Kitita kipya NHIF kilivyobeba nafuu huku wadau wakipewa neno

NA GODFREY NNKO

WATOA huduma katika Sekta ya Afya wametakiwa kutambua kuwa, uhai wa mtu hauwezi kulinganishwa na kitu chochote, hivyo ni wajibu wao kuwahudumia wananchi na kuepuka kutoa taarifa ambazo zinaweza kusababisha hofu na taharuki.

Hayo yamebainishwa Machi 5,2024 katika kikao kazi kati ya wahariri, wanahabari na wataalamu wa afya kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Kupitia kikao hicho,uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Juma Muhimbi uliwapitisha washiriki hao katika Kitita cha Huduma cha NHIF (2023) ambacho kinachotolewa na mfuko huo.

Washiriki akiwemo Steven Chuwa kutoka ITV alifafanua kuwa, "Afya ya mtu, uhai wa mtu ni kitu ambacho hauwezi kukilinganisha na kitu chochote kile.

"Sasa unapotoa taarifa isiyokuwa sahihi kuhusiana na afya ya mtu ni kama unachangia kuua, kwa hiyo taarifa zinapaswa kueleza ukweli na ukweli ambao utasaidia kuponya na si kwamba unakwenda kuangamiza ile afya.

"Kwa hiyo hizi taarifa ambazo zilikuwa zinatoka kiholelaholela siyo za maokoto hizi zinatakiwa ziwe zinachujwa na zinatoka kwenye chanzo cha kuaminika kwa sababu zinashughulika na uhai wa mtu.
"Kwa hiyo ni vitu ambavyo vinatakiwa vidhibitiwe ili kusudi ili tuweze kwenda sambamba, vinginevyo litakuja kuwa janga,"Chuwa alisisitiza.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga amewataka wananchi kutambua kuwa, Kitita Kipya cha NHIF ni orodha ya huduma na bei zake ambazo mfuko huo huingia mkataba na watoa huduma (hospitali) ili kuwahudumia wanachama wake.

Amesema, kitita hicho kipya ambacho kimeanza Machi 1,2024 mwanachama hapaswi kuchangia gharama za matibabu kwa huduma zinazolipiwa na mfuko huo.

Konga amesema,NHIF ilianzishwa kwa Sheria Sura 395 kwa lengo la kusimamia upatikanaji wa huduma za matibabu kwa makundi yanayosajiliwa na moja ya jukumu lake ni kufanya mapitio ya Kitita cha Mafao.

Ni kwa lengo la kuhakikisha kinaendana na mabadiliko mbalimbali yaliyofanyika katika Sekta ya Afya nchini na kwa mujibu wa tathimini ya uhai na uendelevu wa mfuko kama ilivyoainishwa kwenye kifungu cha 39A cha sheria hiyo.

Amesema, maboresho ya kitita yamelenga kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama ikiwa ni pamoja na kuongeza huduma ambazo hazikuwepo awali.

Pia, kufanya maboresho ya huduma na gharama zake kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia na hali halisi ya bei katika soko.
"Ikiwemo kuwianisha Kitita cha Mafao na miongozo ya tiba iliyoboreshwa ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wanufaika wa mfuko.

"Na kuwianisha Kitita cha Mafao na miongozo ya tiba iliyoboreshwa ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wanufaika wa mfuko."

Vile vile amebainisha kuwa, lengo kubwa la kikao hicho ni mwendelezo wa utamaduni wa mfuko kukutana na wadau wake mbalimbali nchini.

Amesema,wanahabari ni kundi moja wapo muhimu ambalo limekuwa likitumia vyombo vyao vya habari kuelimisha wanachama na wananchi kwa ujumla kuhusiana na mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya mfuko wao.

Katika hatua nyingine, Konga aliwataka watoa huduma za afya ambao ni wadau wao kuendelea kuheshimu na kuzingatia mikataba yao ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na wanachama wa mfukko huo.

Miongoni mwa maboresho yaliyofanyika katika kitita hicho kipya ni kuongezwa kwa dawa 247 ikiwa ni suluhu ya mwanachama wa mfuko huo kuwa na uhakika wa kupata dawa vituo vya afya nchini.

Pia,wanachama ambao wanatumia dawa za matibabu ya kisukari na moyo watapata dawa ngazi za chini.

Aidha, kwa sasa huduma za kibingwa na bobezi kwa magonjwa ya figo,saratani na moyo zinapatikana kwenye hospitali za kanda na si lazima kwenda hospitali za ngazi ya Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news