Tanzania yatoa msisitizo Mattei Plan

ROME-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. January Makamba (Mb.) ambaye anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia amesisitiza umuhimu wa mpango wa Mattei kuzingatia mahitaji sahihi ya Afrika ili uweze kuleta matokeo stahiki barani Afrika.
Mheshimiwa Makamba alieleza kuwa mpango huo ukizingatia mahitaji stahiki ya Afrika changamoto nyingi zinazokabili nchi zilizoendelea zinazosababishwa na ukosefu wa maendeleo barani Afrika zitaondoka.

Awali akihutubia katika mkutano wa Nne wa Italia-Afrika, Waziri Mkuu wa Italia, Mhe. Giorgia Meloni amesema,mpango wa Mattei utagusa masuala ya usalama wa nishati na matumizi ya nishati mbadala, maendeleo ya miundombinu, usalama wa chakula, elimu na mafunzo ya ufundi pamoja na kupambana na wahamiaji haramu.

Serikali ya Italia inatarajia kushiriki kwa kiasi kikubwa kukuza maendeleo barani Afrika kwa kupitia Mpango wake Mpya wa Mattei.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat ameomba Afrika ipewe muda wa kuchanganua Mpango wa Mattei kwanza kabla ya kuanza utekelezaji wa mpango huo.

"Tunahitaji kubadilisha maneno kuwa vitendo kwa sababu ni vyema tukajadiliana na kuona ni njia gani zinatumika kutekeleza miradi inayopendekezwa katika Mpango wa Mattei ili kuepuka kuwa na furaha na ahadi ambazo hazitekelezwi,” amesema Mahamat.
Viongozi wakuu wa baadhi ya nchi za Afrika; mawaziri, maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa, wawakilishi kutoka taasisi na mashirika ya kimataifa wafanyabiashara pamoja na mashirika ya kifedha wameshiriki mkutano huo unaoendelea Roma, Italia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news