Mshambuliaji wa Leicester City ashirikiana na Clatous Chama kvuruga mipango ya Taifa Stars michuano ya AFCON

IVORY COAST-Mshambuliaji wa Leicester City, Patson Daka dakika ya 88 akimalizia kwa kichwa kona ya kiungo wa Simba ya Tanzania, Clatous Chama amevuruga mipango ya Taifa Stars.
Ni kupitia mchezo wa Kundi F Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) uliopigwa Januari 21,2023 Uwanja wa Laurent Pokou jijini San-Pedro nchini Ivory Coast.

Daka ambaye katika michuano hiyo anaiwakilisha timu ya Taifa ya Zambia (Chipolopolo) aliifanya timu hiyo ambayo ilikuwa imeshafungwa na Taifa Stars kuondoka uwanjani hapo kwa bao 1-1.

Kipindi cha kwanza, Taifa Stars iliuanza vyema mchezo huo na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 11 tu kupitia kwa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Simon Happygod Msuva aliyemalizia pasi ya Nahodha na mshambuliaji wa PAOK ya Ugiriki, Mbwana Ally Samatta.
Vile vile, Zambia ilipata pigo baada ya kiungo wake, Roderick Kabwe anayechezea Sekhukhune United ya Afrika Kusini kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 44 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.

Sare hiyo inaiacha Tanzania mkiani mwa Kundi F kabla ya mchezo wao wa mwisho dhidi ya DR Congo huku Zambia ikibaki nafasi ya tatu.

Zambia huenda ikahitaji ushindi dhidi ya Morocco siku ya Jumanne ili kuendelea hadi hatua ya mtoano baada ya mkwamo huo wa kushangaza.

Wakati huo huo, mechi nyingine ya Kundi F, Morocco pia ilitoa sare ya kufungana bao 1-1 na DR Congo hapo hapo Uwanja wa Laurent Pokou.

Morocco walitangulia kwa bao la beki wa PSG ya Ufaransa, Achraf Hakimi dakika ya sita akimalizia pasi ya kiungo wa Galatasaray ya Uturuki, Hakim Ziyech.

Ni kabla ya mshambuliaji wa Stuttgart ya Ujerumani, Silas Katompa Mvumpa kuisawazishia DR Congo dakika ya 76 akimalizia pasi ya mshambuliaji wa Young Boys ya Uswisi, Meschak Elia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news