Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dkt.Abiy Ahmed Ali kuwasili nchini kwa ziara ya siku tatu

DODOMA-Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, Mheshimiwa Dkt. Abiy Ahmed Ali anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 29 Februari hadi 02 Machi, 2024 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dkt. Abiy Ahmed Ali. (Picha na Minasse Wondimu Hailu/Anadolu Agency via Getty Images).

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 27,2024 na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dodoma.

Mhe. Dkt.Abiy atapokelewa rasmi Ikulu, Dar es Salaam tarehe 01 Machi, 2024 na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Lengo la ziara hii mbali na kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili, inalenga pia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Ethiopia.

Pande zote mbilizimekuwa zikishirikiana katika maeneo ya biashara na uwekezaji, elimu, utamaduni, usafirishaji wa anga, kilimo, mifugo, udhibiti wa uhamiaji holela, ulinzi na usalama.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ethiopia zina uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu na wa kihistoria ambao ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mtawala wa Ethiopia,Hayati Haile Selassie.

Viongozi hawa walishirikiana bega kwa bega katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika ni miongoni mwa Viongozi Waanzilishi 32 wa Umoja wa Afrika wakati huo OAU mwaka 1963.

Aidha, mbali na ushirikiano wa kidiplomasia, Tanzania na Ethiopia zinashirikiana katika sekta ya anga ambapo mwaka 2016 hadi 2023 jumla ya marubani 75 na wahandisi 25 kutoka Tanzania wamepokea mafunzo katika ngazi tofauti nchini Ethiopia.

Hivyo ni wazi kuwa, ziara hii itafungua milango zaidi ya ushirikiano kaW ya Shirika la Ndege la Ethiopia na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika kujiendesha kibiashara.

Hali kadhalika, Tanzania na Ethiopia zinashirikiana kaWka sekta ya mifugo na kilimo.

Nchi hizi zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo na uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo kama kahawa, chai, asali, mbogamboga na matunda barani Afrika.

Kupitia ziara hii Tanzania na Ethiopia zitaimarisha ushirikiano katika masuala ya umwagiliaji, matumizi ya teknolojia katika kilimo na matumizi ya mbegu zenye ubora na uhakika wa mavuno sambamba na tafiti katika sekta hizo mbili.

Kuhusu sekta ya nishati, ziara hii itaziwezesha Tanzania na Ethiopia kujengeana uwezo na kubalishana uzoefu katika uzalishaji wa umeme unaotosheleza mahitaji ya nchi pamoja na kuzalisha umeme wa kibiashara utakaoiwezesha Tanzania kuuza katika nchi mbalimbali kupitia uanachama wake katika Jumuiya ya kuuziana umeme ya Afrika Mashariki (East African Power Pool).

Aidha, katika sekta ya elimu ziara hii itaziwezesha nchi hizi mbili kubadilishana wanafunzi na kujenga uwezo katika uuandaji wa mitaala na Tanzania kupata fursa ya kufundisha Kiswahili nchini Ethiopia.

Mhe. Waziri Mkuu Abiy na ujumbe wake wataondoka nchini kurejea Ethiopia tarehe 02 Machi 2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news