Suluhisho akiba ya fedha za kigeni, bei ya mafuta ni matumizi ya gesi asilia, Kamati ya Bunge yashauri

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kuendelea kuwekeza zaidi katika vituo vya kujaza gesi asilia kwenye magari na karakana za kubadilisha mifumo.
Lengo likiwa ni kutoa fursa kwa wananchi wengi kutumia gesi asilia kuendeshea magari, hatua ambayo itapunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza mafuta nje ya nchi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo,Dkt.David Mathayo
ameyasema hayo leo Machi 15,2024 baada ya kamati hiyo kutembelea vituo vya kujaza gesi iliyoshindiliwa kwenye magari vya Mastergas TAQA Dalbit CNG Station and Conversion Center kilichopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Sambamba na Kituo cha CNG Ubungo chini ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Uzalishaji Gesi ya PanAfrican Energy Tanzania (PAET) jijini Dar es Salaam.

"Kwa hiyo ninaishauri Serikali pamoja na sekta binafsi waweze kuongeza vituo vya kuuza gesi kwa ajili ya kujaza kwenye magari, lakini pia karakana za kubadilisha mifumo ya Diezeli na Petroli kwenda kwenye gesi ili tuweze kutumia gesi yetu ya hapa nchini.

"Faida kubwa ya kwanza ya matumizi ya gesi, kwanza ni kwamba mafuta yote tunayoyatumia hapa nchini tunayaagiza kutoka nje ya nchi, kwa hiyo tukitumia gesi yetu ya Tanzania tutakuwa hatuhitaji fedha za kigeni kuagiza nje maana tunayo, ni ya kwetu, rasilimali ya kwetu, lakini la pili kwa sababu matumizi ya gesi ni rahisi."

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wamepata fursa ya kushuhudia namna vituo hivyo vinatoa huduma huku wakiuliza maswali na kupatiwa ufafanuzi wa kitaalamu.

Katika hatua nyingine, Dkt.Mathayo ameipongeza Serikali kwa jitihada kubwa ambazo inaendelea nazo za kuhakikisha matumizi ya nishati ya gesi asilia yanakuwa endelevu nchini ikiwemo katika mifumo ya magari.
Amesema, matumizi ya gesi ni nafuu zaidi katika uendeshaji wa magari tofauti na matumizi ya Petroli na Diezeli.

"Lakini, pia unatembea umbali mrefu kwa matumizi kidogo, kwa hiyo ninaipongeza Serikali kwa hilo, sisi kama Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini tungependa kuishauri TPDC na Serikali kwa ujumla kwamba waendelee kuhamasisha vituo viwe vingi na vya kutosha.

"Kwa sababu kadri miezi inavyokwenda wanaohitaji matumizi ya gesi wameongezeka kama mnavyoona hapa, magari mengi yanataka kujaziwa gesi."

Pia, amesema vijana wengi watapata ajira na wataweza kujiajiri kwenye magari kama ya Ubber na Bolt, kwa sababu matumizi ya gesi ni rahisi zaidi.

"Lakini, kama nilivyosema hii ni rasilimali yetu ambayo haihitaji fedha za kigeni, kwa hiyo tunapowekeza tunahakikisha kwamba, fedha zenyewe tunazotumia zinabaki hapa hapa ndani ya nchi na vijana wetu wananufaika zaidi.

"Tunampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, tunaipongeza wizara kwa jitihada wanazochukua, tunampongeza Naibu Waziri Mkuu, Dkt.Doto Mashaka Biteko kwa kazi nzuri anayoifanya.

"Vile vile, kwa sababu haya magari yanayobadilishwa ni yale ambayo yaliingia na mfumo wa mafuta, tunaishauri Serikali kupitia Wizara ya Fedha iweze kuondoa kodi kwa ajili ya vifaa vinavyotumika kwa ajili ya kuunganishia au kubadilisha mifumo ya mafuta kwenda kwenye gesi.
"Ili Watanzania wengi waweze kuunganisha magari yao yaweze kutumia gesi, sasa hivi gari moja kubadilisha mfumo inachukua shilingi milioni moja na laki nane na hamsini mpaka milioni mbili.

"Kwa hiyo, vifaa vile vikishushwa bei ni dhairi kuwa wananchi wengi wataweza kuunganisha mfumo wa magari yao kwa kutumia gesi. Hilo la kwanza."

"Lakini la pili, ninaishauri Serikali vile vile kuhamasisha wale wanaouza magari kuleta magari ambayo tayari yameshabadilishwa yaani kwa mfumo wa matumizi ya gesi, yakitoka nje kwenye viwanda yameshatengenezwa kwa mfumo wa kutumia gesi, kwa sababu kubadilishia hapa ni gharama.

"Sasa, wakiingiza magari ambayo tayari yameshatengenezwa huko nje itasaidia zaidi, lakini pia magari ya Serikali nayo yanayoingia, Serikali ijipange kuhakikisha magari yake yanayoingia yanakuwa na mfumo wa gesi, kuliko kubadilishia hapa nchini ambapo inakuwa ni gharama kubwa."

Amesema, Serikali ikiweza kulitekeleza hilo itapuguza matumizi makubwa ya fedha ambazo zinatumika kwa ajili ya mafuta.

Naibu Waziri

Naye, Naibu Waziri wa Nishati,Judith Kapinga amesema, Serikali kupitia TPDC wanayo mkakati wa kuhakikisha vituo hivyo vinasambaa maeneo mengi na wameyapokea mapendekezo ya kamati.
"Kwanza, niishukuru kamati, lakini niseme tumepokea ushauri na maelekezo ya kamati. Moja kamati imetushauri kuhusiana na kuongeza vituo hivi kwa ajili ya kusogeza huduma zaidi kwa watumiaji.

"Tumepokea ushauri na maelekezo ya kamati, na Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) tayari tunao mkakati wa kuendeleza kuongeza vituo.

"Mpaka sasa vituo vinavyofanya kazi ni vitano, lakini vituo takribani 15 tayari vipo kwenye mchakato na vinaendelea kwa ajili ya kujengwa ili wananchi waweze kunufaika zaidi, ndipo tutakapoweza kupunguza msongamano katika vituo vilivyopo.

"Lakini, vile vile Serikali inayo mkakati wa kushirikiana na sekta binafsi ikiwemo mashirika na kampuni binafsi ili kuongeza karakana kwa ajili ya kubadilisha mifumo ili wananchi wengi waweze kupata huduma hiyo."

Mheshimiwa Kapinga pia amesema, wamelichukua pendekezo la kamati kuhusu namna ambavyo Serikali itaangalia ili kupunguza gharama za kubadilisha mfumo huo.
"Na kwa kuwa, sasa hivi ndipo tumeweka kasi na msukumo kwa ajili ya kuendeleza suala hili, TPDC kwa kushirikiana na wabia wengine binafsi tunaendelea kuchakata na kuona kadri tunavyoongeza teknolojia na tunavyoongeza miundombinu zaidi kuona gharama zinaendelea kupungua ili wananchi waweze kunufaika.

"Lakini, pia nitoe rai kwa Watanzania kwa ujumla, wote tuna jukumu la kutunza mazingira.

"Kutumia gesi iliyoshindiliwa kwenye magari ni bei nafuu sana, wote mmeona kulinganisha na petroli ama diezeli."

TPDC

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),Mussa Mohammed Makame amesema kuwa, vituo ambavyo vinatarajiwa kujengwa ni pamoja na Mlimani City ambapo vitajengwa viwili.

Pia, maeneo ya viwanja vya Posta,Mwenge, Mbezi, Tegeta ambapo pia wadau wa sekta binafsi wakiwemo Puma watashiriki kufanikisha hilo.

Aidha, amesema TPDC wapo katika mchakato wa kununua vituo vya kuhama vitano ambavyo vitanunuliwa kwa mpigo kati ya sasa hivi na mwezi wa nane ili kuvitawanya katika maeneo mbalimbali.

"Na tuna takribani vituo 15 ambavyo vitakuja kwa pamoja ndani ya mwaka mmoja, kwa hiyo hii changamoto ya uchache wa vituo vya kutolea huduma itaondoka."

TAQA Dalbit

Kwa upande wake mwakilishi wa Mastergas TAQA Dalbit CNG Station and Conversion Center kilichopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhandisi Revocatus Chales amesema, matumizi ya mfumo huo yana tija kubwa kwa wamiliki wa magari.
Amesema kuwa, kwa siku wanahudumia magari 700 hadi 800 au zaidi ya hapo inategemeana na mzunguko wa magari kwa siku husika. "Kwa maana ya magari ambayo yameshafungiwa mfumo wa gesi."

Amesema, magari ambayo wanayafunga kwa sasa katika kituo chao ni ya mfumo wa Petrol tu.

"Mfumo wa Diesel bado hatujaanza,lakini magari ya aina zote yanaweza kubadilishwa. Katika kituo chetu mpaka sasa tumeshafunga magari zaidi ya 150 toka mwezi wa 11 tarehe 10,2023 tulipofungua kituo chetu.

"Kwa bei mfumo wa gesi kubadilisha inategemeana na capacity ya mtungi ambao utafungwa kwenye gari.

"Kama ni mtungi wa kilo 11, mtungi wa kilo 15 au mtungi wa kilo 17, kwa mtungi wa kilo 11 bei yetu inaenda mpaka shilingi milioni 1.8 na mtungi wa kilo 15 bei inaenda hadi shilingi milioni 2 mpaka milioni mbili na elfu tisini na nne.
"Lakini, pia bei zinabadilika kulingana na wakati na aina ya gari."

Pia, Mhandisi huyo ametoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa ya kuunganisha magari yao katika mifumo ya matumizi ya gesi,kwani wataokoa fedha nyingi katika matumizi.

"Kwa mfano, bei ya mafuta kwa sasa ni shilingi 3160 na bei ya gesi ni shilingi 1550.
"Hivyo, utaangalia kwenye bei namna ambavyo mtu anayetumia gesi atakuwa amepata unafuu na kuweza kuokoa kiasi fulani cha hela.

"Lakini, pia ukiangalia kwa upande wa mileages mfano kwa madereva Bolt unaweza kukuta mtu anaokoa mpaka elfu 50 kwa siku, pesa ambayo angeitumia kujaza mafuta tu.

"Kwa mfano mtu anaweza kutembea mpaka kilomita 230 kwa gari aina ya IST kwa mtungi wa kilo 15 ambao kuujaza hauzidi elfu 23 kwa kilomita 230,kwa hiyo utaona unafuu huo."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news