OUT yamlilia Rais mstaafu hayati Dkt.Ali Hassan Mwinyi

NA DKT.MOHAMED OMARY MAGUO

RAIS mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaji Dkt. Ali Hassan Mwinyi alikuwa kiongozi mahiri aliyejaaliwa hekima, busara na maono ya hali ya juu.

Ni katika uongozi ambapo alifanikiwa kufanya maamuzi magumu ya mageuzi na kuleta maendeleo makubwa katika nchi yetu ya Tanzania katika kipindi chake cha uongozi mwaka 1985 mpaka mwaka 1995.
Hayo yamesemwa na Prof. Elifas Bisanda ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania alipokuwa akizungumza na kitengo cha Mawasiliano na Masoko cha OUT Kinondoni jijini Dar es Salaam. 

Ikiwa ni sehemu ya salamu za rambirambi zake kufuatia kifo cha Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi kilichotokea tarehe 29 Februari, 2024.

Prof. Bisanda ameeleza,"Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais mstaafu Mzee Mwinyi.

"Huyu alikuwa ni kiongozi mpole, mwenye hekima na mwenye uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi ya kimageuzi ambayo leo ndiyo tunaendelea kuona yakileta maendeleo kwenye nchi yetu.

"Kupitia kauli yake ya "Ruksa" ambayo ilifunguwa fursa za mageuzi ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni na kukaribisha uchumi wa soko huria ulisaidia sana kukuza uwekezaji nchini. 

"Hakika Mzee Mwinyi atakumbukwa daima kutokana na mageuzi aliyoyafanya katika nchi yetu," amesema Prof. Bisanda.

Kutokana na mageuzi makubwa aliyoyafanya Rais Mwinyi, OUT ilimtunuku Shahada ya heshima ya Udaktari wa falsafa mwaka 2011 na hapa,"Prof. Bisanda anaeleza.

"OUT ilifanya utafiti wa kutosha kuhusu mchango wa Rais mstaafu Mzee Mwinyi na kujiridhisha kwamba anastahili kutunukiwa Shahada ya heshima ya Udaktari wa falsafa kutokana na mchango wake mkubwa kwenye maendeleo ya Tanzania.

Seneti ya chuo na Baraza la OUT waliridhia na tarehe 26 Novemba, 2011 katika Mahafali yaliyofanyika Bungo Kibaha Rais Mwinyi alitunukiwa Shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Hivyo Hayati Rais Dkt.Ali Hassan Mwinyi ni Alumni wa OUT na tunajivunia sana uwezo wake mkubwa katika uongozi wa nchi yetu katika nafasi mbalimbali alizohudumu akiwatumikia Watanzania.

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri wa kitaalamu Prof. Deus Ngaruko ameeleza kwamba Rais Dkt. Ali Hassan Mwinyi ndiye aliyetia Saini sheria ya kuanzishwa kwa OUT nambari 17 ya mwaka 1992.

Wakati huo yeye alikuwa ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hayati Rais Benjamini Williamu Mkapa ndiye alikuwa waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia aliyewasilisha mswada wa sheria hiyo bungeni na Bunge likajadili na kutunga sheria hiyo, Rais Mwinyi aliisaini na kutoa fursa ya OUT kuanzishwa. Prof. Ngaruko amefafanua,

"Wazo la kuanzisha OUT lilitolewa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika miaka ya 1960 mara baada ya kupata uhuru na ikaundwa kamati iliyoongozwa na Balozi Nicholaus Kuhanga ambaye amewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadae waziri wa Elimu hapa nchini.

Pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo cha Morogoro.

Kamati hii ilifanya kazi yake vizuri kwa kutembelea vyuo Vikuu Huria duniani ili kuona namna vinavyofanya kazi ya kutoa elimu ya juu kwa jamii kupitia njia za Huria na Masafa. Kamati ilikamilisha ripoti na kuiwasilisha serikalini mwishoni mwa miaka ya 1970.

Kutokana na hali ya vita vya Tanzania na Uganda na uhaba wa mafuta duniani wakati huo, jambo hilo liliwekwa kando kwanza ili kushughulikia matatizo hayo.

Baadae mwishoni mwa miaka ya 1980 kamati ilipewa tena jukumu la kuendeleza mchakato na ndipo mwaka 1992 kazi ikakamilika, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likatunga sheria na kutiwa Saini na Rais Dkt. Ali Hassan Mwinyi.

OUT ikawa ni Chuo Kikuu cha Tatu kuanzishwa hapa nchini baada ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo cha Morogoro," amesema Prof. Ngaruko.

Huu ulikuwa ni mnasaba wenye lengo la kuhakikisha elimu ya juu inawafikia Watanzania wote popote pale walipo iwe mijini au vijijini wakiwa wanaendelea na kazi zao. Kuanzishwa kwa OUT kumetoa fursa pana katika kuendeleza dhana ya elimu bila ukomo na mpaka kufika leo OUT ina wahitimu takribani 60,000 katika fani za ngazi mbalimbali.

Wahitimu hawa wanatumia maarifa na ujuzi walioupata kupitia OUT katika kukuza ubunifu na uvumbuzi wa kutatua changamoto zinazoikabili jamii na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Tanzania na dunia kwa jumla.

Rais mstaafu Dkt.Mwinyi kama ilivyo, kwamba ni kipenzi cha Watanzania, vile vile ni kipenzi cha OUT. Mhadhiri Mwandamizi katika taaluma za Maktaba Dkt. Athumani Samzugi anaeleza kwamba, katika mahafali ambayo Mzee Mwinyi alitunukiwa Shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa tulipata fursa ya kufundishwa Kiswahili na umma wote uliohudhuria mahafali hayo ulifurahia sana.

Wakati akitoa hotuba yake ya kukubali shahada aliyotunukiwa, Rais Ali Hassan Mwinyi alionesha umahiri wake katika lugha adhimu ya Kiswahili jambo lililokoga nyoyo na kuibuka shangwe kubwa kwa wahitimu, wahadhiri na wananchi kwa jumla.

Dkt. Samzugi anaendelea kueleza kwamba, Rais Ali Hassan Mwinyi alisema kwamba yeye ni muumini wa dhana ya elimu bila ukomo (life-long learning) na kwamba OUT ndiko mahali sahihi pa kutekeleza dhana hiyo kwa vitendo.

Hivyo akawataka Watanzania wote kutumia fursa zinazotolewa na OUT ili kujiendeleza kielimu huku wakiwa wanaendelea na majukumu yao kule kule walipo.

Jumuiya ya OUT inaendelea kutoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kufuatia kifo cha Rais mstaafu Dkt. Ali Hassan Mwinyi kilichotokea tarehe 29 February, 2024 na kuzikwa tarehe 02 Machi, 2024 kijijini kwake Mangapwani Unguja Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news