NFRA Sumbawanga yanunua tani 57,000 za mahindi, yaja na mfumo mpya



RUKWA-Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) Kanda ya Sumbawanga imenunua kutoka kwa wakulima mkoani Rukwa na Katavi jumla ya tani 57,000 za mahindi zenye thamani ya shilingi bilioni 52.4 kwa msimu wa mavuno wa mwaka 2023/24 huku tani 46,000 kati ya hizo zikiwa na thamani ya shilingi bilioni 41.4 zikinunuliwa kwa Mkoa wa Rukwa pekee.
Meneja wa Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula Kanda ya Sumbawanga, Bw. Marwa Range amesema kuwa katika msimu wa mavuno wa Mwaka 2024/2025 Wakala imeanzisha utaratibu wa kutoa mikataba (forward contracts) kwa vyama vya ushirika na wakulima binafsi kuuza mazao kwa Wakala kwa bei ya soko mara wanapovuna.

Amesema, manufaa ya mfumo huo wa mikataba ni pamoja na kutoa uhakika wa soko kwa mkulima na kumwezesha kupata mkopo kutoka benki ili kuendeleza shughuli za kilimo.

Aidha,Bw. Range ameeleza kuwa mfumo huo utaongeza tija na ushawishi kwa watu wengi zaidi kujiingiza kwenye shughuli za kilimo na kuongeza uhakika wa chakula kwa Taifa na kuifanya Wakala kuwa tegemeo kwa bara la Afrika siku za usoni.

Mfumo huo umekuja ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa agenda ya kilimo biashara ili kufikia asilimia kumi (10%) ya mchango wa sekta ya kilimo ifikapo 2030.

Range ameeleza kuwa mpaka kufikia Februari 2024, vyama vya ushirika 45 na wakulima binafsi 5 wamenufaika na utaratibu wa mikataba ya kuuza mazao kwa Wakala Kanda ya Sumbawanga. 

Amesema kuwa, ili mkulima binafsi apate mkataba huo atatakiwa kuwa na mazao yasiyopungua kiasi cha tani 200.

Kwa mujibu wa Bw. Range, ununuzi wa mahindi kwa Kanda ya Sumbawanga kwa msimu wa 2023/24 umeiwezesha NFRA kuchangia pato la Mkoa kwa takribani kiasi cha shilingi bilioni 1.5 ambapo Halmashauri za Mkoa wa Rukwa zinatarajia kulipwa fedha hizo kupitia ushuru wa mazao.

Meneja huyo wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula amewahimiza wakulima kuchangamkia fursa ya mikataba ya kuuza kwa bei ya soko ili kuinua pato huku akieleza kuwa Wakala inatarajia kuongeza wigo wa ununuzi wa mazao kwa kuongeza zao la mpunga na mtama kwa msimu wa mwaka 2024/2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news