TPHPA yadhibiti kwelea kwelea milioni 40 na kuokoa tani 5,675 mazao ya nafaka

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imefanikiwa kudhibiti ndege aina ya kwelea kwelea milioni 40 ndani ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Prof. Joseph Ndunguru ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHA) ameyasema hayo leo Machi 13, 2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri, waandishi wa vyombo vya habari nchini kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
"Mamlaka imedhibiti ndege aina ya kwelea kwelea milioni 40 na kufanikiwa kuokoa tani 5,675 za mazao ya nafaka ambayo ni mpunga, mtama na alizeti."

Prof.Nduguru amesema, udhibiti huo umefanyika katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Tabora na Manyara kwa kushirikiana na Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani (DLCO-EA).
"Ndege waharibifu hao walidhibitiwa katika maeneo hayo kwa kunyunyizia kiuatilifu aina ya fenthion 60% ULV kwa kutumia ndege (njia ya anga) na kwa kutumia vinyunyizi mbeleko vyenye injini (njia ya ardhini)."

Amesema, mamlaka hiyo ambayo imeanza kazi rasmi Julai, 2022 imeundwa kwa Sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Na.4 ya mwaka 2020 (Plant Health Act No. 04 of 2020.

Ni kwa kuunganisha iliyokuwa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu ya Ukanda wa Kitropiki ( TPRI)-Sheria Na.18 ya 1979) na Kitengo cha Afya ya Mimea kilichokuwa chini ya Wizara ya Kilimo (PHS)-Sheria Na.13 ya mwaka 1997).

Amesema, mamlaka hiyo iliundwa ili kuweka mfumo wa pamoja wa kisheria wa usimamizi na udhibiti wa afya ya mimea, mazao ya mimea na viuatilifu.
Afisa Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao hicho.

Lengo likiwa ni kukidhi matakwa ya masoko na mikataba ya Kimataifa na kuweka mazingira salama kwa afya ya binadamu, wanyama na mimea kwa kuwa na matumizi sahihi na salama ya viuatilifu nchini.

Hata hivyo, licha ya mamlaka hiyo kuwa chini ya Wizara ya Kilimo pia ni miongoni mwa taasisi na mashirika ya umma ambayo yanasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

TR ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa ofisi inayojitegemea kimuundo.
Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) ofisi ilikabidhiwa majukumu ya shirika hilo.

Kikao kazi cha leo na TPHPA ni mwendelezo wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kuzikutanisha taasisi na mashirika hayo ya umma na wahariri ili ziweze kuelezea walikotoka, walipo na wanapoelekea.

Dhamira ikiwa ni ili umma ambao ndiyo wamiliki wa taasisi hizo waweze kupata mwelekeo wake na kufahamu mafanikio yao.

Katika hatua nyingine, Prof. Ndunguru amesema, mamlaka imefanikiwa kukagua uwepo wa visumbufu katika tani milioni 7.72 za mazao mbalimbali kupitia vituo vya mipakani,bandari na viwanja vya ndege yaliyosafirishwa nje ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news