Salamu za Jumapili: Ndugu uwe mwaminifu

NA LWAGA MWAMBANDE

UKIREJEA katika maandiko ya neno la Mungu hususani kupitia Biblia Takatifu utabaini kuwa, uaminifu ni mojawapo ya tunda la Roho.
PICHA na zackjamescole.wordpress.com

Katika neno lake, Mungu amesema atatimiza yale aliyoahidi katika neno lake, si tu kwa wana wa Israel bali kwa watu wote wanaoishi sawasawa na neno lake.

Kwa hiyo, kwa upande wetu inatupasa sisi nasi kuwa waaminifu kwa kuliishi na kulitenda neno la Mungu.

Ndiyo maana ukisoma Kumbukumbu la Torati 7:9,12 neno la Mungu linasema, "Basi jueni Bwana, Mungu wenu, ndiye Mungu, Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu.

"Na itakuwa, kwa sababu mwazisikiliza hukumu hizi, na kuzishika na kuzitenda, basi Bwana, Mungu wako, atakutimizia agano na rehema aliyowaapia baba zako.

"Ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu halitanirudia bure bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma."

Zingatia kwamba, ntu aliye mwaminifu ni yule ambaye anatenda sawasawa na maagizo, sheria na taratibu.

Rejea Mathayo 24:45-46 neno la Mungu linasena, "Ni nani basi mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimuweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo."

Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande anasema kuwa, ukiwa mwaminifu kwa kile kidogo kitu, Mungu ataachilia baraka zaidi kwako. Endelea;

1.Ndugu uwe mwaminifu, kwa kile kidogo kitu,
Neno latutaarifu, huyo hasa ndiye mtu,
Mungu asiyemkifu, hata kwa kikubwa kitu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

2.Mtu aliye dhalimu, kwa kile kidogo kitu,
Mungu naye hana hamu, kwa makubwa yalo kwatu,
Atabaki humuhumu, huku kijilaumu tu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

3.Si mwaminifu madogo, na hata kwa makubwa tu,
Wewe mtu ni mzigo, huwezi kupendwa katu,
Utakaa kama gogo, lile lisofaa kitu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

4.Mkumbuke Naamani, jemedari yule mtu,
Ila ukomo mwilini, ulidhalilisha utu,
Kijakazi wa nyumbani, ndiye alisema kitu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

5.Alivyomsikiliza, kweli akafanya kitu,
Mwenye akajisogeza, kwa yule wa Mungu mtu,
Huko akajieleza, mwili ulivyo na kutu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

6.Naamani kaambiwa, jambo lililo dogo tu,
Na wala si kuchajiwa, ya kwamba atoe kitu,
Ni kama alizomewa, na hakuelewa kitu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

7.Eti kujitumbukiza, kwenye mto Yordani tu,
Mara saba akiweza, utatoka ukurutu,
Hilo ndo lilimkwaza, kwamba eti mtoni tu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

8.Alitaka kuondoka, kwamba aende kwao tu,
Mito kwao inawaka, maji yake mazuri tu,
Kwa alivyokasirika, iliwapa kazi watu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

9.Vile alishawishiwa, ya kwamba ajichovye tu,
Ushauri kusikiwa, akaamua kwenda tu,
Mara saba kawa sawa, mwili ukarudi kwatu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

10.Kujichovya jambo dogo, kama waambiwa mtu,
Ukijiona kigogo, kuthamini wako utu,
Hapo ipokee logo, huwezi kupata kitu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

11.Liwe some kwetu sote, tufanye mambo kiutu,
Mungu wetu sisi sote, mara hutokea kwetu,
Ili neema tupate, njia zake nyepesi tu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

12.Hayo tukiyadharau, kwamba ni kawaida tu,
Tukitaka angalau, mambo ya ajabu kwetu,
Majibu kwetu ni kau, mwisho tutakuwa butu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo tunainuliwa.

13.Madogo kiaminiwa, utambue Mungu wetu,
Makubwa taaminiwa, jinsi waonesha utu,
Huko ni kuinuliwa, hadhi pia wako utu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

14.Unapewa ushemasi, unaona siyo kitu,
Kwamba huo kwako hasi, ujionavyo ni mtu,
Hata unazua kesi, kwamba hawafai watu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

15.Wataka uaskofu, roho yako iwe kwatu,
Jua Mungu wamkifu, na tena hupati kitu,
Huo wako utukufu, kwake Mungu siyo kitu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

16.Mungu atusaidie, katika maisha yetu,
Muumba tumsikie, jinsi anafanya kwetu,
Na vema tufwatilie, siyo kwa akili zetu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.

17.Kubali mambo manyonge, uyafanye kwa moyo tu,
Na kesho mbele usonge, vema tajulikana tu,
Kutii Neno jipange, huwezi kufeli katu,
Kwa hayo mambo madogo, ndivyo unainuliwa.
(Luka 16:10, 2 Wafalme 5:1-14)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news