Serikali yawekeza zaidi ya shilingi Trilioni 20 reli ya SGR

NA GODFREY NNKO

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imeendelea na uwekezaji katika ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) huku ikilenga kuyafikia nasoko ya kimkakati ndani na nje ya nchi.Hayo yamesemwa leo Machi 24, 2024 jijini Dar es Salaam na Msemaji Mkuu wa Serikali,Mobhare Matinyi wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarani.

Matinyi amesema,Rais Dkt.Samia alipoingia madarakani aliahidi kumalizia ujenzi wa vipande vilivyoanzishwa na Serikali ya Awamu Tano.

Sambamba na kuanza kwa ujenzi kwa vipande vya Makutupora-Tabora (km 368), Tabora-Isaka (km 165), Isaka-Mwanza (km 341) na Tabora hadi Kigoma (km 506).

“Wakati huo kipande cha Dar es Salaam-Morogoro kilikuwa kimefikia asilimia 83.55 na cha Morogoro-Makatupora asilimia 57.57 vikiwa na jumla ya kilomita 722.

"Hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 98.90 kwa kipande cha kwanza na asilimia 96.51 kwa kipande cha pili. Tayari fedha zimeshalipwa kiasi cha shilingi trilioni 6.805 kati ya shilingi trilioni 7.4 zilizotakiwa."

Pia, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia ilianzisha ujenzi wa vipande vitano vipya ambapo vitatu ni katika kukamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza ya reli ya SGR kati ya Dar es Salaam na Mwanza.

Kwa maana ya Makutupora hadi Tabora (km 368) ambapo ujenzi umefikia asilimia 13.98, Tabora hadi Isaka (km165) sasa ujenzi umefikia asilimia 5.44 na Isaka hadi Mwanza (km341) ambapo ujenzi umefikia asilimia 31.07.

Matinyi amesema kuwa,ujenzi wa awamu ya pili umeanza kwa vipande vya Tabora hadi Kigoma (km506) na kwa Uvinza hadi Musongati (km367).

"Kwa sasa taratibu za ununuzi zinaendelea. Hii inafanya jumla ya kilomita 1,560 za ujenzi wa SGR kutekelezwa ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita sawa na asilimia 68.4 ya ujenzi unaoendelea."

Amesema kuwa, thamani ya uwekezaji huo imefikia trilioni 23.3 ukiondoa kipande cha Uvinza hadi Musongati ambacho kipo katika hatua ya ununuzi.

"Jumla ya shilingi trilioni 10.1 zimeshalipwa kwa wakandarasi kwa mujibu wa hati za malipo na malipo ya awali kwa vipande vipya.

“Serikali pia inafanya ununuzi wa treni za kisasa (EMU) seti 10,mabehewa ya abiria 89 na mabehewa ya mizigo 1,430. Uwekezaji huu una thamani ya dola za Marekani milioni 508.6 sawa na shilingi trilioni 1.2,” amesema Matinyi.

Vile vile amesema kuwa, Rais Dkt.Samia alishatoa maelekezo kuhakikisha reli hii mpya inayafikia masoko ya kikanda kwa nchi jirani ikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kuleta manufaa makubwa nchini.

Amesema,juhudi zinaendelea na makubaliano na nchi hizo yameshafikiwa ili reli itoke Uvinza hapa nchini hadi Kindu nchini DRC kupitia Musongati-Gitega-Bujumbura nchini Burundi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news