Wewe uwe Academi, Mimi shule kawaida, Tutakutana chuoni

NA LWAGA MWAMBANDE

KWA mujibu wa Wikipedia, elimu kwa maana pana ni tendo au uzoefu wenye athari ya kujenga akili,tabia ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi.
Aidha, katika dhana ya kiufundi, elimu ni njia ambayo hutumiwa makusudi na jamii kupitisha maarifa,ujuzi na maadili kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine.

Vile vile, kujifunza ni kutaka kujua juu ya jambo fulani ambalo hukulijua kabla.

Hata jambo zuri kuhusu kujifunza ni kwamba hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kukiweka mbali nawe kitu hicho ambacho umejifunza.

Walimu wanapaswa kuelewa somo vilivyo ili kuwasilisha umuhimu wake kwa wanafunzi.

Shabaha hapa ni kuunda misingi ya ujuzi kamili ambayo wanafunzi wanaweza kutumia kujijenga zaidi, kwani wamewekwa wazi kwa matukio mbalimbali ya maisha.

Ndiyo maana walimu wazuri huweza kutafsiri habari kama hukadiria vizuri, hutumia mazoea na hekima hadi kwa elimu husika ambayo mwanafunzi anaweza kuelewa, kuhifadhi na kupititishia wengine.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, bidii katika kujifunza ni nguzo muhimu ambayo itakufanya uendelee kuwa shujaa darasani bila kujali umesoma shule za kawaida au academi. Endelea;

1.Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni,
Uonekane msomi, nionekane mjeda, fainali i mbeleni,
Na wala sikutazami, utaniona mkuda, sote twaenda shuleni,
Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni.

2. Unapanda basi lako, miye kwenye daladala, sote tuko darasani,
Unasoma lugha yako, kwa hiyo nimechalala, ni mmoja mtihani,
Naliona begi lako, waweka hata vyakula, langu halionekani,
Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni.

3. Usidhani nafurahi, jinsi ninahangaika, ndio hali ya nyumbani,
Sipati sitafutahi, mara nyingi napigika, napo siendi mtoni,
Masomo yangu yaswihi, siwezi yapa talaka, yakafia mtaroni,
Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni.

4. Maisha ya duniani, wahenga walishasema, fainali uzeeni,
Tunasumbuka njiani, kwa bidii tunasoma, majibu ni uzeeni,
Wazazi watuamini, kwamba tutajasimama, tukivuka mitihani,
Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni.

5.Mshukuru Mungu wako, wazazi wana nafasi, ungeishia sokoni,
Ifanye bidii yako, kusoma shule kwa kasi, usiishie njiani,
Pata matokeo yako, yaiondoe mikosi, hapa kwetu duniani,
Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni.

6. Nasema miye niliko, mazuri yaendelea, elimu i mkononi,
Tunasoma maandiko, na mimi sitachelea, kuwa kama msibani,
Nafanya yenye mashiko, shule sitaichezea, hadi kule kileleni,
Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni.

7. Huyo amekupa wewe, mimi ndio kaninyima, yote hayo shukurani,
Tusiishi kama mwewe, vifaranga vyamkoma, shule tuipe imani,
Ni faida ya wenyewe, wazazi wakishakoma, tutilie maanani,
Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni.

8.Mtoto unayesoma, hiyo shule akademi, wazazi wa mtegoni,
Kwa sana wanajinyima, wakufanye we msomi, usiwatie shakani,
Kwa tabia mbaya koma, utasutwa kwa ulimi, naki maneno ya kidini,
Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni.

9.Navipenda hivi vyuo, havinaga ubaguzi, sote twenda darasani,
Cha ajabu kwenye vyuo, wote kwa moja saizi, tunafika kileleni.
Wawe nazo nzuri nguo, na hata kwa matanuzi, kwa walimu sote duni,
Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni.

10.Sidhani naona wivu, kwa hapo wewe ulipo, hayo ni mambo ya chini,
Niseme nakupa shavu, nami ningekuwa hapo, ndo hivyo tena jamani,
Tukiwa wakakamavu, maisha siyo kichapo, tutafika kileleni,
Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni.

11.Chuoni ndio darasa, la maisha linaanza, kisha twaenda sokoni,
Tukishapigwa msasa, na mazuri kujifunza, twafunzwa ya duniani,
Na hali halisi sasa, ukurasa tunaanza, hatuishii njiani,
Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni.

12.Watoto wetu tambua, maisha si lelemama, hebu nyote komaeni,
Wazazi wanatambua, mnataka mambo mema, wawahimiza someni,
Shule zote zinajua, kutoa yenye hekima, mlipo sione soni,
Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni.

13. Tamanio langu mimi, tufike ule wakati, shule ziwe kivyuoni,
Ili watoto wasomi, wote wawe katikati, sio wengine angani,
Tuachane na umimi, kwa kuweka mkakati, wa shule ziwe makini,
Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni.

14. Maisha ndivyo yalivyo, siyo ya kishule shule, sote twaanzia chini,
Haijalishi ulivyo, au ulosoma shule, kwetu sote mtihani,
Tukomae tutakavyo, maisha yaende mbele, sote tuko duniani,
Wewe uwe akademi, mimi shule kawaida, tutakutana chuoni.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news