NEC yatangaza uchaguzi mdogo kata 23

DODOMA-Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza uchguzi mdogo wa madiwani kwenye kata 23 za Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele (katikati) akiongoza kikao cha Tume jijini Dodoma tarehe 15 Februari,2024 ambapo pamoja na mambo mengine kilitangaza uchaguzi mdogo wa kata 23 za Tanzania Bara utakaofanyika Machi 20,2024. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji (Rufaa) Mstaafu, Mbarok Salim Mbaruk na kulia ni Katibu wa Tume na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima R.K. (Picha na NEC).

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani jijini Dodoma leo Februari 15, 2024 uchaguzi huo utafanyika Machi 20, 2024.

“Fomu za uteuzi zitatolewa kuanzia t Februari 27, 2024 hadi tarehe 04 Machi, 2024, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 04 Machi, 2024 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 05 hadi 19 Machi, 2024,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeanisha kuwa uchaguzi huo umetangazwa kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, akiitaarifu Tume kuhusu uwepo wa nafasi wazi za madiwani katika kata 23 za Tanzania Bara.

Imeongeza kuwa Waziri ametoa taarifa hiyo kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292.

“Tume inatumia nafasi hii kuvikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi cha uchaguzi huu mdogo,” imesema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kata zitakazofanya uchaguzi huo mdogo ni Kimbiji (Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni), Kasingirima (Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji), Ndevelwa (Halmashauri ya Manispaa ya Tabora), Msangani (Halmashauri ya Mji Kibaha), 

Nyingine ni Fukayosi (Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Mlanzi (Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti), Utiri (Halmashauri ya Mji Mbinga) na Mbingamhalule (Halmashauri ya Wilaya ya Songea).

Aidha, kuna Isebya (Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe), Kibata (Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa), Mshikamano (Halmashauri ya Wilaya ya Musoma), Busegwe (Halmashauri ya Wilaya ya Butiama), 

Nyingine ni Nkokwa (Halmashauri ya Wilaya ya Kyela), Kamwene (Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba), Chipuputa (Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu), Buzilasoga (Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema), Mhande (Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba), Kabwe (Halmashauri ya Nkasi), Bukundi (Halmashauri ya Wilaya ya Meatu) Mkuzi (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza) na Boma, Mtimbwani na Mayomboni (Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news