Utaburudika sana

NA LWAGA MWAMBANDE

KWA mujibu wa makala iliyoandaliwa na Afisa Habari wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Albano Midelo mwaka 2018 ilifafanua kuwa,Ziwa Nyasa ni miongoni mwa maziwa yenye upkee wake duniani.
Muonekano wa Matema Beach. Picha na Visit Tanzania).

Ziwa Nyasa linapita katika wilaya za Nyasa mkoani Ruvuma,Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe na Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya’

Alibaibisha kuwa, utafiti ulibaini kuwa Ziwa Nyasa lina aina zaidi ya 400 za samaki wa mapambo ambao hawapatikani katika maziwa, mito na bahari sehemu nyingine yeyote katika sayari ya Dunia.

Tafiti zinaonesha kuwa, katika sayari inayoitwa Dunia,hakuna ziwa lenye samaki wa mapambo aina zaidi ya 400 badala yake ni Ziwa Nyasa pekee.

Ni ziwa ambalo pia linaongoza duniani kwa kuwa na viumbe wengi katika maziwa yenye maji baridi pia ziwa hilo linaongoza kwa kuwa na maji maangavu.

Kulingana na utafiti ambao ulifanywa na Jumuiya ya Maendeleo nchi zilizo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kushirikiana na nchi ya Uingereza kwenye Ziwa Nyasa kati ya mwaka 1991 hadi 1994 na mwaka 1996 hadi 2000 ulionesha kuwa,ziwa hilo lina kiasi cha tani 165,000 za samaki na kati ya kiasi hicho tani 35,000 za samaki.Ziwa Nyasa lina aina 1,500 za samaki.

Ziwa Nyasa limezungukwa na nchi tatu ambazo ni Tanzania,Malawi na Msumbiji.Ziwa hilo lipo kwenye usawa wa mita 500 toka usawa wa bahari ambapo kina cha ziwa hilo ni karibu mita 750,urefu wake ni karibu kilomita 1000, upana mkubwa ni kilomita 80 na upana mdogo ni kilomita 15.

Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa nchini ambayo imejaliwa kuwa na maeneo ya hifadhi na vivutio vizuri vya utalii kama vile Makumbusho ya Taifa ya Majimaji, Mapango ya Chandamali,majengo ya kihistoria Peramiho, samaki wa mapambo, fukwe na visiwa katika Ziwa Nyasa.

Vivutio vingine ni maeneo ya wapigania uhuru nchi za Kusini mwa Afrika,mapori ya wanyamapori ya Liparamba, Selous, Litumbandyosi na misitu ya asili ukiwemo msitu katika milima ya Matogoro ambao ni chanzo cha Mto Ruvuma unaomwaga maji yake Bahari ya Hindi.

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anabainisha kuwa,licha ya ziwa hilo kuwa na vitu adimu duniani, pia fukwe za Ziwa Nyasa ni za namna yake. Endelea;

1.Huu utajiri wetu, fukwe zake Ziwa Nyasa,
Mchanga hauna kutu, kupumzika hamasa,
Kuogelea ni zetu, sisi watu wa kisasa,
Kifika Matema Beach, utaburudika sana.

2.Maji ya ziwa nasema, kweli yapendeza hasa,
Humo ndani ukizama, mchanga mweupe hasa,
Mawimbi ukitazama, kweli yananesa nesa,
Kifika Matema Beach, utaburudika sana.

3.Samaki kila aina, wanameremeta hasa,
Tena ni watamu sana, hasa mbelele na mbasa,
Ukila utajikuna, na ubwabwa wa kisasa,
Kifika Matema Beach, utaburudika sana.

4.Ni mkubwa ukarimu, wakazi wa Ziwa Nyasa,
Kiwa huko utadumu, na Wanyaki na Wanyasa,
Tena wana ufahamu, wa uvuvi wa kisasa,
Kifika Matema Beach, utaburudika sana.

5.Kwa utalii wa ndani, Nyasa fukwe za kisasa,
Taogelea majini, na kuburudika hasa,
Hata mawazo kichwani, mchanga tayatakasa,
Kifika Matema Beach, utaburudika sana.

6.Kwafikika kirahisi, barabara ya kisasa,
Na tena kuna mabasi, hata kibeba lumbesa,
Jitafutie nafasi, tembelea Ziwa Nyasa,
Kifika Matema Beach, utaburudika sana.

7.Matema sehemu moja, utajiri Ziwa Nyasa,
Itunge nayo ni moja, nako mpya ukurasa,
Sikae sehemu moja, changamkia fursa,
Kifika Matema Beach, utaburudika sana.

8.Mbamba Bay sijasema, ni bandari ya kisasa,
Meli hakuna kukwama, ni mpya na za kisasa,
Serikali yetu njema, inajali Ziwa Nyasa,
Kifika Matema Beach, utaburudika sana.

9.Tanzania nchi njema, vivutio vya kisasa,
Ramani ukiisoma, maziwa makubwa hasa,
Tanganyika ya Kigoma, Victoria yetu hasa,
Kifika Matema Beach, utaburudika sana.

10.Hoteli utazikuta, na chakula cha kisasa,
Tamaduni tazikuta, zinazotoa hamasa,
Na minazi taikuta, ni kama uko Mombasa,
Kifika Matema Beach, utaburudika sana.

Lwaga Mwambande
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news