Ameondoka Lowassa, Jina lake linabaki

NA LWAGA MWAMBANDE

FEBRUARI 10,2024 Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Tisa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipokea nafasi hiyo kutoka kwa Mheshimiwa Fredrick Tluway Sumaye alifariki.
Lowassa alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia Desemba 30, 2005 hadi Februari 7, 2008 alipojiuzulu na hatimaye kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri.Alikifuatiwa na Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda.

Taarifa za kifo cha Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa zilitolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Isdori Mpango kupitia runinga ya Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC).

"Amefariki leo (Februari 10,2024) akipatiwa matibabu kwa ugonjwa wa kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu. Hayati Ngoiyai Lowassa ameugua kwa muda mrefu na amekuwa akipatiwa matibabu tangu tarehe 14 mwezi Januari mwaka 2022,"alisema Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Mpango.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, Waziri Mkuu mstaafu Edward Ngoyai Lowassa ameondoka, lakini jina lake linabaki. Endelea;

1.Kweli baba kaondoka, tuimbe mazuri yake,
Yale yaliyofanyika, katika uhai wake,
Chapa haitafutika, kwetu ni mchango wake,
Ameondoka Lowassa, jina lake linabaki.

2.Wenye akili timamu, wakumbuka enzi zake,
Kazi alizohitimu, kwenye utumishi wake,
Alifanya ya muhimu, katika kipindi chake,
Ameondoka Lowassa, jina lake linabaki.

3.Machache nitayataja, kati yale mengi yake,
Hayo ninajenga hoja, ya kwamba tumkumbuke,
Yalotuleta pamoja, kuenzi maisha yake,
Ameondoka Lowassa, jina lake linabaki.

4.Hasa akiwa waziri, katika wizara zake,
Alikuwa ni mahiri, akijenga hoja zake,
Kwa kweli wengi twakiri, alifanya kazi yake,
Ameondoka Lowassa, jina lake linabaki.

5.Pale Mnazi Mmoja, kumbukeni enzi zake,
Pangeliuzwa kimoja, miliki yetu itoke,
Alisema neno moja, biashara mwisho wake,
Ameondoka Lowassa, jina lake linabaki.

6.Mwakumbuka City Water, na yao mengi makeke,
Maji Dare ni utata, akaipiga mateke,
Kulalama City Water, kesi ushindi ni wake,
Ameondoka Lowassa, jina lake linabaki.

7.Maji Ziwa Victoria, anao mchango wake,
Mkapa limtumia, katika mipango yake,
Sasa tunafurahia, hayo matumizi yake,
Ameondoka Lowassa, jina lake linabaki.

8.Siasa ustarabu, Lowassa ni chata yake,
Matusi hakuyajibu, akifanya mambo yake,
Alifwata taratibu, kwenye harakati zake,
Ameondoka Lowassa, jina lake linabaki.

9.Kama Waziri Mkuu, nafasi ya juu kwake,
Figisu zikawa juu, wakitaka roho yake,
Tunazo zake nukuu, ule uamuzi wake,
Ameondoka Lowassa, jina lake linabaki.

10.Lingine hili ni jema, katika maisha yake,
Kalea watoto vema, pamoja na mke wake,
Sasa waliko wavuma, kwa adabu si makeke,
Ameondoka Lowassa, jina lake linabaki.

11.Toka kuhitimu kwake, katika elimu yake,
Wote utumishi wake, siasa likuwa yake,
Ilifanya apikike, aive nafasi zake,
Ameondoka Lowassa, jina lake linabaki.

12.Pole nyingi tunatoa, hiyo familia yake,
Mungu amemuondoa, umekwisha muda wake,
Faraja aweze toa, kumbukeni wema wake,
Ameondoka Lowassa, jina lake linabaki.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news