Waziri Mkuu ataka halmashauri zifanye ubunifu

*Ni kwenye miradi ya kimkakati ili kuongeza mapato

MARA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewetaka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya wawe wabunifu na waandae miradi ya kimkakati ili kuongeza mapato ya wilaya hiyo.
Ametoa wito huo leo Jumatano, Februari 28, 2024 wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Utegi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Usogo, wilayani Rorya, mkoani Mara.

“Nimepokea maombi wa Waheshimiwa Wabunge juu ya haja ya kuwa na soko kule mpakani na stendi kubwa hapa Utegi. Halmashauri mnayo dhamana ya kujenga kituo cha mabasi na miradi mingine ya kimkakati, ni kitu kizuri ili mradi mpange jinsi ya kukusanya mapato,” amesema.

“Ninawaagiza muwe wabunifu kwenye Halmashauri yenu. Andaeni andiko na mnaweza kuamua kulipeleka TAMISEMI ambako wana mfuko maalum na kama wakiridhika na andiko lenu wanawapatia mkopo.

Au mnaweza kwenda Benki ya TIB ambako mtawaeleza jinsi mtakavyolipa kulingana na makusanyo,” amesema.

Kuhusu afya, Waziri Mkuu amewaeleza wananchi hao kuwa alienda kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Halmashauri hiyo ambako zilitolewa sh. bilioni 3.5.

“Hospitali hizi zinapaswa kuwana na majengo 27, ninyi mmeanza na majengo 16 ambapo saba yamekamilika na tisa yanaendelea kujengwa.”

Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani aliamua kuwe na hospitali za Halmashauri badala ya kutegemea hospitali za wilaya peke yake.

“Kwa maana hiyo kama kuna Halmashauri mbili, kila moja itakuwa na hospitali yake na zote zinajengwa kwa hadhi ileile kama ya hospitali ya wilaya.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news