Mamia ya watalii wamiminika Kilwa, TAWA yatoa neno huku meli zikipishana

NA BEATUS MAGANJA

REKODI ya idadi ya watalii wa kigeni waliotembelea Hifadhi ya Urithi wa Dunia na Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara iliyo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) tarehe 4 Machi, 2024 imevunjwa baada.
Ni baada ya meli ya nane kutia nanga hifadhini humo ikiwa na watalii 125 kutoka Mataifa mbalimbali na hivyo kufikisha jumla ya watalii 925 waliotembelea hifadhi hiyo katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Februari 3, 2024.
Kwa mujibu wa takwimu za idadi ya watalii wa kigeni waliotembelea hifadhi hiyo katika kipindi cha hivi karibuni mwaka 2024 umetajwa kuwa ni mwaka wenye mafanikio makubwa kwa TAWA kupata safari nyingi za meli za watalii kupitia Hifadhi hiyo yenye urithi wa kihistoria na kiutamaduni, ukongwe wa magofu ya kale yaliyojengwa kwa ustadi mkubwa kiasi cha kustaajabisha na kuvutia watalii mbalimbali wanaotembelea hifadhi hiyo

Imeelezwa kuwa takwimu za miaka mitatu kuanzia mwaka 2022, idadi ya meli zilizotia nanga hifadhini humo zilikuwa mbili (2) zikiwa na zaidi ya watalii 200, ambapo mwaka 2023 meli 3 ziliwasili katika hifadhi husika zikiwa na zaidi ya watalii 300 na mwaka huu wa 2024 meli zipatazo nane zikiwa na zaidi ya watalii 900 zimetia nanga hifadhini humo.
Ongezeko hilo la watalii katika Hifadhi hiyo ni ishara kuwa utalii wa malikale unazidi kuchechemka nchini ukichagizwa na jitihada za dhati zilizofanywa na Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuitangaza Nchi yetu na vivutio vyake kupitia filamu maarufu ya Tanzania The Royal Tour iliyoleta matokeo makubwa kwa muda mfupi.

Pia nguvu kubwa ya kuwekeza katika kuboresha miundombinu wezeshi ya utalii iliyofanywa na Serikali kupitia TAWA ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuvutia watalii wengi kutembelea hifadhi hiyo lakini bila kusahau mchango mkubwa wa Sekta binafsi katika kutangaza vivutio vya utalii wa Nchi yetu.
Hii ni dalili tosha kuwa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 na malengo ya Serikali ya kufikisha idadi ya watalii Million 5 na mapato ya takribani dola billioni 6 ifikapo mwaka 2025 yanakwenda kufikiwa kwa kishindo na TAWA ikiwa ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika kuchangia kufikia malengo hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news