Somalia yajiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)

ARUSHA-Nchi ya Shirikisho la Jamhuri ya Somalia imejiunga rasmi kuwa mwanachama wa nane wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tukio hilo limefanyika katika makao makuu ya EAC jijini Arusha na kuelezwa kuwa, itasaidia suala zima la msukumo wa changamoto za ajira kwa nchi wanachama pamoja na kupanua soko la pamoja.
Kujiunga kwa Somalia ni kutokana na kikao cha wakuu wa nchi kilichoketi Desemba 25, mwaka jana jijini Arusha na kukubali nchi hiyo kujiunga na jumuiya hiyo.

Dkt.Peter Mathuki ambaye ni Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo katika sherehe fupi ya kupandisha bendera na kupokea hati za unachama wa Somalia makao makuu ya EAC jijini Arusha amesema, soko la jumuiya limepanua wigo na kuwa na watu takribani milioni 350 kwa sasa na hivyo kuiwezesha jumuiya hiyo kujipanua kibiashara.

Amesema, kiwango cha ukuaji wa pato la EAC limeongezeka kutoka dola bilioni 2.5 hadi dola bilioni 3 na kuongeza soko la ajira kuondoa changamoto za ukosefu wa ajira kwa nchi wanachama na ongezeko la bidhaa.

Dkt.Mathuki amesema kuwa,kuongezeka kwa soka hilo la watu wanaofikia milioni 350 kutaondoa changamoto za upungufu wa ajira na kupelekea wananchi kuchangamkia uzalishaji wa bidhaa na kuuza katika soko la pamoja.

"Hii ni moja ya kuondoa changamoto za ajira na kurudisha hali ya usalama katika mataifa ya jumuiya ikiwa soko la jumuiya kwa sasa lina watu takribani milioni 350,uzalishaji wa bidhaa utaondoa upungufu na kuzalisha ajira hivyo kuwepo kwa usalama katika nchi zetu."

Naye Waziri wa Habari wa Somalia,Daud Aweso amesema wanayofuraha kubwa kukamilisha safari ndefu ya miaka 12 na safari hiyo ilikuwa na kazi kubwa yenye changamoto, lakini hawakuchoka kufikia hatua hiyo ya kukamilisha utaratibu wa mwisho wa kujiunga na EAC.

Pia amesema,jumuiya hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa Somalia na nchi zote wanachama kwa kuwa nchi ya nane kujiunga na jumuiya hiyo.

EAC ni jumuiya ya kiserikali inayoundwa na nchi nane kwa sasa za Afrika Mashariki ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Somalia,Uganda na Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news