Waziri Mkuu afanya ziara ofisi za RUWASA, atoa maagizo kwa Waziri Aweso

LINDI-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Maji Jumaa Aweso kufika katika ofisi za Wakala wa Maji na usafi Mazingira Vijijini Mkoa wa Lindi (RUWASA) na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Lindi (LUWASA) kufuatilia mapungufu yaliyopo ikiwemo kutotumika kwa gari la uchimbaji visima lililotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu Juni, 2023 ili kuwezesha uchimbaji wa visima vya maji.
“Hii wizara ina Waziri makini sana, mnafanya vitu kwa ufichouficho, sasa Waziri aje hapa, mnamuona anavyohangaika Waziri wenu, vitu vidogo vidogo hivi mpaka waziri aje na ninyi mpo, kwanini mpo hapa,” Waziri Mkuu alisisitiza na kuongeza kuwa anahitaji taarifa ya kwa nini mashine hiyo tangu imefika haijachimba kisima hata kimoja.

Ametoa agizo hilo Januari 8, 2024, baada ya kufanya ziara katika ofisi za RUWASA zilizopo Manispaa ya Lindi na kushuhudia mtambo wa kuchimba visima ukiwa umeegeshwa na hakuna kisima kilichochimbwa tangu ulipotolewa mwaka jana huku katika mikoa mingine iliyopewa mtambo kama huo visima vinachimbwa kama ilivyokusudiwa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alihoji sababu ya kutotumika kwa pikipiki zilizonunuliwa na RUWASA Mkoa wa Lindi tangu mwaka 2021 kwa ajili ya kuzigawa kwa jumuiya za watumia maji kwa madai kuwa bado hazijapata usajili. “Huu ni uzembe haiwezekani fedha za wananchi zinapotea nyie mpo tu. Hizi pikipiki zimeanza kuharibika.”

Akizungumzia kuhusu pikipiki hizo Afisa Manunuzi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Mkoa wa Lindi (RUWASA) Bw. Kenedy Mbagwa alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakifuatilia suala la vibali vya kutumia pikipiki hizo kutoka makao Makuu ya RUWASA bila ya mafanikio, ambapo Waziri Mkuu baada ya kupata maelezo hayo amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Lindi afuatilie suala hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news