Mwinjilisti Temba amuomba Rais Dkt.Samia kusaidia kukwamua ujenzi wa Ngangamfumuni International Bus Stand Terminal mkoani Kilimanjaro

NA DIRAMAKINI

MHUBIRI na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kusaidia kukwamua ujenzi uliokwama kwa muda mrefu wa Stendi Kuu ya Mabasi mkoani Kilimanjaro iliyopo eneo la Ngangamfumuni huko Majengo.
“Ninamuomba Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan aweze kuingilia kati ili aweze kunusuru ahadi ambayo Serikali tangu Awamu ya Tano iliweka.

“Ikizingatia Mama Samia ana kauli mbiu yake ya Kazi iendelee, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia nami ninakuomba uwezeshe kazi iendelee kwenye ujenzi wa Stendi ya Kilimanjaro, Ngangamfumuni pale Majengo.

“Mheshimiwa Rais, mwaka 2024 ni jambo la heri sana kwa stendi hii kukamilika, hivyo kabla ya 2025 iweze kutumika.

“Tuna imani kubwa kabisa kuwa, Serikali italifanyia kazi jambo hili, ikizingatiwa kwamba Rais wetu Mheshimiwa Dkt.Samia ni msikivu mno na anapenda kila eneo nchini lipate maendeleo;

Ameyasema hayo baada ya kufika eneo la Ngangamfumuni Majengo ambako inajengwa Stendi ya Mabasi ya Mkoa wa Kilimanjaro na kushuhudia hatua kubwa iliyofikiwa katika ujenzi huo, ingawa imekwama.

Pia, Temba amefafanua kuwa,wananchi mkoani Kilimanjaro wana shauku kubwa kuwa, mradi huo wa ujenzi unakwenda kukamilika ikiwa pia ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

“Na huu ni mradi ambao tayari umeshatumia gharama kubwa, na hauwezi kuishia hapa ulipo,hivyo niendelee kuwasihi Watanzania na wananchi wa Kilimanjaro kuendelea kuwa wavumilivu na waamini kabisa kwamba, Serikali iko mbioni kumalizia mradi huo na inajali Mkoa wa Kilimanjaro na haujaachwa nyuma,”amefafanua Temba.

Vile vile, Temba amebainisha kuwa, tayari amefunuliwa na Mungu kwamba, mradi huo unakwenda kukamilika kwa viwango bora ili uanze kutoa huduma kwa wananchi wa Kilimanjaro na kutoka maeneo mbalimbali nchini, kwani ujenzi wa jengo la stendi umefikia asilimia 70 ya ujenzi.

Amesema, mradi huo ulisimama kwa muda wa takribani miaka mitatu kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo ya maji ambayo yalikuwa yanatoka chini ya ardhi, lakini yakadhibitiwa.

“Licha ya changamoto hiyo kudhibitiwa, mradi huu ulionekana kuwa kimya kwa muda mrefu, licha ya kwamba zipo ahadi mbalimbali zilizotolewa na Waziri Mkuu pamoja na viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro.

“Kwamba, zingetumwa fedha kwa ajili ya kumalizia mradi huo,lakini kumekuwa na kusuasua kwingi, hivyo kuchelewesha mradi huo kutokamilika.”

Kutokana na hali hiyo, Mwinjilisti Temba amesema, ni shauku ya wananchi wa Kilimanjaro kuona stendi hiyo inakamilika ili iweze kutoa huduma za usafirishaji kwao.

Vile vile, Temba amefafanua kuwa, licha ya stendi hiyo iwapo itakamilika ikaanza kutoa huduma kwa wananchi, pia ni chanzo kikubwa cha mapato kwa Serikali pamoja na kutoa fursa za ajira kwa makundi mbalimbali ya wananchi.

“Kwa hiyo, kukamilika kwa stendi hii kutaifanya Serikali kupata mapato mengi katika mkoa huu wa Kilimanjaro.

“Kwani, Mkoa wa Kilimanjaro una changamoto mbalimbali za barabara kwa ajili ya kupandisha kule milimani na taa za barabarani, hivyo kukamilika kwa mradi huu kutaiwezesha Serikali kukusanya fedha ambazo zitatumika kwa ajili ya kutatua changamoto hizo kwa ajii ya kuupanga mji na kuleta maendeleo,”amefafanua Mwinjilisti Temba.
“Wananchi wa Kilimanjaro wanategemea stendii hii ikamilike na ninaamini kabisa,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, mwaka huu wa 2024 itahakikisha jengo hili la stendi linakamilika.”

Amesema, baada ya kukamilika kwa jingo hilo la kisasa, Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro itaingiza mapato mengi kupitia watu watakaopanga hapo na watakaotumia stendi hiyo.

“Kwa hiyo,tunaiomba ya mkoa na Serikali Kuu ya Mama Samia, itusaidie kukamilisha jengo letu la Stendi ya Mkoa la Ngangamfumuni limalizike.

Ilivyoanza kujengwa

Januari, 2019 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro ilisaini mkataba na Kampuni ya ukandarasi ya Kimataifa ya CRJE (EAST AFRICA LTD) kwa ajili ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mabasi cha Ngangamfumuni.

Ujenzi wa kituo hicho cha Kimataifa cha mabasi cha Ngangamfumuni (Ngangamfumuni International Bus Stand Terminal ) ulianza rasmi Januari 17,2019 mbapo hadi kukamilika mradi huo wa ujenzi ulitarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 27.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi alisema kuwa, ujenzi wa kituo hicho utatekelezwa kwa awamu tatu tofauti huku ukichukua muda wa miaka miwili hadi kukamilika.

Hata hivyo, Mwandezi alisema kuwa, mradi huo mpya wa kituo cha mabasi utaibadilisha manispaa hiyo katika nyanja ya kichumi pamoja na utekelekezaji wa malengo ya Serikali kuhakikisha miradi yake inakamilika kwa wakati.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Moshi, Rayamod Mboya alisema kuwa,ujenzi wa kituo cha Ngangamfumuni ulisubiriwa kwa muda mrefu na wananchi wa Manispaa ya Moshi na wadau wa usafirishaji hivyo kukamilika kwake kutaongeza hadhi pamoja na kutoa fursa ya ajira kwa wakazi wa Manispaa ya Moshi.

Alisema, ujenzi wa kituo hicho cha mabasi utatekelezwa kwa awamu tatu ambapo awamu ya kwanza itakuwa ni kukamilisha eneo la maegesho ili kuweza kuanza kazi ambapo awamu nyingine ni pamoja na kuanza ujenzi wa jengo la ghorofa tano ambalo litakuwa na hoteli,maduka, migahawa pamoja na ofisi mbalimbali.

Kukamilika kwa ujenzi wa kituo kipya cha mabasi cha Ngangamfumuni kutaifanya Manispaa ya kuwa mojawapo ya manispaa zitakazokuwa na kituo ya mabasi chenye ubora zaidi nchini na Ukanda wa Afrika Mashariki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news