na:- (i) Ulinzi, Amani, Usalama na mahusiano ya kimataifa Katika kipindi chote cha miaka 62 ya Uhuru na Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar tumeshuhudia nchi yetu ikiendelea kuwa kisiwa cha amani kutokana na uongozi bora na uimara wa vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama.

Tanzania imekuwa nchi ya kupigiwa mfano Duniani kote katika kuitunza na kuilinda amani tunashuhudia majeshi yetu na Viongozi wa nchi yetu wakiteuliwa katika misheni mbalimbali za kimataifa za usuluhishi wa migogoro, kulinda na kurejesha amani katika mataifa mbalimbali Duniani, 

Taifa letu tangu Uhuru limeendelea na msimamo wake kimataifa na sera ya mambo ya nje ya kutofungamana na upande wowote, sera ambayo imeifanya nchi yetu kupata marafiki kila kona ya dunia.

(ii) Utoaji haki na Hali ya Muungano

Muungano wetu umeendelea kuwa imara na kero za muungano zimekuwa zikitatuliwa siku hadi siku tangu awamu ya kwanza hadi sasa awamu ya sita. Mahakama zetu zimeendelea kutoa haki kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria za nchi.

(iii) Uboreshaji wa huduma za jamii elimu, afya na maji

Tumepata mafanikio makubwa katika sekta ya elimu ambapo idadi ya watanzania wanaojua kusoma na kuandika imendeelea kuongezeka huku idadi ya wanafunzi wanaomaliza shule za msingi, sekondari, vyuo na vyuo vikuu ikiongezeka mara dufu huku miundombinu na vifaa vya elimu navyo vikiendelea kuboreshwa.

Kwa kiasi kikubwa adui ujinga tumempiga. Sekta ya Afya tumeshuhudia mageuzi makubwa katika kipindi cha miaka 62 ya Uhuru na miaka 60 ya Mapinduzi zikiendelea kuboreshwa ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za rufaa za mikoa na Hospitali za Rufaa za Kanda hadi kufikia viwango vya ubingwa na kupunguza idadi ya wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Pia kwa kiasi kikubwa adui maradhi tumempiga. 

(iv) Sekta za uzalishaji na miundombinu ya kiuchumi uboreshaji mkubwa umefanyika wa miundombinu ya barabara, madaraja, reli, viwanja vya ndege, meli, ndege, bandari, umeme ambapo imepelekea kupiga hatua kubwa za kiuchumi na maendeleo. Pia uzalishaji umeongezeka katika sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Misitu na wanyamapori.

Raslimali za Taifa kama madini, gesi, mafuta nako tumepiga hatua na kusaidia kwa kiasi kupunguza umasikini.

4. CHANGAMOTO TULIZONAZO BAADA YA UHURU NA MAPINDUZI

Ndugu Wanahabari, Licha ya Mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kipindi cha miaka 62 ya Uhuru na miaka 60 ya Mapinduzi bado hatujafanikiwa kuwapiga na kuwashinda maadui hawa Ujinga, Maradhi na Umasikini kwa asilimia 100.

Nitataja baadhi ya changamoto ambazo zinarudisha nyuma jitihada za nchi yetu kukuza uchumi na kujiletea maendeleo kama ifuatavyo:-

(i) Raslimali za taifa Ardhi, gesi, mafuta, madini, misitu, bandari, wanyama, mazao ya uvuvi nk. kulinufaisha taifa kwa kiwango kidogo sana kutokana na Mikataba Mibovu inayoingiwa na Serikali, kuingia Mikataba ya siri na baadhi ya raslimali za nchi kukabidhiwa wageni kwa mlango wa nyuma kwa kisingizio cha uwekezaji.

Hali hii inaifanya nchi yetu kukosa mapato ya kutosha kugharamia shughuli za maendeleo na kukuza uchumi wa nchi huku raslimali zake zikinufaisha mataifa na makampuni ya kigeni.

(ii) Hatuwezi kujivunia kupambana na umasikini wakati Wizi, Rushwa na Ufisadi umetamalaki nchini, taarifa za wakaguzi zinaonyesha upotevu wa matrilioni ya fedha za umma kila mwaka, mfano Taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022 inaonyesha wizi na ubadhirifu wa fedha za umma zaidi ya Tsh. Trilioni 30 huku Taarifa ya Kitengo cha Udhibiti wa Fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi (FIU) ikionyesha miamala shuku ya zaidi ya Tsh. Trilioni 280.

Kwa mwendo huu hatuwezi kupata fedha za kutosha kugharamia maendeleo ya nchi na kujenga uchumi kwani sehemu kubwa ya fedha za umma zinaporwa na na kumilikiwa binafsi na baadhi ya Viongozi waliopewa dhamana.

(iii) Upande wa Sheria, licha ya Sheria kutungwa na Bunge lakini kumekuwepo na Sheria kandamizi, zinazoleta dhuluma na kurudisha maendeleo nyuma, mfano Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na.5 ya mwaka 2009 inayoruhusu askari wa hifadhi kutumia silaha za moto kwa mwananchi aliyeingia ndani ya hifadhi hata kama hana silaha, hajakataa kukamatwa au pengine anajaribu kukwepa kukamatwa.

Leo tunashuhudia majeruhi na mauaji ya kutisha ya wananchi na mifugo yao kandokando mwa hifadhi. Pia sheria hiyo inaruhusu utaifishaji wa mifugo kwa kukutwa tu ndani ya hifadhi wala si athari zilizosababishwa na mifugo.

Lakini pia tumeshuhudia baadhi ya watumishi wa umma kutoza faini na adhabu nje ya Sheria. Aidha baadhi ya mawaziri wanatunga Sheria ndogo zinazokinzana na Sheria mama na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. hali hii inayopelekea uvunjifu wa amani, dhuluma na maonevu makubwa yaliyopitiliza kwa wananchi wanyonge.

(iv) DPP kuwa na mamlaka ya kuondoa mashtaka Mahakamani wakati wowote hata kama kuna ushahidi unaojitosheleza. Hali inayopelekea kuporwa haki na kufanya dhuluma kwa wananchi.

(v) Ajira za watanzania hazina ulinzi, kuruhusu bidhaa hafifu, bandia, feki na zisizolipa kodi kuingia nchini pamoja na uagizaji holela wa bidhaa kutoka nje ya nchi. Hali inapelekea kuua ajira na viwanda vya ndani.

Pia, zabuni na kandarasi nyingi wanapewa wageni badala ya wazawa wenye fedha zao za kodi, hivi sasa wageni wanapata zaidi ya 61% ya thamani ya zabuni zote zinazotolewa na Serikali.

Pamoja na upendeleo mkubwa unaofanywa kwa wageni wazabuni wazawa wamekuwa hawalipwi kwa wakati jambo linalowafanya kufilisika na kutumbukia kwenye ufukara na umasikini mkubwa. Kitendo hiki kinaua uchumi wa nchi na kuhamisha ajira za watanzania.

(vi) Misamaha na uanzishwaji wa Kodi zisizo na utafiti na tathmini za kina hali inayopelekea kuwa na kodi zisizo 10 na usawa, kandamizi, upotevu wa mapato, kuua ajira na kuchochea umaskini kwa wananchi.

(vii) Kushindwa kukamilisha miradi kwa wakati, miradi iliyoligharimu taifa matrilioni ya fedha na bila sababu za msingi, mfano mradi wa SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere na baadhi ya miradi ya barabara, madaraja na miradi ya maji.

(viii) Wananchi kuuawa na kuporwa mali zao, katika siku za karibuni imekuwa ni jambo la kawaida wananchi kuuwawa na kuporwa mali zao kwa visingizio vya kusimamia sheria za uhifadhi, mfano katika maeneo jirani na hifadhi kunaripotiwa taarifa za wafugaji kuuawa, wanawake kuuawa wakiwa wanakusanya kuni kwenye misitu ya hifadhi.

Wengine Mifugo yao kutaifishwa na kuuzwa kiholela na Serikali na hata wakishinda kesi mahakamani mifugo yao hawarejeshewi.

Haya ni maonevu na dhuluma iliyopitiliza kwa wananchi wetu na ni kinyume kabisa na malengo ya Uhuru na Mapinduzi.

(ix) Wakulima kuuziwa mbegu, dawa na mbolea feki na kwa gharama kubwa. Imekuwa ni jambo la kawaida wananchi kuuziwa mbegu kwa gharama kubwa na bila Maelezo mfano kilo ya mbegu ya mahindi kuuzwa Tsh 10,000 wakati kilo ya mahindi inauzwa Tsh 600. 

Kuuziwa dawa feki za kupulizia mazao zisizoua wadudu 11 na badala yake zinanenepesha wadudu, kuuziwa mbolea kwa bei kubwa na zisizo na ubora hali inayoathiri afya ya udongo na kushuka kwa mavuno ya Wakulima na kuwaingiza kwenye njaa na hasara kubwa.

Pia, kuwepo makato makubwa ya fedha yasiyo na uhalali kwa kisingizio cha ununuzi wa pembejeo mfano Wakulima wa Pamba katika msimu wa kilimo wa 2022 walikatwa kiasi cha Tsh. 400 na mwaka 2023 walikatwa Tsh. 300 kwa kila kilo waliyouza. Makato haya hayana uhalali na ni dhuluma kwa Wakulima.

Bei ya kilo moja ya pamba ni Tsh. 1,360 halafu mkulima anakatwa Tsh. 300 kwa kila kilo moja sawa na 22% kulipia pembejeo kwa maelezo ya aina yoyote suala hili halikubaliki. Badala ya kuwainua Wakulima tunawatia umasikini.

Upande wa Masoko, Masoko ya ndani ya mazao kuhujumiwa na Masoko ya nje kukosa usimamizi hali inayopelekea wakulima kukosa masoko na bei nzuri ya mazao yao na kuendelea kubaki masikini.

(x) Shughuli zingine za Kiuchumi, kuwepo migao na katakata ya umeme isiyo na sababu za msingi, kukosekana kwa dola, riba kubwa za mabenki, kupanda kiholela kwa bei ya nishati ya mafuta na bidhaa zingine muhimu kama mafuta ya kula, ngano, sabuni na vifaa vya ujenzi na kupelekea mfumko mkubwa wa bei na ugumu wa maisha, kuvuruga huduma za jamii na 12 kuharibu uchumi wa nchi.

Hatuwezi kuimarisha uchumi kama kuna usimamizi dhaifu na ufisadi mkubwa kiasi hiki katika maeneo nyeti.

(xi) Kuanzishwa kwa Sera mpya ya elimu ambayo inaruhusu mwanafunzi kusoma kuanzia shule ya awali hadi kidato cha 4 bila kuwepo na mtihani wa taifa uamuzi ambao ni mkakati wa kuua elimu nchini.

Pia kukosekana mikakati madhubuti ya kutengeneza vijana wenye ujuzi mahiri katika fani mbalimbali. Pia hakuna tafiti zinazofanywa kubaini mahitaji ya soko la ajira.

(xii) Baadhi ya Madaktari na wauguzi kuripotiwa kutumia lugha chafu kwa wagonjwa na kutumia maeneo ya huduma za afya za Serikali kama eneo la kukutana na wagonjwa (meeting point) na baadaye kuwahamishia kwenye hospitali zao binafsi ambapo ndiko muda mwingi wanautumia huko.

Vifaa Tiba vilivyoko kwenye hospitali za umma kama MRI, CT–Scan, X-ray nk. kutokufanya kazi kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutofanyiwa matengenezo, kukosa wataalamu na wakati mwingine kuhujumiwa ili kuwezesha hospitali binafsi kupata biashara.

Hali hii inapelekea wagonjwa wengi kukosa matibabu na kupelekea vifo ambavyo vingeweza kuzuilika.

(xiii) Kutokufanyika kwa ukaguzi wa kimatibabu kulingana na vigezo vilivyowekwa na WHO ili kujipima viwango vya 13 ufanisi katika utoaji wa huduma za afya nchini.

Hali hii inapelekea kushindwa kujua ufanisi wa utoaji huduma katika Hospitali za Serikali, kuchochea uzembe na kushindwa kuwajibika kikamilifu kwa mamlaka zinazohusika.

(xiv) Hospitali za Serikali kuacha jukumu lake la msingi na kuanza kufanya kazi za anasa kama kuongeza ukubwa wa makalio badala ya kujishughulisha kikamilifu kutibu maradhi yanayosumbua wananchi. Tunao uhaba mkubwa wa raslimali fedha katika kutatua matatizo ya huduma za afya.

Mfano leo ni zaidi ya miaka 3 tumeshindwa kutoa mtaji kwa MSD wa takribani Tsh. Bilioni 500 kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba kutokana na ukosefu wa fedha. Hizi fedha za kununua mitambo na vifaa vya kuongeza ukubwa wa makalio zimetoka wapi?

(xv) Kuendelea kuripotiwa kwa vifo visivyo na Maelezo kwa wagonjwa hususan akina Mama wajawazito na watoto wakiwa eneo la huduma. Ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika maeneo ya utoaji wa huduma za afya za umma.

Pia zaidi ya vijiji na mitaa 6,000 havina zahanati kote nchini tangu Uhuru jambo linalowafanya wananchi wa maeneo hayo kukosa huduma za afya ya msingi.

HITIMISHO

Ndugu Wanahabari, Wakoloni tuliwang’oa na wakafungasha virago vyao wakaondoka tukashusha bendera yao na kupandisha bendera ya kizalendo kuashiria Uhuru kamili. (Complete Independence).

Leo nani anaendesha dhuluma, nani anaendesha uonevu, wizi, rushwa na ufisadi wa mali za umma mambo ambayo tuliyakataa tangu siku ya kwanza ya kupata Mapinduzi Uhuru wa nchi yetu. ninaamiini sio mwananchi wa kijijini anayefanya haya isipokuwa ni sisi Viongozi tuliopewa dhamana.

Kupitia Kauli mbiu ya Miaka 60 Mapinduzi Zanzibar 2024 inayosema “Tuimarishe Uchumi, Uzalendo, Amani kwa Maendeleo ya Taifa Letu” tukafanye tathmini na kubaini mahala tulipokosea na kurekebisha changamoto zilizopo ili taifa na wananchi waendelee kufurahi na kufaidi matunda ya Mapinduzi na Uhuru kama yalivyokuwa malengo ya waasisi wetu.

Kamwe tusikubali dhuluma, wizi, rushwa na ufisadi kuendelea katika taifa letu na wale wote wanaojihusisha na maovu haya washughulikiwe bila huruma kama sehemu ya kuenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Uhuru wa nchi yetu.

Naamini inawezekana kwani penye nia pana njia, The most frustrating things is not the size of the challenge but the size of the opportunity. 

Asanteni kwa kunisikiliza,

……………………………..
Luhaga Joelson Mpina (Mb) 
Mbunge wa Jimbo la Kisesa

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news