Lazima muheshimu mikataba yenu na NHIF-Waziri Ummy

LINDI-Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, ameelekeza vituo vyote vya afya, ikiwa ni pamoja na vile vya binafsi na vya umma, vilivyosaini mikataba na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kuendelea kutekeleza mikataba hiyo ipasavyo.
Akiongea na vyombo vya habari leo Machi 1, 2024 mkoani Lindi, Waziri Ummy amesisitiza umuhimu wa kila mtoa huduma kwa wanachama wa NHIF kuheshimu na kufuata masharti ya mikataba waliyoingia na NHIF.

Amesema kwamba ni wajibu wa vituo vyote vya afya kutoa huduma kulingana na makubaliano yaliyomo katika mikataba hiyo.

"Kila mtoa huduma za afya kwa wanachama wa NHIF ameingia mkataba na NHIF, hivyo wazingatie masharti ya mikataba walioingia na NHIF katika kuwahudumia wanachama,"amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amezitaka hospitali zote binafsi ambazo zilikuwa zimesitisha kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF kuendelea kutoa huduma hizo.

Amesema, kamati ya kitaalamu imeundwa kwa ajili ya kufanya majadiliano na watoa huduma wakati huduma zikiendelea kutolewa, na kwamba majadiliano hayo yataendelea huku huduma zikiwa bado zinaendelea kutolewa.

Aidha, ameelekeza hospitali zote, za umma na binafsi, kuwapokea wagonjwa wa dharura kulingana na matakwa ya sheria za usajili wa vituo vya afya na kwamba ni kinyume cha sheria kutowapokea wagonjwa wa dharura na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa watakaokiuka agizo hilo.

"Nazielekeza hospitali au vituo vyote binafsi na vya umma kuendelea kuwapokea wagonjwa wa dharura pindi wanapofika katika vituo vyao kwani hili ni takwa la kisheria namba 151 la usajili wa vituo binafsi vya afya na kanuni yake namba 32, kutokuwapokea wagonjwa wa dharura ni kuvunja sheria". Amesema Waziri Ummy

Hata hivyo, Waziri Ummy ametoa onyo kali kwa watoa huduma ambao wamekuwa wakitangaza nia ya kuwaondoa wagonjwa waliopo wodini ndani ya masaa 48. Amesema kuondoa wagonjwa hao ni kinyume cha sheria na ni kuvunja haki za wagonjwa.

“Nimeona habari au tangazo wakisema watawatoa wagonjwa waliopo wodini ndani ya masaa 48 nataka kusema ni marufuku kuondoa wagonjwa waliopo wodini kwasababu kufanya hivyo ni kuvunja sheria ya madakatari,"amesema Waziri Ummy.

Pia, amezitaka hospitali za serikali,kujiandaa vyema na kuweka utaratibu mzuri wa kupokea wagonjwa wengi zaidi ambao wanaweza kushindwa kupata huduma katika vituo binafsi huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma bora za afya kulingana na haki yake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news