DAR ES SALAAM-Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba ameonesha kuuzunishwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kushindwa kushughulika changamoto za Bandari Kavu jijini Dar es Salaam.
Hali ambayo amesema husababisha msongamano wa malori yanayoingia jijini kwa ajili ya kupakua na kupakia mizigo.
Mwinjilisti Temba amesema kuwa, amechukua hatua ya kufuatia baadhi ya madereva kulalamikia msongamano mkubwa ulioko katika Bandari Kavu ya Ubungo, hali inayosababisha wao kupoteza muda mwingi jijini wakisubiri kushusha ama kupakia mizigo.
"Na bila kupepesa macho wanalalamika kwamba wanaendelea kuteseka kwa sababu wamekaa muda mrefu sana Zambia na Kongo miezi kadhaa walikuja wakatumia zaidi ya wiki mbili Misugusugu mpaka waje washushe mzigo katika Bandari Kavu ya Ubungo.
"Mara hii nainyoshea mkono TPA na TANROADS kwa sababu nimekuwa nikilalamikia jambo hili la Bandari Kavu kwa zaidi ya mara 15 ndani ya miaka mitano mitano.
"Lakini hakuna juhudi za haraka zaidi ambazo zimekuwa zikifanyika, hivyo sasa namuomba Mungu kwa sasa waone kwa vitendo athari hizi,"amesema Mwinjilisti Temba.
Mwinjilisti Temba ambaye ametembea nchi zaidi ya 10 ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia ameeleza kwamba, haitakiwi malori kama hayo kukaa hata sekunde moja katikati ya miji.
Vile vile amesema, nchi nyingi duniani zimeondoa utaratibu wa malori kuingia katikati ya miji, ambapo amebainisha kuwa hata kama yakiingia huwa ni kwa muda maalum hususani nyakati za usiku.
"Na hata malori haya yakiruhusiwa kuingia yanaruhusiwa kushusha au kupakia mzigo katika viwanda na magodauni yaliyopo katika miji hiyo kwa vibali maalum na mara nyingi huwa yanaingia usiku ili yasichangamane na wananchi.
"Na mara nyingine malori hayo yanatakiwa yakija yawe masafi, lakini malori hayo yanakuja kutoka nchini Kongo ambako kuna maradhi mbalimbali ya kansa ya ngozi, yako maradhi ya macho aina ya ukoma, yako maradhi kama ya Ebola na maradhi mengine ambayo yanaweza yakawa yamebebwa na vumbi la malori hayo lilisombwa kutoka Kongo na kuja kukung'utia watu hapo Ubungo.
"Ukizingatia kabisa Ubungo ni kama kona ya jamii kubwa asilimia zaidi ya 35 ya Jiji la Dar es Salaam inaweza kupata maambukizi ya magonjwa endapo kutakuwa na mlipuko huo," amesema Mwinjilisti Temba.
Mwinjilisti Temba amesema, kwa bahati mbaya nchini hakuna sehemu maalum zilizotengwa pembeni mwa barabara za lami na kuwekwa maji yaliyochanganywa na dawa ili magari yapite sehemu hiyo kwa ajili ya kuua bakteria akitolea mfano nchi za Zambia na Botswana ambao wameweka utaratibu huo.
"Kwa bahati mbaya hakuna Vetenari ambao wanakaa katikati ya barabara, kwa mfano nchi za Zambia na Botswana, kwa Botswana huwezi ukatoka mpakani mpaka kuingia Gaboron bila kukutana na watu wa mifugo ambao wanamwaga dawa barabarani.
"Katika barabara ya lami wametengeneza gari lipite pembani mwa barabara ambako kunakuwa kuna dawa zimechanganywa na maji, hivyo gari hilo ama basi au gari ndogo ikifika hapo inabidi ikanyage hayo maji ambayo yamechanganywa na dawa kwa ajili ya kuua bakteria, ukienda Zimbabwe wanafanya hivyo pia," amesema Mwinjilisti Temba.
Mtumishi huyo wa Mungu Mwinjilisti Temba amesisitiza kwamba utaratibu huo kwa Tanzania haupo jambo ambalo ni hatari sana kutokana na vumbi linaloletwa na magari hayo yanayotoka Kongo na Zambia na kuja kukung'utwa Ubungo.
Amesema, madhara yake yanaweza kuathiri kizazi kijacho na kikapata shida kubwa ya kiafya, kimazingira na kupatikana magonjwa ambayo yanaweza kusababisha Serikali kutumia gharama kubwa ili kuweza kuponya kwa kuwapatia tiba Watanzania ambao watakuwa wameathirika.
"Hivyo nawaambia TPA inabidi ni muachie Mungu awaonyeshe kwa njia nyingine, kwa sababu inaonekana kwamba nina maslahi binafsi kumbe naipenda nchi yangu.
"Uzalendo ndio unaonisukuma kupiga kelele zaidi ya mara 15 ndani ya miaka 10 nimekuwa nikizungumzia kuhusiana na mambo mbalimbali juu ya upangaji mji, juu ya malori haya, juu ya mambo mbalimbali ya kijamii na Taifa yanavyopaswa kuwa.
"Lakini kumekuwa na ukimya, wamekuwa wakiniangalia na wakati mwingine wakisema kwamba mimi nimekuwa nikitafuta umaarufu, lakini matokeo yake sasa hivi tunaona Watanzania wenyewe.
"Madereva wanapiga kelele na bahati mbaya waandishi wa habari mbalimbali hawaendi Misugusugu, hawaendi Ubungo kwenda kuona mambo haya, kuangalia namna gani Serikali ichukue tahadhari zaidi kwa sababu ya magonjwa ya mlipuko," amesema Mwinjilisti Temba.
Mwinjilisti Temba akiendelea kuzungumza kuhusu magonjwa ya mlipuko amesema, nchini Kongo kuna mambo mengi na shida ambazo zimekuwa zikisababishwa na magonjwa mbalimbali ambayo yanabebwa na vumbi la magari hayo na kuja kukung'utwa Ubungo.
"Kwamba Ubungo ndiyo senta ya njia ya kwenda maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kama vile Buguruni, Temeke, Posta, Tegeta, Kimara, Kariakoo na kadhalika.
"Hivyo kama kuna magonjwa ya mlipuko ambayo yatawaambukiza watu katika eneo lile (Ubungo) yataathiri watu wengi sana.
"Lazima tusema uhatari huu ili Serikali iweze kuona na TANROADS kuona namna gani ni vizuri kuwa na kinga kuliko tiba.
"Ikiwezekana ni vizuri wataalam wa afya wakapita wakachukua sampuli maeneo yale ya kuangalia kama kuna viashiria vyovyote vya janga lolote la maambukizi ya kiafya yanayoletwa na malori haya.
"Hata pale Misugusugu ni vizuri wataalam wakaenda wakachukua sampuli wakaangalia je tuko salama? Ni vizuri kukapigwa dawa maeneo yale, jamani Kongo ni hatari, tumuombe Mungu atuepushe na janga lolote lisije likatokea," amesisitiza Mwinjilisti Temba.
Mwinjilisti Temba ni mtumishi wa Mungu ambaye Watanzania wengi wanaomfuatilia wanasema ni zawadi kwa nchi kutokana na ufahamu na ujasiri mkubwa alionao.
Hata hivyo, wengine wanaenda mbali zaidi na kumfananisha na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), Hayati Mchungaji Christopher Mtikila.