Tanzania, Poland mbioni kuwa na safari za moja kwa moja

DAR ES SALAAM-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema kuwa,timu ya wataalam imeshaelekezwa kuchukua hatua zitakazowezesha kuanza safari za moja kwa moja kati ya Poland na Tanzania.

"Asubuhi ya leo nimemkaribisha nchini na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Poland, Mheshimiwa Andrzej Duda. 

"Uhusiano kati ya Tanzania na Poland ni wa kihistoria na umedumu kwa zaidi ya miaka 60. Hii ni mara ya kwanza kwa Rais wa Poland kufanya ziara ya kitaifa Tanzania, na nimemshukuru kwa kuchagua Tanzania kama nchi mojawapo kufika katika ziara yake barani Afrika.

"Poland ni nchi ya 21 kwa ukubwa wa kiuchumi duniani na mshirika wetu muhimu katika Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. 

"Tunashirikiana katika maeneo mbalimbali ya kwa manufaa ya wananchi wetu hasa kwenye utalii ambapo Poland ni kati ya nchi 10 zinazoleta watalii wengi zaidi nchini. 

"Kutokana na ukuaji huu wa biashara ya utalii baina yetu, nimemueleza nia yetu ya kuwa na safari za moja kwa moja za ndege kutoka Poland kuja Tanzania. 

"Mbali na utalii, pia tuna ushirikiano mkubwa katika sekta ya afya, wakishiriki nasi miradi kwenye hospitali za Aga Khan, Temeke, Mwananyamala, Kituo cha Afya Chanika na Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana. 

"Tumekubaliana kuendelea kushirikiana zaidi katika maeneo ya elimu, kilimo, biashara, uwekezaji, utalii na TEHAMA eneo ambalo wenzetu wamepiga hatua kubwa. 

"Kiuchumi, tumeweka nia ya pamoja na kuazimia kuhamasisha uwekezaji zaidi kwenye sekta za kimkakati kama viwanda, uzalishaji, nishati, madini, gesi asilia na uchumi wa bluu. 

"Nimeshukuru pia kwa utayari wa nchi yake kupitia wakala wa mikopo ya usafirishaji kutoa bima kwa benki za biashara katika utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa nchini kwa vipande vya Makutopora - Tabora na Tabora - Isaka. 

"Kwa ujumla, sote tumeona kwamba kwa umri na historia ya ushirikiano uliopo kati yetu, maswala ya biashara na kuinua uchumi bado ni madogo hivyo basi lazima kuongeza ushirikiano wetu kiuchumi kwa njia za uwazi, haki na kuaminiana. 

"Mheshimiwa Rais amenipa pia mwaliko wa kutembelea Jamhuri ya Poland, na mimi nimemuahidi kuwa panapo majaliwa, mimi na ujumbe wangu kwa niaba ya nchi yetu tutafanya ziara ya kitaifa nchini humo."
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Mgeni wake Rais wa Poland Andrzej Duda, Ikulu jijini Dar es Salaam leo Februari 9, 2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news