Siyo dakika tisini,mpira unarudiwa tena

NA LWAGA MWAMBANDE

TIMU ya Genk kutoka Ubelgiji imeshinda rufaa dhidi ya makosa ya Refa Msaidizi wa Video (VAR) wakati wa mechi na Anderlecht.

Uamuzi huo wa kihistoria unakuja ikiwa ni takribani mwezi mmoja umepita baada ya Anderlecht kushinda mabao 2-1.
Shirikisho la Soka la Ubelgiji limeamua mechi ya raundi ya 19 ya michuano ya Ligi Kuu ya Ubelgiji dhidhi ya Anderlecht na Genk irudiwe kwa sababu ya makosa yaliyofanywa wakati wa kutumia mfumo wa VAR.(Picha na dynamo).

Kupitia mtanange huo ambao ulipigwa Desemba 23,2023 katika dimba la Lotto Park, baada ya kujiridhisha Baraza la Nidhamu la Mpira wa Miguu nchini Ubelgiji limeidhinisha rufaa ya Genk ya kurudia mechi hiyo dhidi ya Anderlecht.

Genk iliwasilisha malalamiko kwenye Idara ya Waamuzi baada ya kupata bao la dakika za mwisho lililokataliwa na VAR kwa kuotea.

Hayo yanajiri huku Anderlecht wakiwa wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji, na Genk wakiwa nafasi ya tano.

Tarehe ya mechi hiyo ya marudio inatarajiwa kutangazwa baadaye. Mara nyingi, uamuzi wa nadra wa kurejesha mechi kwa ukamilifu huangazia masuala ya teknolojia ya VAR na huzua shaka kuhusu maamuzi ya refa yaliyofanywa kwa usaidizi wake.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema uamuzi huu wa Ubelgiji yafaa ufike na Tanzania. Endelea;

1.Siyo dakika tisini, mpira unarudiwa,
Sheria za kizamani, kwamba unamaliziwa,
Palepale kiwanjani, huku watu wakosewa,
Yale ya Ubelgiji, bora na kwetu yafike.

2.Umeshachezwa mpira, ligi inashindaniwa,
Penati ikawa kura, timu moja kapatiwa,
Mepanguliwa mpira, kwa mwingine kazidiwa,
Yale ya Ubelgiji, bora na kwetu yafike.

3.VAR ilipoingilia, goli likakataliwa,
Kwamba alomalizia, penati liingiliwa,
Hadi mwisho kuishia, washindi walopigiwa,
Yale ya Ubelgiji, bora na kwetu yafike.

4.Baraza likachunguza, penati kukataliwa,
Kumaliza kuchunguza, vizuri likaelewa,
Kosa walilopuuza, mchezo meharibiwa,
Yale ya Ubelgiji, bora na kwetu yafike.

5.Badala kuwa adhabu, penati walopatiwa,
Kwamba mtu liharibu, penati kuingiliwa,
Wapo walioharibu, penati walopigiwa,
Yale ya Ubelgiji, bora na kwetu yafike.

6.Miguu kumi na nane, penati ikitolewa,
Wasiingie wengine, sheria zajaribiwa,
Waliingia wengine, kile hakikutakiwa,
Yale ya Ubelgiji, bora na kwetu yafike.

7.Kosa ni la kisheria, adhabu waliopewa,
VAR wangeitumia, kwa penati kurudiwa,
Hili walipuuzia, baada kufwatiliwa,
Yale ya Ubelgiji, bora na kwetu yafike.

8.Wa penati kuonewa, mchezo unarudiwa,
Hivi hapo mwaelewa, ya VAR yapinguliwa,
Tisini limaliziwa, wengine kushangiliwa,
Yale ya Ubelgiji, bora na kwetu yafike.

9.Refa kifanya makosa, hata timu kuonewa,
Matokeo wakakosa, kule kusababishiwa,
Kurudia iwe ruksa, haki waweze tendewa,
Yale ya Ubelgiji, bora na kwetu yafike.

10.Tatizo kubwa la VARI, na watu inatumiwa,
Picha wanazihariri, wengine kufanikiwa,
Kwa wengine si vizuri, jinsi wanavyoonewa,
Yale ya Ubelgiji, bora na kwetu yafike.

11.Tunao mwarobaini, mechi iweze rudiwa,
VARi wakiwa makini, haya tutaepushiwa,
Viwango vikiwa chini, mechi zizidi rudiwa,
Yale ya Ubelgiji, bora na kwetu yafike.

12.Kwa michezo ya Afconi, VARi wamefanikiwa,
Jinsi walivyo makini, kwa kweli tunavutiwa,
Ulaya huko igeni, muache kulalamikiwa,
Yale ya Ubelgiji, bora na kwetu yafike.

13.Mpira jasho na damu, wakicheza latolewa,
VARi isiwe ni sumu, moja timu kuonewa,
Haki ni vema idumu, itazidi shangiliwa,
Yale ya ubelgiji, bora na kwetu yafike.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news