Ilemela yakabidhiwa mpango wa usimamizi wa maafa

MWANZA-Serikali imekabidhi nyaraka za usimamizi wa maafa katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza huku ikisisitiza kuwa, ni muhimu masuala hayo kujumuishwa katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku siku ili kuendelea kuwa na matokea chanya katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini.
Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala akikabidhi nyaraka za usimamizi wa maafa kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masala wakati wa uzinguzi wa nyaraka hizo katika wilaya hiyo jijini Mwanza.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia matukio wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Nyaraka za Usimamizi wa Maafa katika halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.

Wito huo umetolewa Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala akimwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Nyaraka za Usimamizi wa Maafa katika halmashauri hiyo.

Nyaraka zilizokabidhiwa ni pamoja na za Matokeo ya tathmini ya vihatarishi, mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa na mkakati wa kupunguza vihatarishi vya maafa nchini.
Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala akikabidhi nyaraka za usimamizi wa maafa kwa Mbunge wa Ilemela Dkt. Angelina Mabulla wakati wa uzinguzi wa nyaraka hizo katika wilaya hiyo jijini Mwanza.

Amesema kuwa uandaaji wa nyaraka hizo za usimamizi wa maafa ni hatua nzuri kueleka katika ujenzi wa jamii iliyo stahimilivu dhidi ya majanga katika Manispaa ya Ilemela.

Brigedia Jenerali Ndagala ametoa wito kwa Idara, Vitengo na Taasisi zote zilizopo katika Halmashauri hiyo kuzingatia dira hii katika kutekeleza vipaumbele vya kisekta.

“Nitoe wito kwamba, nyaraka hizi zilizoandaliwa ziwe ni chachu ya kuongeza ushirikishwaji wa jamii na wadau, kujenga uelewa wa jamii kuhusu masuala ya usimamizi wa maafa,kuimarisha mfumo wa utoaji tahadhari ya awali, kujenga uwezo wa kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa na maafa na kujenga uwezo wa kukabiliana na maafa,"alieleza.
Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala akikabidhiwa nyaraka za usimamizi wa maafa na Bi. Dorothy Pantaleo Mratibu wa Maafa wa Ofisi hiyo wakati wa halfa ya kuzindua na kukabidhi nyaraka hizo Ilemela Mwanza.

Amebainisha kuwa matokeo ya tathmini ya maafa iliyofanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mwezi Februari, 2024 yameonesha kuwa Manispaa hiyo imekuwa ikikabiliwa na maafa.

Ameeleza kuwa maafa hayo yamekuwa yakisababishwa na majanga ya mafuriko, upepo mkali, moto, magonjwa ya mlipuko pamoja na ajali za barabarani na majini.

Amesema anatambua kwa sasa Manispaa hiyo inakabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu hivyo kuwapongeza kwa jitihada wanazoendelea nazo katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Aidha, amewasisitiza kuendelea kuchukua jitihada mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia matukio wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Nyaraka za Usimamizi wa Maafa katika halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.

“Ni imani yangu kuwa matokeo ya tathmini iliyofanyika yamezingatiwa ipasavyo katika kuandaa Mpango wa Kujiandaa na Kukabili Maafa na Mkakati wa Kupunguza Vihatarishi vya Maafa katika Manispaa ya Ilemela.

"Hivyo, ni matumaini yangu kuwa, mpango huu utasaidia sana kuongeza ufanisi katika kukabiliana na maafa kwa kuwa unaainisha majukumu ya wadau wote wanaohusika na masuala ya maafa katika Manispaa ya Ilelemela kabla, wakati na baada ya maafa kutokea,"amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masala ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kuratibu masuala ya maafa nchini huku akieleza kuwa, wamepokea nyaraka hizo za Usimamizi wa Maafa ili kuendelea kuwa na nguvu ya pamoja katika kukabiliana na maafa nchini.
Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala (katikati waliokaa) pamoja na meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na wanakamati wa hafla ya Uzinduzi wa Nyaraka za Usimamizi wa Maafa katika halmashauri hiyo.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa Wilaya itautumia kwa manufaa huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha jamii inakuwa stahimilivu katika masuala ya menejimenti ya maafa.

“Tutaendelea kutoa elimu kuhusu masuala haya ya maafa na kuhakikisha kamati yetu ya maafa inatekeleza kikamilifu majukumu kwa tija na matokeo yaliyokusudiwa,”alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news