Serikali yasema umeme wa kutosha upo njiani, Sekta ya Utalii yaimarika

NA GODFREY NNKO

Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa kihistoria wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji kwenye bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP).

Mradi huo utakuwa na vinu tisa vyenye uwezo wa kuzalisha megawati 235 kila kimoja na kufanya jumla ya megawati 2,115.
Hayo yamesemwa leo Machi 24, 2024 jijini Dar es Salaam na Msemaji Mkuu wa Serikali,Mobhare Matinyi wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarani.

“Ikumbukwe kwamba uwezo wa jumla wa kuzalisha umeme katika nchi yetu hivi sasa ni megawati 1,911 tu."

Amesema, wakati Rais Dkt. Samia anaingia madarakani, ujenzi wa bwawa hilo ulikuwa umefikia asilimia 33 lakini hivi sasa umekamilika kwaasilimia 96.28.

"Kinu Na. 9 kimeshawashwa na Na. 8 kinatarajiwa kuwashwa mwezi huu kikifuatiwa karibuni na kinu Na. 7.

"Mradi huu mkubwa wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unagharimu shilingi trilioni 6.5 na mpaka sasa serikali imeshamlipa mkandarasi shilingi trilioni 5.7 sawa na asilimia 88.7,” amesema Matinyi.

Amesema,miradi mingine ni ya ujenzi wa njia kubwa za kusafirisha umeme ambazo zitaunganisha mikoa mbalimbali hadi nchi jirani ambapo kutaiwezesha Tanzania kuuza nishati hiyo nje ya nchi pindi itapozalisha umeme wa ziada.

Matinyi ameitaja nchi hizo ni Uganda, Kenya itakayounganisha hadi Ethiopia, Sudan Kusini, Sudan na Misri pamoja na Zambia itakayounganisha umeme wa Tanzania na wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Aidha, chini ya TANESCO miradi ya vyanzo vingine inafanyiwa kazi ili hatimaye Tanzania ifikie uzalishaji wa megawati 10,000 ifikapo mwaka 2035.

Wakati huo huo, amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeunganisha jumla ya vijiji 5,481 na kufikisha vijiji vyenye kuwa 11,843 sawa na 96.14% ya vijiji vyote nchini ambavyo ni 12,318.

Pia, vitongoji 5,562 vimefikishiwa huduma ya umeme na kufanya jumla kuwa vitongoji 32,750 (51%) ya vitongoji vyote nchini ambavyo ni 64,760.

"Inatarajiwa kwamba kabla ya mwaka 2025 kumalizika, vitongoji vingine 8,150 vitakuwa vimefikishiwa umeme."

Utali

Matinyi amesema kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu idadi ya watalii nchini imeongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 walioipatia nchi mapato dola za Marekani bilioni 1.31 hadi watalii 1,808,205 mwaka 2023 walioingiza dola bilioni 3.37.

“Kwa kuongeza idadi ya watalii wengi baada ya mlipuko wa UVIKO-19 Tanzania sasa inashika nafasi ya pili barani Afrika baada ya Ethiopia na kwa kuongeza mapato makubwa inashika nafasi ya tatu baada ya Morocco na Mauritius."

Amesema,Tanzania imeendelea kutambuliwa kimataifa na kupata tuzo mbalimbali.

"Tuzo hizo ni Hifadhi ya Taifa Serengeti kuwa hifadhi bora barani Afrika kwa miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2023, Tanzania kuwa nchi ya saba miongoni mwa nchi 18 duniani zilizo bora kutembelewa kiutalii kwa mwaka 2022.

"Hifadhi ya Taifa Serengeti kumeorodheshwa kama eneo maridhawa la kutembelewa kwa mwaka 2023 na Hifadhi ya Taifa Serengeti kushika nafasi ya tatu ya vivutio bora vya asili duniani kwa mwaka 2023,” amesema Matinyi.

Mbali na hayo amesema kuwa, Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro imeshinda tuzo mbili za Best of the Best Travelers’ Choice na Africa’s Leading Tourist Destination kwa mwaka 2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news