Waziri Mkuu aweka jiwe la msingi soko la kisasa Tarime Mjini

*Ujenzi wake kugharimu sh. bilioni 9.6, kukamilika Mei, 2024

MARA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa soko la kimkakati la Tarime mjini unaotarajiwa kugharimu sh. bilioni 9.6 hadi kukamilika kwake.
Muonekano wa soko la kisasa katika halmashauri ya mji Tarime ambalo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko hilo, wakati wa ziara yake Mkoani Mara, Februari 28, 2024. Soko hilo limegharimu shilingi bilioni 9.68. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Akipokea taarifa ya ujenzi wa soko hilo jioni ya Jumatano, Februari 28, 2024 Waziri Mkuu alielezwa kwamba mradi huo kwa sasa upo katika hatua ya umaliziaji na umefikia asilimia 82 ya utekelezaji.

Akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Tarime, Bi. Gimbana Ntavyo alisema shughuli zinazoendelea kwa sasa ni skimming, upakaji wa rangi, ufungaji wa milango kwenye maduka na vyoo na ufungaji wa mifumo ya umeme na maji kwenye jengo kuu la soko.
Alisema kazi nyingine ni uwekaji wa vigae na terazo kwenye vizimba, maduka ya nje na ndani na kwa upande wa kazi za nje, wanaendelea na uzalishaji wa paving na kuandaa maeneo ya kuzipanga.

“Hadi sasa malipo yaliyofanyika kwa mkandarasi ni sh. bilioni 5.77 na kwa mshauri ni sh. milioni 120.36 sawa na asilimia 60.86 ya gharama za mradi,” alisema na kuongeza: “Mradi huu utakuwa na maduka 325, vizimba 160, mabucha matatu, migahawa miwili, supermarket moja na Benki mbili.”
Akielezea manufaa ya mradi huo, Mkurugenzi huyo alisema mradi huo umetoa ajira za muda kwa watu 441 na utakapokamilika, Halmashauri inatarajia kuongeza mapato yake ya ndani kwa sh. milioni 588 kwa mwaka kutokana na mapato yatakayokusanywa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news