Usikope kwa sababu wengine wanakopa-BoT

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema si jambo la busara kwenda kukopa mkopo kwa watoa huduma za fedha kwa kuwaona wengine wanakopa.

"Mkopaji anashauriwa kukopa kwa ajili ya uwekezaji unaozalisha kama vile kununua sehemu ya ardhi ambapo ataweza kuzalisha mazao au kuongeza biashara.

"Hii itamuwezesha mkopaji kurejesha mkopo na kuweza kukopa zaidi baadaye kama itahitajika. Tumia mkopo kwa busara na kamwe usikimbilie kukopa. Fikiria mara mbili kabla ya kukopa kwa ajili ya starehe au kununua vitu vya matamanio;
Hayo yamesemwa leo Februari 15, 2024 na Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Sekta ya Fedha-Idara ya Usimamizi wa Huduma Ndogo ya Sekta ya Fedha BoT, Deogratius Mnyamani.

Ni katika siku ya pili ya semina kwa waandishi wa habari za uchumi iliyoandaliwa na BoT ambapo amewasilisha mada ya maendeleo ya utekelezaji wa Sheria Ndogo ya Huduma za Fedha (The Microfinance Act.2018).

"Usikope kwa sababu wengine wanakopa, si busara kuchukua mkopo kwa kuwa watu wengine walio karibu nawe wamefanya hivyo. Jiulize kama kweli unahitaji mkopo. Mara nyingi, ni bora kuweka akiba kuliko kuchukua mkopo.

"Chukua mkopo kama ambao wanakwenda kukopa mikopo kufahamu gharama za mkopo na kuziafiki kabla ya kuchukua mkopo,"

Bw.Mnyamani amesema,gharama hizo ni pamoja na riba na ada nyingine zilizoainishwa katika mkataba wa mkopo.

"Kabla ya kuchukua mkopo, muulize mkopeshaji kuhusu jumla ya kiasi ambacho unapaswa kulipa katika kipindi chote cha mkopo. Ni wajibu wa mkopeshaji kumfahamisha mkopaji jumla ya gharama zote zinazohusiana na mkopo husika."

Amefafanua kuwa, riba n kiwango cha gharama ya mkopo ambacho hulipwa kwa mtu au taasisi ya fedha inayokopesha.

Vile vile, riba hukokotolewa kutoka kwenye kiwango cha mkopo uliotolewa, ambapo kwa kawaida huwa ni asilimia ya kiasi cha mkopo kwa kipindi husika.

"Mfano kama utachukua mkopo wa shilingi 100,000 kwa riba ya asilimia 12 kwa mwaka, utalipa riba ya shilingi 12,000 pamoja na shilingi 100,000 ambayo utapokea kama mkopo.

"Katika kipindi cha mwaka mmoja, mkopaji atawajibika kumlipa mkopeshaji shilingi 112,000 (100,000 +12,000),"amefafanua Bw.Mnyamani.

Ameongeza mfano m,wingine kuwa, kama utachukua mkopo wa shilingi 100,000 kwa riba ya asilimia 12 kwa mwezi, utalipa riba ya shilingi 12,000 kila mwezi.

"Kwa mwaka, mkopo huu utakuwa na riba ya kiasi cha shilingi 144,000. Kwa hiyo utahitajika kumlipa mkopeshaji jumla ya shilingi (100,000 + 144,000) sawa na shilingi 244,000."

Mnyamani amesema, riba inaweza kuwa isiyobadilika au inayobadilika. Riba inayobadilika hutolewa kulingana na kiasi cha mkopo ambacho hakijarejeshwa.

Riba isiyobadilika amesema. kiwango chake huwa hakibadiliki wakati wote wa kurejesha mkopo.

"Kutambua aina za riba kunakuwezesha kupanga kwa usahihi namna ya kurejesha mkopo.Unajua ni adhabu gani utapata ikiwa hutolipa mkopo wako kwa muda?

"Wakati unataka kuchukua mkopo, linganisha gharama za mikopo inayotolewa kutoka taasisi mbalimbali za fedha kwa kuzingatia viwango vya riba, muda wa kurejesha mkopo, tozo na adhabu za kushindwa kurejesha mkopo kwa wakati.

"Kukopa kwa mkopeshaji mwenye gharama nafuu za mkopo kutamuwezesha mkopaji kulipa mkopo kwa wakati, hivyo ni muhimu mkopaji kufanya utafiti wa gharama na masharti ya mkopo kabla ya kukopa.

"Ni wajibu wa mkopeshaji kutoa taarifa zote zinazohitajika kwa mkopaji ili aweze kufanya maamuzi sahihi,"amefafanua Bw.Mnyamani.

Amesema, ni muhimu kabla ya kuchukua mkopo, kupanga jinsi gani utarejesha mkopo pamoja na riba. Pia, mkopaji ana wajibu wa kurejesha kiasi alichokopa, riba na gharama nyingine za ziada.

Kama mkopaji anafahamu kuwa hataweza kurejesha mkopo katika kipindi cha makubaliano, hapaswi kuchukua mkopo. Inashauriwa kupanga kwa makini matumizi ya mkopo kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa.

"Usichimbe shimo kujaza shimo lingine, kama tayari una madeni ya mikopo, epuka kuchukua mkopo mwingine kwa vile mkopo huo utaongeza madeni yako na hivyo kukuongezea mzigo zaidi. Kumbuka utatakiwa kulipa gharama za ziada, ada na riba ya mkopo huo mpya.

"Usikate tamaa au kupoteza matumaini kama unapata changamoto kulipa mkopo wako. Shauriana na familia au marafiki kuhusu namna bora ya kulipa deni la mkopo.

"Kama utashindwa kulipa kwa wakati kama ilivyowekwa kwenye mkataba, mtaarifu mkopeshaji wako mapema.

"Usijaribu kupoteza muda kwa kulipa na hundi ambayo itakataliwa benki (kutoa hundi wakati huna pesa za kutosha kwenye akaunti yako). Usitoe taarifa yoyote ya uongo au ya kupotosha,"amesisitiza Mnyamani.

Mbali na hayo amesema, ikiwa unachukua mkopo kutoka kwenye taasisi ya fedha inayosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania, historia yako ya ulipaji itarekodiwa.

"Wakati mwingine utakapoomba mkopo, taarifa hii itatumika kusaidia wakopeshaji kuamua kukupa au kutokupa mkopo na masharti yake.

"Historia yako ikiwa bora, na masharti ya mkopo wako yatakuwa nafuu. Ikiwa kuna makosa kwenye taarifa yako ya mkopo, tafadhali wasiliana na taasisi yako ya fedha ya kukopesha na kuelezea malalamiko yako ambayo yatawasilishwa kwenye taasisi za ubadilishanaji wa taarifa za mikopo (Credit Reference Bureau) kwa ajili ya kupata suluhu."

Amesema, ni muhimu kwa mkopaji kukopa kwenye taasisi za fedha zilizosajiliwa na kutambulika na Benki Kuu ya Tanzania au mamlaka kasimishwa.

Hii itasaidia kutatua changamoto zitakazojitokeza kwa kuwa taasisi hizi zinaendeshwa kwa mujibu wa Sheria na kanuni zilizowekwa na Serikali.

Mamlaka kasimishwa, Mnyamani amesema ni Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) inayosimamia Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOs) na Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs) inayosajili na kusimamia vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kama vile vikundi vya hisa na akiba (Village Loans Association (VLSA) na Village Community Banks (VICOBA)).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news