Cuba, Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kimkakati

DAR ES SALAAM-Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt.Emmanuel John Nchimbi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba, nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne Vera.
Katika mazungumzo hayo Dkt. Nchimbi na Mhe. Balozi Vera wamejadiliana juu ya masuala mbalimbali yanayohusu namna ya kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Tanzania na Cuba na Chama Cha Mapinduzi na Chama Cha Kikomunisti cha Cuba (CPC).

Wakati wa mazungumzo hayo yaliyofanyika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar Es Salaam, leo Jumamosi Machi 5, 2024, Mhe. Balozi Vera ameishukuru Tanzania na CCM kwa jinsi ambavyo daima wamesimama na nchi hiyo katika nyakati zote.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Nchimbi amemhakikishia Mhe. Balozi Vera kuwa CCM, chini ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kitafanya kila linalowezekana kuhakikisha urafiki na uhusiano kati ya Tanzania na Cuba kwa upande mmoja na CPC na CCM kwa upande mwingine unaenziwa na kuimarishwa zaidi kwa ajili ya manufaa ya pande zote mbili.

Kupitia majadiliano hayo, pamoja na masuala mengine, viongozi hao wa pande zote mbili, wamejadiliana na kuainisha maeneo yatakayofanyiwa kazi kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha ushirikiano kati ya Wananchi wa Tanzania na Wananchi wa Cuba, Serikali za nchi zote mbili na vyama vinavyoongoza nchi hizo, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza mipango ya kubadilishana utaalam katika maeneo mbalimbali na kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news