Asali kutoka Tabora yatikisa kwa ubora duniani,TFS yabainisha mengi

NA GODFREY NNKO

KAMISHNA wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),Prof.Dos Santos Silayo amesema, uzalishaji wa mazao ya nyuki nchini umeongezeka hadi kufikia wastani wa tani 32,691 kutoka tani 31,179 sawa na ongezeko la asilimia tano huku asali ya Tabora ikiongoza kwa ubora duniani.
Ni mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Prof.Silayo ameyasema hayo leo Machi 19,2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri wakiwemo waandishi wa habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Amesema, asali inayozalishwa mkoani Tabora imeshika nafasi ya pili kwa ubora kupitia mashindano ya ubora wa asali zinazozalishwa barani Afrika.

Aidha, kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita Tanzania imeuza jumla ya tani 5.6 za asali nje ya nchi yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 40.

TFS ambayo ipo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii huku ikiwa miongoni mwa taasisi na mashirika yaliyopo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ulianzishwa kisheria kupitia Tangazo la Gazeti la Serikali (GN 269) la Julai 30,2010 na kuzinduliwa rasmi Julai 18,2011

Kuanzishwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu ni kwa mujibu wa Sheria ya Wakala "The Executive Agencies Act Cap. 245 (Revised Edition 2009)”, pamoja na Sera ya Misitu ya mwaka 1998.

Nyingine ni Sera ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998, Sheria za Misitu na Nyuki Sura 323 na Sura 224 za mwaka 2002.

Prof.Silayo amesema, asali ya Tanzania hupimwa katika maabara za Kimataifa za ithibati kila mwaka na kwa miaka yote Tanzania imepata alama za juu za wastani 96/100.

“Masoko makubwa yako nchi za Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, Uarabuni, Marekani na EAC na SADC.”

Prof.Silayo amebainisha kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt.Samia wamefanikiwa kuimarisha sekta ya uhifadhi, kutoa ajira kwa askari na maofisa zaidi ya 500 na ujenzi wa miundombinu.

Amesema,mafanikio hayo yanatokana na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kujali na kuthamini uhifadhi nchini.

Vile vile amesema,Rais Dkt.Samia anatoa msukumo wa moja kwa moja yeye binafsi,  hivyo kuifanya sekta ya misitu na hifadhi nchini kustawi.

Prof.Silayo amesema, wakala umeongeza wigo wa upandaji miti ya aina mbalimbali huku wakihudumia wadau zaidi ya 11,670 kutokana na malighafi za misitu.

"Viwanda vya misitu hujumuisha vile vidogo vya kutengeneza samani, uchakataji mbao, utengenezaji bidhaa zilizohandisiwa kama vile marine boards na veneer

"Viwanda vya nishati ya mkaa, viwanda vya nguzo hadi vile vikubwa vya kutegeneza karatasi.

"Wadau hawa hupata malighafi toka misitu na mashamba ya watu binafsi na sehemu kubwa toka misitu ya serikali, taarifa zinaonesha tunahudumia wadau takribani 11,670 nchi nzima."

Prof.Silayo amesema, wenye viwanda vya kati na vikubwa waliongezeka toka 6029 hadi 7356 sawa na ongezeko la asilimia 18 katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt.Samia.

"Katika kipindi cha miaka mitatu kiasi cha meta za ujazo 4,485,488.31 kilivunwa katika misitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenye mashamba ya miti."

Amesema, mwaka huu wa fedha 2023/2024 imepangwa kuvuna kiasi cha meta za ujazo 1,218,082 na mwaka 2024/2025 kiasi cha meta za ujazo 1,245,019 zinatarajiwa kuvunwa.

Prof.Silayo amebainisha kuwa, takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu uuzaji bidhaa za misitu nje ya nchi uliongezeka kwa asilimia 87.

Ni kutoka meta za ujazo 227,615 mwaka 2020/21 hadi meta za ujazo 356,593 kwa mwaka 2021/2022 hadi meta za ujazo 426,805 kwa mwaka 2022/2023.

"Katika kipindi cha miaka mitatu jumla ya ujazo wa mazao ya miti yaliyosafirishwa kwenda nje ya nchi ni meta za ujazo 1,011,013.

"Hii inatokana na viwanda vingi kuanza kutengeneza bidhaa zao nchini badala ya kusafirisha malighafi pekee kwenda nje ya nchi."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news