Jitafute ujipate

NA LWAGA MWAMBANDE

REJEA katika Biblia Takatifu katika Kitabu cha Yeremia 29:11-13, neno la Mungu linasema..."Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.
Picha na Yourstory.

"Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza.Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote."

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa,unapojotafuta ili uweze kutimiza ndoto na kuyafikia malengo yako, zingatia kumshirikisha kila hatua Mungu, maana anayajua mawazo yako. Endelea;

1. Ni vema kujitafuta, kichwakichwa usiende,
Si kuokotaokota, na mwisho tenge uende,
Maarifa mengi chota, upande wako uende,
Jitafute ujipate, ndipo utafanikiwa.

2.Umekuja duniani, una kusudi utende,
Mungu wako wa mbinguni, ataka kitu utende,
Wala hakuachi duni, uloeloe umande,
Jitafute ujipate, ndipo utafanikiwa.

3.Kila mtu duniani, kapewa kitu atende,
Hili jambo la imani, si hovyohovyo ukwende,
Ung’ang’ane maishani, mbegu hovyo usipande,
Jitafute ujipate, ndipo utafanikiwa.

4.Waweze kitu kupenda, utake huko uende,
Kumbe moyo umepinda, tamaa mbele ni tende,
Utasota na kukonda, na popote usiende,
Jitafute ujipate, ndipo utafanikiwa.

5.Hapo wakati mwingine, magoti vema wende,
Usiulize kwingine, madhabahuni upande,
Mungu mwenye akuone, kwako mema ayatende,
Jitafute ujipate, ndipo utafanikiwa.

6.Pengine wewe kilimo, mazao mengi upande,
Kwa hiyo kama masomo, upande huo uende,
Utaongezeka kimo, kipato chako kipande,
Jitafute ujipate, ndipo utafanikiwa.

7.Pengine wewe mwimbaji, jukwaa hilo upande,
Huo ni wako mtaji, upende na usipende,
Huduma yakuhitaji, mengine yote yavunde,
Jitafute ujipate, ndipo utafanikiwa.

8.Watu wengi duniani, maisha kama matende,
Wanakwenda machakani, bila kuwa na upande,
Hawaipati amani, kila kitu ni vibonde,
Jitafute ujipate, ndipo utafanikiwa.

9.Ni bahati mbaya sana, kutoujua upande,
Ule unafaa sana, mambo yako uyashinde,
Tena inauma sana, hadi kifo kiwashinde,
Jitafute ujipate, ndipo utafanikiwa.

10.Kama unajitafuta, mtihani uushinde,
Amani utaipata, yale yako uyatende,
Na mpenyo utapata, hata ngazi uzipande,
Jitafute ujipate, ndipo utafanikiwa.

11.Jitafute ujipate, na hiyo njia uende,
Giza machoni ufute, furaha upate punde,
Raha kote ikufwate, ngazi kivyako upande,
Jitafute ujipate, ndipo utafanikiwa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news