Waziri Mkuu:Shilingi bilioni 1.3 zitakamilisha ujenzi Soko la Kimataifa la Mazao Renagwe

MARA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeridhia kutoa sh. bilioni 1.3 kwa ajili ya ukamilishaji wa soko la kimataifa la mazao ya kilimo lililopo Renagwe, wilayani Tarime, mkoani Mara.

“Masoko haya tumeyajenga kila palipo na mpaka. Tumejenga Namanga, Tunduma, Kasumulo, Horohoro, Holili pamoja na hili la Tarime ambalo ni la muda mrefu, zabuni ya kulikamilisha hili na la Horohoro tayari zimeshatangazwa,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Februari 28, 2024 wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Sirari kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Tarafa, wilayani Tarime, mkoani Mara.

Waziri Mkuu amesema kuwa zabuni zimekwishatangazwa na kazi itaanza kabla mwezi Machi haujaisha.

“Serikali inataka wakulima walitumie soko hilo kupeleka mazao yao ili wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi wakanunue mazao katika soko hilo.”

Ametumia mkutano huo kuwaagiza mameneja wa TANESCO katika mikoa na wilaya nchini wapige kambi vijijini na kutoa huduma hapohapo ili kurahisisha ulipaji wa gharama za kuunganishiwa umeme badala ya kusubiri kufuatwa makao makuu.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema watumishi wa umma wanapaswa kuweka ratiba ya kuwatembelea wananchi walioko vijijini ili wawasikilize na kuwapatia ufumbuzi wa matatizo waliyonayo.

“Hapa nimepokea hoja kwenye mabango na Rorya pia nimepokewa na mabango. Hii ni dalili kuwa watu wana kero zao lakini hawana majibu.

"Watumishi wa umma mnatakiwa kila siku muwe na ratiba ya kuwatembelea wananchi kwenye maeneo yao, mkae kwa utulivu na kusikiliza hoja zao.

"Pia mchukue hoja hizo na kuzipatia majibu hukohuko, wananchi wasisumbuke kuja kuwafuata ofisini,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesisitiza kuwa: “Masuala mengi yanayoelezwa kwenye haya mabango ni ya kiutendaji, yanawahusu ninyi na ndiyo maana nimekuwa nasisistiza kuwa kati ya siku sita za kazi, mtenge siku tatu hadi nne, mpite vijijini kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news