Ajali ya lori la mafuta, mabasi ya abiria Pwani

PWANI-Askari wawili wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wamejeruhiwa wakiwa katika harakati za kuokoa marehemu waliokuwa wamenasia kwenye gari.

Ni baada ya kuzuka moto ghafla na magari kuwaka moto kutokana na mlipuko wa lori la mafuta katika Bonde la Ruvu mkoani Pwani.
Kamanda wa Polisi Mkoa Mkoa wa Pwani, SACP Pius Lutumo amewataja askari waliojeruhiwa kuwa ni Koplo Elias Bwire na Koplo Hamisi Kungwi ambao wote wamekimbizwa Hospitali ya Taifa Mloganzila kwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.

"Machi 28,mwaka huu majira ya saa 10:15 alfajiri katika bonde la Ruvu Wilaya ya Kipolisi Mlandizi, Mkoa wa Pwani barabara ya Morogoro, Dar es Salaam gari namba T668 DTF aina ya Scania Kampuni ya Sauli ikiendeshwa na dereva Idd Aloyce (35) mkazi wa Mafinga ikitokea Dar es Salaam kwenda Mbeya liligonga ubavuni lori la mafuta ya Petroli.

"Lenye namba za usajili RAF672N na tela lenye namba RL2594 aina ya Howo lililokuwa linatoka Dar es Salaam kwenda nchini Rwanda likiendeshwa na dereva Mushimana Musiyimana lililokuwa limesimama kupisha gari lililokuwa linakuja mbele yake."

Kamanda huyo amesema, basi hilo lilikuwa limeongozana na basi la Golden Deer la Kampuni ya New Force lenye namba za usajili RAF672N na likiendeshwa na dereva aitwaye Burton Jacob (33) mkazi wa Mbeya ambapo nalo lililigonga kwa nyuma basi la Saul lililokuwa mbele yake.

Amesema, ajali hiyo imesababisha vifo vya watu wawili ambao hawakufahamika majina yao na majeruhi watatu ambao ni Salimu Daud (50) mkazi wa Mbozi Mbeya, Farida Idrisa (26) mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam na Kiambile Geofrey mkazi wa Uyole Mbeya.
RPC Lutumo amesema, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa madereva wa mabasi yote mawili kushindwa kuchukua tahadhari kwa kuyapita magari mengine, lakini pia kushindwa kutunza umbali kati ya gari moja na lingine huku yakiwa yamefuatana.

"Pamoja na hayo uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya injini ya basi la Saul iliyokua imekita chini baada ya kugonga gari lingine na kulipua petroli wakati wa uokoaji,"amesema RPC Lutumo.

Amewataka madereva kutii sheria za Usalama Barabarani kwa mujibu wa taaluma zao na ifahamike kwamba madereva wanachukua dhamana kubwa ya maisha na mali za watu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema, atayafungia mabasi yatakayoendelea kuvunja sheria za usalama barabarani baada ya ajali hiyo.

Amesema, yeye ameamua kwa kushirikiana na wanaotoa lesseni, LATRA na Jeshi la Polisi kuwa wataweka mkakati wa kudhibiti ajali ndani ya Mkoa wa Pwani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news