Waziri Simbachawene aelekeza kusimamisha mishahara ya viongozi walioshindwa kuwasimamia watumishi kutekeleza zoezi la PEPMIS

NA LUSUNGU HELELA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amemuelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi kusimamisha mishahara ya viongozi walioshindwa kuwasimamia watumishi wao kujisajili na kujaza mipango kazi yao katika Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma na Taasisi za Umma (PEPMIS/PIPMIS) na kukwamisha utekelezaji wa zoezi hilo lenye masilahi mapana katika utumishi wa umma na taifa kwa ujumla.
Mhe. Simbachawene ametoa maelekezo hayo leo mkoani Iringa alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara wakati akifungua baraza hilo.
Amesema, ujenzi wa mfumo wa PEPMIS/PIPMIS pamoja na mifumo mingine ya TEHAMA ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kwa dhati kuwa na Serikali ya kidijitali itakayorahisisha utendaji kazi wa watumishi wa umma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Mfumo huu wa PEPMIS na PIPMIS ni mbadala wa Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji kazi (OPRAS) na Mfumo wa Mikataba wa Utendaji Kazi wa Taasisi (IPCS) ulioonekana kuwa na changamoto za usimamizi wa utendaji kazi zilizojitokeza katika utekelezaji wa mfumo wa awali wa OPRAS hivyo mfumo huu umeboreshwa ili kuondokana na changamoto hizo, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kushiriki kikamilifu katika kutekeleza mfumo huu muhimu,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Amesema, mifumo hii ya TEHAMA ni nyenzo muhimu katika kutekeleza majukumu na inalenga kuleta tija, ufanisi na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya watumishi wa umma na nchi kwa ujumla.

Amesema,wanaotakiwa kuwajibishwa kwanza kwa kushindwa kutekeleza zoezi hili la PEPMIS/PIPMIS ni viongozi ambao wameshindwa kuwasimamia watumishi wao, hivyo hatua za kusimamisha mshahara zianze kwa viongozi huku watumishi ambao hawajatekeleza wapewe muda wa kutekeleza na wakishindwa, hatua zichukuliwe kwa watumishi hao.

Vilevile, amekemea tabia ya baadhi ya Waajiri kukataa kuwapokea watumishi wanaohamishiwa kwenye taasisi wanazoziongoza na baadhi kutoruhusu watumishi kuhama hata pale inapoelekezwa na Mamlaka kwani kwa kufanya hivyo ni ukosefu wa maadili na ni jambo ambalo halikubaliki.
‘’Hili jambo sio sahihi kwenye Utumishi wa Umma kwani kuna baadhi ya Waajiri wanaendesha ofisi za Umma kwa utashi na matakwa binafsi,’’ amesisitiza Mhe. Simbachawene.

Akitoa maelezo ya awali kuhusu baraza hilo, Katibu Mkuu-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo amesema elimu ya utekelezaji wa Mifumo ya TEHAMA ikiwemo Mfumo wa PEPMIS/PIPMIS na Mfumo wa Kubaini Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma (HR Assessment) imetolewa nchi nzima lakini kumekuwa na kutowajibika kwa baadhi ya viongozi katika kuwasimamia watumishi wao kutekeleza zoezi hilo.

Katibu Mkuu Mkomi amesema hatua zimeshaanza kuchukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa kwa wote ambao wameshindwa kutekeleza zoezi hilo.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wajumbe wa Baraza, Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara, Bw. Joel Kaminyoge amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha masilahi na stahiki za watumishi wa umma nchini kwani malalamiko mengi ya watumishi ikiwemo kudai stahiki zao yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Amesema, kufuatia maboresho makubwa aliyoyafanya Mhe. Rais, jukumu walilo nalo sasa ni kuwahimiza watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kutoa huduma bora kwa umma kama ambavyo serikali imekusudia.

Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara lilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa Umma Sura 105.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news