Uendelezaji miji uzingatie Mpango Kabambe-Naibu Waziri Pinda

NA MUNIR SHEMWETA
WANMM

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda amezielekeza Halmashauri zote nchini kuhakikisha maendelezo yoyote yanayofanyika yanazingatia na kufuata mipango kabambe ya maeneo husika
Mhe. Pinda ametoa kauli hiyo Februari 6, 2024 Bungeni Dodoma wakati aikijibu swali la nyongeza la Mbunge wa jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza Mhe. Stanslaus Mabula aliyetaka kujua ni nini mikakati ya serikali kuhakikisha maendelezo yanayofanyika kwenye halmashauri hayavunji au utekelezaji wake hauendi kinyume na mpango kabambe kwa kufanyiwa matumizi mengine yasiyokusudiwa.

Kwa mujibu wa Mhe. Pinda baadhi ya meneo hasa majiji makubwa tayari yana mipango mahususi (mpango kabambe) ya kuendelezwa ikiwemo jiji la mwanza lakini kumekuwa na utofauti katika kusimamia kile ambacho halmashauri imejipangia kwenye utekelezaji wa mipango kabambe ya miji yao.

‘’Nitoe rai kwa mamlaka za miji na majiji kuzingatia yaliyopitishwa na mamlaka zao kwa kuhakikisha miji inatoka na sura nzuri sana kwa kuzingatia mipango kabambe na hili la Mwanza wazingatie kile walichokubaliana,’’alisema Mhe. Pinda.

Akielezea zaidi kuhusiana na suala la jiji la Mwanza, Mhe. Pinda alitoa msisitizo kwa jiji hilo kuzingatia kile walichokubalina kwenye mpango kabambe kwa kuwa kiasi kikubwa cha fedha kimetumika wakati wa kuandaa mpango huo wa uendelezaji katika jiji hilo.

Awali,Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Asia Sharif Omar alisema, kumekuwa na ujenzi holela katika maeneo mbalimbali licha ya uwepo sheria zinazoweka masharti ya ujenzi katika miji nchini.

Amebainisha kuwa, chanzo kikubwa cha ujenzi holela ni ukuaji wa kasi miji midogo kutoka vijiji unaotokana na shughuli za kibinadamu ambapo amesema kuwa, kutokana na hali hiyo wizara yake imekuja na mikakati ya kupima nchi nzima hadi vijijini.

Kwa mujibu wa Mhe. Pinda kampeni ya kupima vijiji inayofanywa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi sambamba na upimaji miji unaofanywa na halmashauri kwa ushirikiano na wizara ni sehemu ya juhudi za kupambana na ujenzi holela.

Aidha, alisema ipo miradi ya urasimishaji wa makazi na upimaji shirikishaji aliyoieleza kuwa ni mikakati ya kupamabana na ujenzi holela na kuweka wazi kuwa Serikali itaendelea kukabiliana na changamoto za ujenzi holela usiozingatia taratibu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news