Huduma ndogo za fedha zina mchango mkubwa katika uchumi-BoT

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 imelenga kubadilisha mazingira kwa watoa huduma za fedha nchini ili waweze kushiriki kikamilifu kuwezesha Watanzania vijijini na mijini kujikwamua kiuchumi.
Hayo yamesemwa leo Februari 14, 2024 jijini Zanzibar na Naibu Gavana wa Sera za Uchumi na Fedha wa BoT, Dkt.Yamungu Kayandabila wakati akifungua semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari za uchumi nchini.

“Lakini, tutakuwa na jambo la pili kuhusu Sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha (2018), ambapo Benki Kuu ilipewa jukumu la kuisimamia sekta hiyo ndogo ya fedha.

“Huduma hizi ndogo za fedha, mfano katika nchi za Asia zimekuwa na matokeo mazuri sana, kwa hiyo na kwetu ina umuhimu mkubwa sana.”

Amefafanua kuwa,mikopo ambayo inatolewa na taasisi za kifedha vikiwemo vikundi vyenye leseni halali imekuwa ikisaidia jamii kutatua changamoto mbalimbali na kujipatia mitaji ya kuendeshea biashara zao.

Katika hatua nyingine, Dkt.Yamungu amefafanua kuwa, semina hizo wamekuwa wakizifanya kwa zaidi ya miaka 10 sasa na zimeonesha matokeo mazuri.

“Tumekuwa tukifanya hivi, sisi kama BoT na kama taasisi ya umma tungependa kuendeleza utaratibu huu.

“Dhumuni la semina hii ni kuwapa uelewa wa kutosha kuhusu utekezaji wa mfumo mpya wa wa Sera ya Fedha.”

Katika hatua nyingine, Dkt.Yamungu amebainisha kuwa,elimu ya fedha ni endelevu kwani inasaidia kuwapa uelewa mpana wana jamii ili waweze kutumia fursa zilizopo ikiwemo mikopo inayotolewa na taasisi rasmi kujiletea maendeleo.
“Mtakumbuka, kuna wakati ambapo watu walikuwa wanatapeliwa unaambiwa ukiweka laki tano, utapata kama milioni tatu kwa mwezi.

“Jamaa wale wanafanya ujanjaujanja fulani hivi,wanaangalia wanakupa kama milioni moja na nusu hivi, jambo ambalo halipo.Kwa hiyo, elimu hii ya fedha, nadhani ni maeneo yote lazima tuendelee kujifunza.

“Kwa hiyo tukasema, itakuwa vizuri zaidi kwa sababu sasa mnafahamu kazi kubwa na ya msingi ya benki zote kuu duniani ni kuandaa na kusimamia Sera ya Fedha,”amefafanua.

Vile vile, amesema Sera ya Bajeti kwa maana ya mapato na matumizi na Sera ya Fedha ni shilingi moja yenye pande mbili.

“Hivyo, ni vizuri tupite pia kwenye Sera ya Bajeti, kwa sababu tutakuwa tunajenga uelewa zaidi jinsi hizi sera mbili ambazo ni kama mapacha zinavyofanya kazi.

“Kwa hiyo kuna uhusiano mkubwa sana, kwa hili la kwanza tutawapitisha kwenye mfumo mpya wa Sera ya Fedha, lakini lazima tuweke background ya Sera ya Bajeti.”

Aidha, amewashukuru wanahabari kwa kuendelea kuonesha ushirikiano mkubwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Kwa lugha rahisi, na wengi mtakuwa mmefuatilia historia za Benki Kuu duniani, ni chombo pekee, taasisi pekee iliyopewa mamlaka ya kuchapisha sarafu ya nchi husika.

“Na yenyewe baada ya kupewa hilo jukumu, lazima iangalie thamani ya hiyo fedha inayoitoa na mfumuko wa bei, kwa sababu kuna watu au kuna sehemu moja inaamini kwamba hii taasisi inayochapisha hizi fedha ndiyo inayosababisha haya yote.”

Kaimu Mkurugenzi wa Tawi la BoT Zanzibar, Bw.Massoud Suleiman amesema, BoT imekuwa na utaratibu wa kukutanisha pamoja wanahabari ili kujifunza masuala mbalimbali yahusuyo benki hiyo.

Pia, ametoa wito kwa wanahabari ambao wanashiriki mafunzo hayo baada ya kumaliza mafunzo kwenda kuwa mabalozi wazuri wa BoT katika jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news