Tanzania nchi ya pili Afrika kwa usalama wa mitandao

DAR ES SALAAM-Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetajwa kuwa ni nchi ya pili barani Afrika kwa usalama wa mitandao.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama nchini (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga.

Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama nchini (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga, katika mahojiano maalumu wakati alipozungumzia mafanikio, mipango na mikakati ya kukuza tehama nchini.

Kwa mujibu wa Dkt. Mwasaga, kupaa kwa Tanzania katika usalama wa mitandao kunatokana na taarifa za Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) kupitia Global Cybersecurity Index. Tanzania ni mjumbe wa Baraza Kuu la ITU.

Aliongeza kuwa, licha ya kung’ara katika usalama wa mitandao, Tanzania imetajwa kuwa ya kwanza katika huduma ya ufikishaji wa huduma ya intaneti kwa kasi kwenye nyumba na majengo. 

Hii ni kwa mujibu wa vipimo vya utayari wan chi kuhusu mitandao (global Network Readiness Index 2023) inayoandaliwa na taasisi za Portulans na Shule ya Biashara ya Said katika Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza.

Dkt. Mwasaga alisema kwamba, mafanikio hayo ni jitihada za ICTC katika kubuni, kukuza na kuendeleza kazi na programu bunifu za teknolojia.

“Tunajitahidi kutoa fursa kwa vijana kubuni kazi na programu mbalimbali za tehama ili kuendeleza teknolojia hii na kuifanya Tanzania ya kidijitali,” alisema Dkt. Mwasaga.

Alisema, katika kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali, Serikali kupitia ICTC inaendelea na mpango wa kujenga vituo nane vya tehama nchini.

Alisema, lengo kubwa la kuanzishwa vituo hivyo ni kuhakikisha inasimamia nguzo tano ikiwemo kukuza vipaji bunifu katika tehama na kupanua wigo kwa vijana kufanya ubunifu na kuuendeleza.

Serikali kupitia ICTC inakusudia kujenga vituo nane nchini vya ubunifu wa teknolojia vitakayowezesha vijana na wananchi kwa ujumla kuvitumia kuboresha kazi zao za kibunifu.

Vituo hivyo vinatarajiwa kujengwa katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Lindi, Tanga, Mwanza, Mbeya na Zanzibar.

“Huu ni mpango wa awali, lakini mkakati uliopo ni kujenga vituo katika mikoa yote na wilaya zote, ili wananchi waweze kuvitumia na kujifunza suala zima la teknolojia,” alisema.

Aidha, alisema, vituo hivyo vitajengwa katika maeneo ya shule ambavyo vitasaidia vijana nchini kuendelea kuibua vitu mbalimbali vinavyuohusiana na teknolojia pamoja na kuendeleza, ambapo vitakuwa na uwezo wa kuingiza watu 200 kwa wakati mmoja.

Amewaomba wadau mbalimbali kushirikiana katika kuanzisha vituo hivyo, lengo likiwa ni kukuza vipaji tofauti na kulinda kazi bunifu za kiteknolojia.

Dkt. Mwasaga alisema, watu wengi wamekuwa na hofu na akili bandia au akili mnemba (Artificial Intelligence – AI) kwamba inaweza kuwakosesha kazi, jambo ambalo alisema siyo kweli, kwani AI inaleta tija na kwamba watu wakipewa ujuzi mpya kuhusu teknolojia hiyo itasaidia.

Alisema watajenga kituo cha Artificial Intelligence kwa ajili ya kuendeleza wataalam wa Tehama pamoja na kuwezesha mafunzo maalum ya wataalam wa Tehama 500 ili kukuza na kuendeleza ujuzi wa Tehama nchini.

Inaelezwa kwamba, ujenzi wa vituo hivyo ni sehemu ya vipaumbele 13 vya ICTC ambavyo vina lengo la kuleta mapinduzi ya teknolojia na ubunifu nchini.

“Tunatarajia kuanzisha kituo cha kutengeneza na kuboresha vifaa vya Tehama (ICT Refurbishment and Assembly Centre) na vituo vya majaribio vya ubunifu Tehama (District ICT Start-up Innovation Hubs) katika wilaya 10,” alisema Dkt. Mwasaga.

Aidha, alisema watafanya tafiti za maendeleo ya Tehama nchini na kufanya tathmini ya kitaifa ya hatua za utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya Tehama.

Aliongeza kwamba, wataratibu na kuandaa matukio ya kuvutia uwekezaji na kutangaza masoko ya bidhaa za Tehama ndani na nje ya nchi.

“Tutashirikiana na washirika wa maendeleo na kampuni za kimataifa katika kuendeleza bunifu za Tehama ikiwemo kuwezesha utengenezaji wa bidhaa za Tehama hapa nchini,” alisema. 

Kutokana na juhudi za ICTC na Serikali kwa ujumla, ITU inakusudia kushirikiana na serikali kujenga kituo cha ubunifu wa Tehama kitakachohudumia Kanda ya Afrika Mashariki.

Alisema, majukumu mengine watakayoyafanya ni pamoja na kukuza soko la bidhaa na huduma za kampuni ndogo ndogo “start-up” kwa kushiriki maonesho na makongamano yanayohusu fursa za startups duniani.

ICTC pia inakusudia kuratibu na kutengeneza mfumo wa usimamizi wa utekelezaji wa Sera ya Tehama na kufanya tafiti za kuweza kufanya maboresho ya sera kulingana na mabadiliko ya teknolojia.

Mikakati mingine ni pamoja na kujenga Metaverse Studio kwa ajili ya kutengeneza maudhui ya metaverse na pia kuboresha maudhui ya mitandao ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti za maendeleo ya Tehama kwa kila wilaya na kuanzisha Kituo cha Resilience Academy hapa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news