Bunifu zimewezesha Sekta ya Fedha nchini kustawi-Prof.Ishengoma

NA GODFREY NNKO

SEKTA ya Fedha nchini imepiga hatua kubwa huku bunifu na mazingira wezeshi yakiwezesha wananchi kupata huduma karibu na mazingira wanayoishi.
Hayo yamesemwa leo Machi 8, 2024 na Prof.Esther Ishengoma ambaye ni Mratibu wa Kituo cha Utafiti kuhusu Huduma za Kibenki na Fedha katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS).

Ni katika siku ya pili ya Kongamano la 21 la Taasisi za Fedha (COFI) linaoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.

Kongamano hilo la siku mbili ambalo limeanza Machi 7, mwaka huu limefunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Mpango.

Aidha, linaongozwa na kauli mbiu ya "Kuimarisha Ustahimilivu wa Sekta ya Fedha Nyakati za Changamoto za Kiuchumi" ambapo limeandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Mabenki Tanzania (TBA).

Prof.Ishengoma akiwasilisha mada ya Ustahimilivu wa Sekta ya Fedha wakati wa Changamoto za Kiuchumi; Sheria za Usimamizi,Ubunifu na Usimamizi wa Vihatarishi amesema, kwa asilimia kubwa Tanzania imepiga hatua.

“Na bunifu zimewezesha tangu mwaka 2007/08 kuwa na bidhaa mpya za huduma za kifedha ikiwemo kutuma na kupokea fedha kwa njia ya simu za mkononi, hii ni hatua kubwa.

“Pia, mtakumbuka mwaka 2014 huduma za kifedha kidigitali zilipanuka zaidi ambapo tulianza kushuhudia watu wakijiwekea akiba, wakipata mikopo, bima, akiba za vikundi, mikopo ya vikundi na nyinginezo.”

Pia amesema, wananchi wamepata uwanda mpana wa kufanya uwekezaji mseto katika hisa na dhamana mbalimbali kupitia mifuko kama vile UTT Amis huku huduma ndogo za fedha zikiendelea kuwanufaisha.

Prof.Ishengoma ameongeza kuwa, bunifu mbalimbali katika sekta ya fedha hususani upande wa mikopo na akiba kidigitali zinazotolewa na watoa huduma nchini ikiwemo Airtel Timiza, Airtel Vikoba, Timiza Akiba, Songesha, M-Powa, Mgodi, Bima Kidigitali.

M-Koba, Insurance Loan, Tigo Nivushe Plus, Mshiko Fasta, Tigo Kibubu na Floti Fasta kadri zinavyotumika kwa malengo yaliyokusudiwa zimekuwa zikiwasaidia wananchi wengi licha ya changamoto ya riba na masharti.

Vile vile amesema, maboresho ni makubwa katika sekta ya fedha,lakini bado kuna changamoto ya wananchi kuendelea kutunza fedha zao nyumbani kuliko katika mifumo rasmi ya kifedha kwa maana ya benki na sekta nyinginezo za kifedha nchini.

Katika hatua nyingine amesema, Serikali imeendelea kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha kunakuwepo na sheria, kanuni na miongozo ambayo inawapa dira watoa huduma za fedha kuhakikisha wanawahudumia wananchi bila kuwaumiza.

Vile vile ameshauri kuwa, ili kuwapa nafasi wananchi wengi kutumia fursa za mikopo kuna umuhimu kwa watoa huduma za kifedha kuhakikisha wanatoa mikopo ambayo riba ni himilivu ili waweze kukopa kwa wingi kuendeleza miradi, huduma na biashara zao.

ELIMU

Kwa upande wake,Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Wananchi Zanzibar (PBZ), Dkt.Muhsin Salim Masoud amesema kuwa,uimara na uendelevu wa Sekta ya Fedha unachangiwa kwa kiasi kikubwa na elimu kwa umma.

“Elimu ni suala muhimu sana hususani katika kipindi ambacho tunapitia changamoto mbalimbali za kiuchumi ili kuwapa uelewa wa kutosha wananchi.”

Prof. Ulrich

Profesha Ulrich Volz ambaye ni Profesa wa Uchumi na Mkurugenzi wa Kituo cha Fedha Endelevu katika SOAS, Chuo Kikuu cha London amesema, mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa chanzo cha maafa makubwa yanayojumuisha mafuriko, ukame na mengineyo yamekuwa kikwazo katika ukuaji wa uchumi,kwani yanachangia ukuaji wake kwenda taratibu.

“Kwa hiyo, athari za pamoja za vipindi virefu vya kiangazi na matukio ya mvua kubwa huenda zikapunguza kasi ya ukuaji uchumi.”

Amesema, hali hiyo imekuwa ikiathiri kwa kiwango kikubwa sekta muhuhimu katika uchumi ikiwemo kilimo, miundombinu, nishati na nyinginezo huku akibainisha kuwa, kuna umuhimu wa watunga sera kuja na mikakati ya muda mrefu ambayo itawezesha kuokoa jahazi.

"Wahusika wote katika mifumo ya kifedha wanatakiwa kuelewa na kushughulikia hatari za hali ya hewa zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news