Mwinjilisti Temba atoa tamko nzito kuhusu maandamano ya CHADEMA

DAR ES SALAAM-Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba ameshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe kukutana na kufanya mazungunzo ili kusitisha maandamano yaliyopangwa kufanywa na chama hicho cha upinzani nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.  Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo tarehe 09 Mei, 2022.(Picha na Ikulu/Maktaba).

Hayo yanajiri ikiwa Januari 13, 2024 CHADEMA kilitangaza dhamira ya kufanya maandamano Januari 24, 2024 ikishinikiza kuondolewa miswada mitatu ya mabadiliko ya sheria ya uchaguzi.

Aidha, Januari 17, 2024 kilitangaza njia ambayo maandamano hayo yataanzia na kuishia na kulitaarifu Jeshi la Polisi.

Akizungumza leo wakati akieleza maono aliyofunuliwa na Mungu mwaka jana kwamba Tanzania katika miaka 15 hadi 20 ijayo itakuwa imekuwa kiuchumi na kuwa nafasi ya pili kiukuaji barani Afrika baada ya Afrika Kusini inayoshika nafasi ya kwanza, Mwinjilisti Temba amesema, anaamini Rais Dkt. Samia na Mbowe wakikutana na kuzungumza watasaidia nchi kuwa na amani.

"Mimi ninaamini watu hawa wawili (Rais Samia na Mbowe) wakikutana na kuzungumza itakuwa vizuri sana kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

"Na kwa kuwa Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema wazi Rais halazimishwi kupokea ushauri kutoka kwa mtu yeyote wala chama chake, namshauri Rais wangu, Mama yangu Samia Suluhu Hassan atumie fursa hiyo, akutane na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Haikael Mbowe waweke makubaliano yatakayosaidia nchi yetu kuwa na amani.

"Hawa watu wawili ndio wenye nguvu ya kuivusha Tanzania ikawa na amani na hili sio la kubishana.

"Nguvu waliyonayo ndio itasaidia Rais Samia na chama cheke na Mbowe na chama chake hatuwezi kuwadharau na kuingia kwenye mitandao ya kijamii na kuwatukana tukifikiri kwa kufanya hivyo tunawapendezesha wao na Watanzania,"amesema Mwinjilisti Temba.

Pia, ametoa tahadhari kwa Watanzania kwa kuwaeleza kuwa wasifikiri kuwa kutukana na kuendelea kusifia ujinga na upuuzi kwenye mitandao ya kijamii ni jambo jema huku wakiacha hali ya amani ivurugike.

Amesema kuwa,  haitakuwa na maana yoyote kwani Watanzania watashindwa kufanya kazi zao na kutumia muda wao kuwaza, hali hiyo ya maandamano inayoweza kutokea na kuondoa amani na utulivu wa nchi.

"Ninataka nisimame kwa miguu ya wazee wa Tanzania wasioweza kujitetea, nataka nisimame kwa miguu ya watoto wadogo ambao hawawezi kujitetea.

"Nataka nisimame kwenye miguu ya walemavu ambao hawawezi kujitetea, tunahitaji msaada wa Rais Samia, tunahitaji msaada wa Mhe. Mbowe usaidie nchi hii kuwa na amani, hatuhitaji kuwatukana, kuwabeza, hao ni viongozi ambao Mungu ametupa.

"Hatuhitaji kuingia kwenye maisha yao kwa dharau, na yeyote anayefanya, hivyo laana itampiga kwa sababu anakuwa ni sehemu ya kusababisha nchi hii isiwe na amani," ameeleza Mwinjilisti Temba.

Mwinjilisti Temba amesisitiza kuwa, kama Tanzania inahitaji kuwa na amani Serikali haina budi kukubali kufanya mazungumzo na CHADEMA ili kumaliza tofauti zilizopo, kwamba Mungu anataka viongozi wafanye mambo ambayo yataifanya nchi kuendelea kuwa amani.

Katika kusisitiza hilo,  Mwinjilisti Temba amesema kuwa awamu mbalimbali za viongozi wa Serikali zilipita ikiwemo ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Dkt. Jakaya Kikwete, Dkt. John Pombe Magufuli na sasa ni ya Rais Dkt. Samia kwamba na hii itapita na itakuja nyingine na kupita, lakini amani ya nchi ni ya muhimu, kwani Tanzania haitapita mpaka mwisho wa Dunia.

"Hivyo nina simama kwa ajili ya mama Tanzania, sisimami hapa kwa ajili ya chama chochote cha siasa wala mtu yeyote, ninasimama kwa ajili ya Mama Tanzania. 

"Neema ya kutuokoa, pamoja na kuomba, pamoja na kufanya mambo yote tunayotaka kufanya, lazima viongozi hawa wawili tuwaheshimu, lazima tumheshimu Mbowe, tumheshimu Mama Samia na wakae watusaidie kuitengeneza Tanzania hii ili watu wakapone na watu wafurahi," amesisitiza Mwinjilisti Temba.

Mwinjilisti Temba akizungumzia maono ya Tanzania kuwa na uchumi mkubwa miaka 15 hadi 20 ijayo, amesema ili iweze kufikia hatua hiyo hakuna budi nchi kuwa na amani na utulivu ambao utashawishi na kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini.

Amesema kwamba, hakuna wawekezaji ambao wanaweza kuja kuwekeza na kujenga viwanda vyao katika nchi ambayo ina maandamano yasiyo na ukomo na hata waliopo wanaweza kukimbia na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi ndio maana anahimiza mazungumo ya viongozi hao wawili ili kuweka utulivu wa kuwashawishi wawekezaji kuwekeza nchini na hatimaye kusukuma ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

"Imani yangu ni kwamba haya yakifanyika (Rais Samia na Mbowe kukutana na kufanya mazungumzo) baada ya miaka 20 ijayo Tanzania itakuwa na uchumi mkubwa kwani wawekezaji wengi watakuja.

"Tanzania itakuwa ni nchi ya kukimbilia, Tanzania itakuwa ni nchi ya furaha na Tanzania itakuwa ni nchi ya mafanikio," amesema Mwinjilisti Temba.

Akiendelea kufafanua juu ya uchumi kukua baada ya miaka 20 ijayo, Mwinjilisti Temba amesema kuwa ni kutokana na Viwanda vinajengwa kwa mamia nchini.

Amebainisha kwamba, itafika kipindi hicho mataifa ya jirani na Watanzania hawatalazimika tena kwenda China kufunga wala kuagiza mizigo na badala yake watapata mizigo yote nchini hivyo kukuza pato la ndani na ustawi wa nchi.

"Ndiyo maana kwa maono hayo Mungu alinionyesha uchumi utakua sana mbeleni hivyo lazima Serikali ilinde misingi ya ukuaji wa kiuchumi ikiwepo nguzo kubwa ya Amani na mshikamano kama nchi.

"Maandamano yasiyo na Kikomo yanafifisha uchumi na kuwafanya wawekezaji kutokutumia mitaji yao kuwekeza na manunguniko ya maandamano ndiyo mabaya zaidi kuliko hata wangeruhusiwa waandamane,"amesema Mwinjilisti Temba.

Katika hatua nyingine, Mwinjilisti Temba ametoa onyo kwa vyama 13 vya siasa na makundi mbalimbali ya watu yaliyoibuka na kutoa matamko ya kumshambulia Mbowe na chama chake kwa dhamira yao ya kufanya maandamano ya Januari 24, mwaka huu, akieleza kuwa jambo hilo halina faida kwa nchi bali linachochea chuki.

"Niseme tu wazi katika hili nasimama kuitetea nchi na si vinginevyo ni kweli vitu vimepanda bei sana, tena kila mtu anapanga bei ya vitu atakavyo na nauli za Mabasi wanapanga watakavyo mfano Desemba, mwaka jana nauli za kwenda Moshi zilifika hadi shilingi 80,000 pale Mbezi na Dodoma 50,000 na Polis waliona, lakini walishindwa kushugulikia," amebainisha Mwinjilisti Temba na kuongeza.

"Na watu wengi walipata shida hususani wanafunzi na watu waliokwenda likizo, leo tunaona viongozi wa vyama vya siasa wakipambana na maandamano huku wakijichanganya kuwa huo muswada siyo mzuri watatoa maoni yao baadaye ama kuandamana au la, sasa hivi nchi hii nani mtoto au kwa nini hatumuheshimu Mungu je mnataka laana ya vilio vya watu?".

Mwinjlisti Temba ameshangazwa na viongozi wa vyama hivyo vya siasa kutokueleza juhudi walizofanya za kukaa na CHADEMA na kutafuta muafaka badala yake wanakuja kwa Watanzania na kulalamika huku vikundi vya machinga na bodaboda nao wakifanya hivyo hivyo kupinga mahandamano hayo ambayo yapo Kikatiba.

"Mbona hamtaki maandamano yafutwe katika hiyo Katiba, tuache unafiki msimchezee Mungu Biblia ilimwonyesha Mfalme Sauli alivyo mdhiaki Mungu katika Uongozi wake akaishia pabaya. 

"Hivyo Serikali ina dhamana kutoka kwa Mungu, pili wanadamu wawe na mijadala ya haki maana Biblia inasema haki huinua Taifa. Kinachofanyika kitasababisha hasira ya Mungu kuongezeka katika Taifa letu.

"Wakati Yesu anazaliwa Mfalme Herode alianza kuua watoto wachanga akiwa amemlenga kumuua Yesu, hivyo Mfalme aliua, ndipo Malaika akamwambia Yusufu amkimbize Mtoto Misri kujificha, baada ya muda Malaika akamrudia na kumwambia mrudishe mtoto (Yesu) kwa kuwa waliotaka uhai wa mtoto wote walikwisha kufa,"amesema Mwinjilisti Temba.

Anasema, katika kizazi cha leo watumishi wa Mungu wa kweli wanaokemea uovu hata kama unafanywa na baba zao wazazi ni wachache, kwani wengi wao hufumbia macho kwa lugha ya kwamba wataombea nchi huku wakijua uovu usiotubiwa hauwezi kuombewa.

"Tunajua Watanzania wanaendelea kuwadharau watu ama viongozi wanaotanguliza maslahi yao, kuwapendeza wanadamu na kuacha kumpendeza Mungu ni laana kubwa sana inayoweza kusababisha kizazi chako kuwa katika mahangaiko, tuijenge nchi pamoja na Mungu atatusaidia," anaongeza Muhubiri wa Kimataifa Mwinjilisti Temba.

Mwinjiliti Temba amewaomba Watanzania wamfuatilie vizuri katika unabii alioutoa usiku wa mwaka mpya ili wajue nini Mungu alimfunulia juu ya Tanzania kwani alieleza hazarani.Utabiri wa Mwinjilisti Temba, bofya hapa kuusoma>>>

"Tena nikasema mtaweza kuyapuuzia, unabii wangu kabla haujatimia Mungu ataleta watumishi wengine wakiwepo kutoka nje ya nchi kutoa unabii juu ya Tanzania na yote yametimia. Nabii nyingi zimejirudia, yote niliyoyasema yametimia na yanaendelea kutimia.

"Je, hatujiulizi viongozi wetu wanakuja hadharani katika mikutano ya hadhara na kuahidi magreda kutengeneza barabara zote wiki ijayo mfano kule Jimbo la Kawe na siku inayofuata Mungu kashusha mvua kubwa kama siku zote, lakini nyumba nyingi zimesombwa na maji.

"Tukawasikia watu wakishuhudia kuokota magari na baadhi kusombwa na maji hadi kung'ang'ania kwenye miti iliyoko mitoni, kwa mara ya kwanza barabara imekatika katikati, mali na watu kupotea hata hili hamuoni Mungu ameanza kazi na Tanzania?," amesema Mwinjilisti Temba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news