Salamu za Jumapili: Sifa apewe daima

NA LWAGA MWAMBANDE

REJEA Ufunuo 1:18, "Na aliye hai, nami nilikuwa nimekufa, na tazama,ni hai milele na milele.Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu."
Ukitafakari neno hili la Mungu, utaona kuwa,funguo ni ishara ya mamlaka,Yesu Kristo ni mkuu juu ya kifo.

Ushindi wa Kristo kwa kifo ulikuwa wa kudumu na wa milele. Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,kufufuka kwake Yesu, sifa apewe daima.Endelea;

1.Kujidhabihu ni kazi, kwake Mungu hiyo njema,
Kumwadhimisha Mwokozi, kwa fadhili zake njema,
Kujitoa yote dozi, kuondoa uhasama,
Kufufuka kwake Yesu, sifa apewe daima.

2.Ndivyo tunavyotakiwa, tumpe sifa daima,
Yale tuliyotendewa, Mungu azidi kuvuma,
Kwamba tumependelewa, kustahili uzima,
Kufufuka kwake Yesu, sifa apewe daima.

3.Kumwadhimisha daima, siku ngumu siku njema,
Ndivyo Neno linasema, wala kusiwe kukwama,
Hiyo ni njema huduma, tuzidi pata rehema,
Kufufuka kwake Yesu, sifa apewe daima.

4.Tuliokuwa wadhambi, na mwovu akitulima,
Sasa tuko kwenye kambi, yake Yesu ni salama,
Tushalitimua vumbi, mwovu hayuko salama,
Kufufuka kwake Yesu, sifa apewe daima,

5. Kazi kumsifu Bwana, huyu mtoa uzima,
Tulikuwa hapana, mbele yake sisi wema,
Naye twasikilizana, sasa na hata daima,
Kufufuka kwake Yesu, sifa apewe daima.

6.Unapoamka sifu, mbele ya Mungu ni vema,
Unapotembea sifu, kwamba Mungu wetu mwema,
Na kimoyomoyo sifu, akusikiliza mwema,
Kufufuka kwake Yesu, sifa apewe daima.

7.Tulokuwa tumekufa, sasa tunao uzima,
Hayo mema maarifa, Yesu alivyojituma,
Sasa tunafanya dhifa, kwa yake matendo mema,
Kufufuka kwake Yesu, sifa apewe daima.

8.Mshukuruni Mwokozi, kwa kuwa yeye ni mwema,
Amekuwa mkombozi, kwa kupangua hujuma,
Hii inatosha dozi, tufike kwenye uzima,
Kufufuka kwake Yesu, sifa apewe daima.

9.Sasa tujapo pigika, twajua tuna uzima,
Safarini tukichoka, mwishoni kuna uzima,
Ukombozi umefika, sasa na hata daima,
Kufufuka kwake Yesu, sifa apewe daima.

10.Sasa maishani mwetu, ni vema tuishi vyema,
Mwenendo na njia zetu, kwa Mungu ziwe salama,
Hata ushuhuda wetu, uwe ule wa uzima,
Kufufuka kwake Yesu, sifa apewe daima.

11.Haleluya kafufuka, Yesu mtoa uzima,
Nasi tunachangamka, kilio kimeshakoma,
Sasa muda twainuka, kunena habari njema,
Kufufuka kwake Yesu, sifa apewe daima.
(Waebrania 13:15)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news