Kigundulika mapema, saratani inapona

NA LWAGA MWAMBANDE

IJUMAA iliyopita Mke wa Mwanamfalme William, Catherine (Kate Middleton) wa Wales alisema kuwa, yuko kwenye hatua za mwanzo za matibabu.
Ni baada ya uchunguzi wa kimatibabu kubaini kwamba anaugua saratani.

Catherine katika ujumbe alioutoa kwa njia ya video alisema ilikuwa mshangao sana kwake baada ya miezi kadhaa ya mahangaiko makubwa.

Ingawa alibainisha kuwa, ana nguvu na anaendelea kupata nafuu kila siku. 

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,saratani ikigundulika mapema inapona, hivyo hakuna kukata tamaa, fika katika vituo vya afya kwa maelekezo. Endelea;

1.Ameanza matibabu, ugonjwa wa saratani,
Lengo hasa kuutibu, usienee mwilini,
Ni kazi ya matabibu, kule hospitalini,
Kigundulika mapema, saratani inapona.

2.Ugonjwa huu watisha, kuutaja mdomoni,
Vile sana unafisha, watu wenda mautini,
Lakini ndio maisha, unatufika mwilini,
Kigundulika mapema, saratani inapona.

3.Kichunguza nchi nyingi, zilizopo duniani,
Magonjwa ya vifo vingi, mmoja ni saratani,
Shida kubwa watu wengi, wanachelewa njiani,
Kigundulika mapema, saratani inapona.

4.Kate ameshatangaza, anaumwa saratani,
Tena ameshaeleza, atibiwa saratani,
Muda wa kujiuguza, akiwa kwake nyumbani,
Kigundulika mapema, saratani inapona.

5.Changamoto hapa kwetu, kugundua saratani,
Ni vigumu sana kwetu, tukisumbuka mwilini,
Kuona waganga wetu, kuicheki saratani,
Kigundulika mapema, saratani inapona.

6.Watalamu wanasema, kuihusu saratani,
Kigundulika mapema, kwenye sehemu mwilini,
Kwa uhakika kupima, tiba kamili njiani,
Kigundulika mapema, saratani inapona.

7.Aina ya saratani, iathiriyo mwilini,
Muda wa kuwa mwilini, ikipimwa vipimoni,
Inaleta kuamini, itaondoka mwilini,
Kigundulika mapema, saratani inapona.

8.Hatua ile ya kwanza, kigundua saratani,
Tiba maramoja anza, pambana na saratani,
Dawa nguvu zinatenza, lakini mwisho amani,
Kigundulika mapema, saratani inapona.

9.Hata hatua ya pili, ugonjwa wa saratani,
Gonjwa haliendi mbali, linadhibitiwa chini,
Mtu arudia hali, ya kuridhisha mwilini,
Kigundulika mapema, saratani inapona.

10.Kate tunampa pole, ugonjwa wa saratani,
Na wagonjwa wote pole, nyumbani hospitalini,
Lakini wasonge mbele, kwa tiba ya saratani,
Kigundulika mapema, saratani inapona.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news