Tanzania yatoa uzoefu wake katika kuendeleza madini mkakati

CAPE TOWN-Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amepata fursa ya kuelezea uzoefu wa Serikali ya Tanzania katika Uendelezaji Madini Muhimu na Mkakati na kutoa wito kwa nchi za Afrika kuona umuhimu wa kuwa na Sera ya Pamoja kusimamia madini ili Bara la Afrika linufaike ipasavyo.
Dkt. Kiruswa amepata fursa hiyo katika Kongamano la Mawaziri wanaosimamia Sekta za Madini kwa nchi za Afrika zinazotarajia kushiriki Mkutano wa Uwekezaji wa Mining Indaba unaoanza Februari 5 hadi 8, 2024, Capetown nchini Afrika Kusini ambao mwaka huu unatimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake.

Akizungumza katika kongamano hilo, Dkt. Kiruswa ameeleza hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Tanzania imeendelea kuzichukua katika uendelezaji wa madini muhimu na mkakati na kuielezea miradi ya uchimbaji na uchakataji wa madini ya nikeli unaotekelezwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Tembo Nikel na miradi ya uchimbaji madini ya graphite ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Halikadhalika, Dkt. Kiruswa ameeleza kuhusu uwepo wa masoko ya madini yapatao 42 na vituo vidogo vya ununuzi madini vipatavyo 96 yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali nchini na namna ambavyo masoko hayo yameongeza uwazi, tija na kurahisisha biashara ya madini kwa Tanzania.

Ameongeza kuhusu uwepo wa mfumo wa uombaji leseni za madini ambao umeongeza uwazi kwa waombaji wa leseni za madini na kueleza namna ambavyo Serikali inaamini katika kushirikiana na sekta binafsi kuendeleza sekta za madini.
"Tunajua kuwa tunahitaji kushirikiana na wawekezaji ili tuwe pamoja na kuwa na sauti moja,’’amesema Dkt.Kiruswa.

Pia, ameeleza kuhusu umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika uchumi wa Madini na kuieleza hadhira hiyo juu ya jitihada ambazo zimefanywa na Serikali ya Tanzania kurasimisha shughuli za uchimbaji mdogo wa madini ambapo mchango wao katika maduhuli ya Serikali umeongezeka na kufikia asilimia 40.

Mbali na kutoa uzoefu huo, Dkt. Kiruswa amezinadi fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta yaMadini Tanzania na kuzitaja kuwa ni pamoja na utafiti wa madini hususan madini mkakati, uongezaji thamani madini pamoja na kueleza mazingira rafiki ya biashara yaliyopo katika Sekta ya Madini ikiwemo Sheria, Sera na Kanuni zinazosimamia sekta ya madini nchini ambapo pia amevitaja vipaumbele vya Serikali katika kuendeleza Sekta ya Madini.
Wakizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo kwa nyakati tofauti, Waziri wa Nishati na Madini wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Gwane Mantasha amesisitiza kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano kati ya Serikali za Afrika na kusisitiza umuhimu wa madini kuongezwa thamani ndani ya bara la Afrika.

Naye, Rais wa Taasisi ya Jiolojia ya Afrika Kusini, Norera Fakude amezitaka nchi za Afrika kuiona na kuifanya kesho ya Afrika kuwa sasa na kuhakikisha rasilimali madini zinazinufaisha bara hilo sasa na wakati mwingine.
Katika kongamano hilo, mada mbalimbali zimejadiliwa ikiwemo masuala yanayohusu teknolojia, kushirikishana ujuzi na uzoefu na umuhimu wa kutumia viwanda vya uongezaji thamani madini vya ndani ya bara hilo.
Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano huo kwa mwaka huu umekuwa wa pamoja tofauti na miaka mingine ambapo Wizara ya Madini imeshirikiana na Chemba ya Migodi kuwezesha ushiriki huo. Tanzania katika mkutano huo inatarajia kushiriki katika shughuli mbalimbali kuendelea kuzinadi fursa zake za kiuwekezaji katika Sekta ya Madini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news