Serikali yasaini mikataba uwekezaji SWICA

NA HAPPINESS SHAYO

WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imetia saini mikataba sita ya uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Uwekezaji wa Wanyamapori (Special Wildife Investment Concession Areas - SWICA) yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 278, sawa na shilingi za kitanzania Bilioni 696 kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya utalii katika maeneo sita ya uwekezaji.
Maeneo hayo ya uwekezaji ni Pori la Akiba Mkungunero Mkoani Dodoma, Mapori ya Akiba ya Ikorongo na Grumet Mkoani Mara pamoja na Mapori ya Akiba ya Maswa Kimali, Maswa Mbono na Maswa Kaskazini yaliyopo Mkoani Simiyu.

Hafla ya utiaji saini imefanyika leo Januari 3, 2024 katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema utekelezaji wa SWICA utaongeza utalii na mapato katika maeneo yatakayofanyiwa uwekezaji huo, hali itakayochangia kwa kiasi kikubwa kutekeleza lengo la kuongeza idadi ya watalii kutoka milioni 1.5 mwaka 2021/2022 hadi milioni 5 mwaka 2025/2026.

“Uwekezaji huu utaiingizia Serikali mapato yanayokadiriwa kufikia dola za Kimarekani milioni 314 katika kipindi cha miaka 20 ya uwekezaji sawa na dola milioni 16 kwa mwaka (sawa na shilingi za kitanzania bilioni 40). Mafanikio haya yanatokana kwa kiasi kikubwa na utangazaji utalii kupitia Filamu ya “Tanzania- The Royal Tour” iliyoandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,"amesisitiza Mhe. Kairuki.
Ameongeza kuwa miongoni mwa manufaa mengine yatakayopatikana kutokana na uwekezaji huo ni kuimarika kwa uhifadhi, utafiti na kuboresha maisha ya jamii zinazozunguka maeneo ya uwekezaji ambapo takribani dola za Kimarekani milioni 50, sawa na shilingi za kitanzania bilioni 125, zitatumika kufadhili Miradi ya Maendeleo ya Jamii katika kipindi cha miaka 20 ya uwekezaji.

Aidha, amezipongeza kampuni za Bushman Safari Trackers Ltd, Grumeti Reserves Ltd, Mwiba Holdings Ltd na Magellan General Trading LLC kwa kufanikiwa kusaini mikataba ya uwekezaji mahiri.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwindaji ya Bushman Safari Trackers Ltd, Talal Abood amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake binafsi za kukuza utalii na kushirikisha sekta binafsi kwa lengo la kukuza uchumi wa Tanzania.
“Tunaishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ushirikiano na tunaahidi kwamba tunaenda kutekeleza hili jambo kwa ufanisi mkubwa na uharaka mkubwa ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita kwenye kutekeleza Sera ya Utalii,” amesema Bw. Talal.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb), Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko, Makamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya Uhifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), baadhi ya watendaji na maafisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na TAWA pamoja na wadau mbalimbali wa uhifadhi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news