Palilia Familia

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, familia bora ndiyo kitovu cha maendeleo, furaha na kwa jumla ustawi wa maisha.
Vile vile, familia ni mahali ambako watoto hujifunza umoja na upendo miongoni mwao.

Ndiyo maana familia zina wajibu wa kuhakikisha ziko salama, zina afya njema, elimu, zinahudumia wazee, zinaimarika kiroho na zinakuwa na upendo.

Familia yenye umoja inakuwa na upendo wa Mungu, na ni alama ya Utatu Mtakatifu na kwa hakika upendo wa Mungu kwa ubinadamu huonekana.

Ingawa dhana ya familia inaweza kuonekana kuwa rahisi, matendo ya binadamu yameifanya kuwa ngumu zaidi.

Ndiyo maana suala la familia linapewa kipaumbele. Kuna Siku ya Familia Duniani ambayo huadhimishwa Mei 15 kila mwaka na kanisa pia lina Siku ya Familia.

Familia si jambo dogo, bali ni jambo linalostahili kuheshimiwa na jamii na watu duniani kote.

Familia ni msingi, ndipo mtu huzaliwa, hutunzwa, hulelewa na kufundishwa tunu za kimaadili na kiroho ambazo ndiyo msingi wa maisha ya mtu.

Kama mtu ana msingi imara kimaadili na kiroho atafaulu mambo mengi maishani mwake.

Lakini kama anakosa tunu hizi pengine hata akiwa na kisomo kiasi gani anaweza asifanikiwe.

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,kila mmoja wetu ana wajibu wa kupalilia familia ili kuendeleza maisha. Endelea;

1.Mamlaka nazo pesa, ni matunda ya maisha,
Matunda ukiyakosa, yaendelea maisha,
Familia ndiyo hasa, mzizi unaotosha,
Palilia familia, tuendeleze maisha.

2.Mti pasipo mizizi, kamwe hauna maisha,
Familia ni mzizi, unaojenga maisha,
Yahitaji mandalizi, kuendeleza maisha,
Palilia familia, tuendeleze maisha.

3.Familia baba mama, kwa sehemu wanatosha,
Baraka pia ni njema, watoto kujumlisha,
Jinsi waishivyo vema, twaendeleza maisha,
Palilia familia, tuendeleze maisha.

4.Hawa na yeye Adamu, ndio mwanzo wa maisha,
Sisi hapa tunadumu, walidumisha maisha,
Mume mke wakidumu, dunia haitakwisha,
Palilia familia, tuendeleze maisha.

5.Tukitunza familia, maelewano yatosha,
Watoto kituzalia, yaendelea maisha,
Wazazi wakiishia, familia taanzisha,
Palilia familia, tuendeleze maisha.

6.Maelewano nyumbani, vema tukiyazidisha,
Wayajue ya shuleni, kutoa kujumlisha,
Na baadaye kazini, mali wakiizalisha,
Palilia familia, tuendeleze maisha.

7.Familia mume mke, kusiwepo kupotosha,
Mti na uongezeke, kwa matunda kuzalisha,
Ndoa jinsi moja teke, dunia isije kwisha,
Palilia familia, tuendeleze maisha.

8.Kama familia poa, watoto watafundisha,
Wakikua wawe poa, waendeleze maisha,
Akija wa kubomoa, hao watamkomesha,
Palilia familia, tuendeleze maisha.

9.Naombea familia, maisha yawe tamasha,
Mambo zinajifanyia, yawe ni ya kuzalisha,
Mbele Mungu tangulia, wapate ya kuridhisha,
Palilia familia, tuendeleze maisha.

Lwaga Mwambande
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news