Taarifa mapitio ya maboresho ya kitita cha mafao ya mwaka 2023 cha NHIF yatua kwa Waziri Ummy

DAR ES SALAAM-Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu amekutana na Umoja wa Wamiliki wa Vituo Binafsi vya Afya (APHFTA), viongozi wa vituo vinavyomilikiwa na Mashirika ya Dini (CSSC na BAKWATA) kwa lengo la kupokea taarifa ya kamati aliyoiunda ya kufanya mapitio ya maboresho ya kitita cha mafao ya mwaka 2023 cha NHIF ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware.
Waziri Ummy amepokea taarifa hiyo leo Februari 19, 2024 katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam ambapo ameishukuru na kuipongeza kamati hiyo ya Wataalam kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya.

Miongoni mwa mapendekezo ya kamati ni pamoja na wizara kuandaa mwongozo wa ukokotoaji wa bei za huduma za Afya kwa vituo vya umma na vituo binafsi ambao utabainisha bei halisi katika utoaji wa huduma.

Pia, Wizara kuandaa mwongozo wa vifaa, vifaa tiba na vitendanishi vinavyohitajika katika utoaji wa huduma mbalimbali za matibabu, Wizara kufanya utafiti na kuishauri Serikali ili kuwezesha watoa huduma binafsi kupata msamaha kwa baadhi ya kodi au ruzuku na kupata fursa za mitaji nafuu kutoka taasisi mbalimball za kifedha.

Aidha, Waziri Ummy ametoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya kwa kuwa ni himilivu na endelevu katika kuelekea Utekelezaji wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote iliyosainiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news