Tanzania yatekeleza ahadi ya Beijing

NA SALMA LUSANGI
New York

LICHA ya changamoto za kiuchumi duniani, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweza kutekeleza hatua mbalimbali zilizolengwa ili kupunguza athari kwa wanawake, na kuimarisha dhamira ya Utekelezaji wa Jukwaa la Beijing na ahadi ya Kizazi chenye Usawa.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto Zanzibar,Mhe. Riziki Pembe Juma akitoa taarifa ya utekelezaji masaula ya Wanawake na Wasichana nchini Tanzania katika mkutano wa Hadhi ya Wanawake (CSW68) uliyofanyika wiki iliyopita katika ukumbi wa Umoja wa Mataifa jijini York Nchini Marekani.

Kauli hiyo imetolewa katika mkutano wa Hadhi ya Wanawake (CSW68) uliyofanyika wiki iliyopita katika ukumbi wa Umoja wa Mataifa jijini New York nchini Marekani na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji masaula ya wanawake na wasichana nchini Tanzania.

Amesema, hivi karibuni Tanzania ilizindua Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Jinsia na Wanawake (2023) iliyopitiwa upya, ambayo pia inaangazia Bajeti inayozingatia Jinsia kama nyenzo muhimu ya kutathmini athari za kijinsia za sera ya uchumi mkuu na sera za fedha, kwa kutambua athari zake katika ukuaji wa uchumi, maendeleo ya rasilimali watu na ajira kwa usawa.
Mheshimiwa Riziki ametoa taarifa hiyo kulingana na mada ya mkutano huo ambayo imesema: kuharikisha upatikanaji wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote kwa kukabiliana na umaskini na kuimarisha taasisi na fedha kwa mtazamo wa kijinsia.

Hivyo ameeleza Serikali ya Tanzania imetenga rasilimali zaidi kwa ajili ya kushughulikia usawa wa kijinsia katika sekta zinazoathiri moja kwa moja ustawi wa wanawake na wasichana. Amesma hasa, bajeti ya Wizara yenye dhamana ya Jinsia, katika Mwaka huu wa Fedha 2023/24 mgao wa bajeti uliongezeka kwa asilimia 71 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Alifahamisha kwamba Benki Kuu ya Tanzania imeanzisha Chombo cha ufadhili wa takriban Dola za Kimarekani Milioni 400 kwa benki na taasisi za fedha kupata riba ya asilimia 3%. Bchombo hicho kimeongeza fedha katika sekta ya kilimo ambapo asilimia 50.3 ya wanawake wanaajiriwa katika sekta ya kilimo.

Amefafanua kwa kusema utoaji wa mikopo hiyo umepewa kipaumbele kwa wanawake wa vijijini ambapo zaidi ya asilimia 35 ya fedha zote zimetengwa kwa wanawake katika sekta ya kilimo, ufugaji, ufugaji nyuki, kilimo cha mwani n.k.

Aidha alisema Serikali pia inatekeleza sera ya elimu bila malipo na imeanzisha mpango wa kuwarejesha skuli/shuleni wasichana waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali. Zoezi la uandikishaji limeanza tangu mwaka 2020 na linaendelea hadi sasa, ambapo uwiano wa shule za awali, msingi na sekondari kwa sasa ni 1:1 kati ya wavulana na wasichana.

Amesema Jumla ya wasichana Milioni 29.5 wamefaidika na elimu bila malipo, na juhudi kama hizo zinaendelea ili kuhakikisha kuwa ongezeko la uandikishaji wa elimu linaleta kazi nzuri kwa wanawake na wasichana katika soko la ajira.
Pia amesema kwa kutambua umuhimu wa kuziba pengo la usawa wa kijinsia katika upatikanaji na matumizi ya teknolojia, Serikali pia inatekeleza Mpango wa Udhamini wa Mama Samia unaotolewa kwa wanafunzi katika Vyuo vya Elimu ya Juu.

Alisema utekelezaji wa programu shirikishi za hifadhi ya jamii, kama vile Mpango wa kupunguza ukali wa umasikini Tanzania (TASAF) na Pensheni jamii kwa Wazee wa Zanzibar, inasisitiza mbinu ya kina ya uwezeshaji wa kiuchumi Tanzania.

Aidha Mhe Riziki mapema aliwasilisha salamu za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (URT) Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Kwanza Mwanamke katika Kanda ya Afrika Mashariki. Chini ya uongozi wake mahiri, umeweka mipango na programu kadhaa za kukabiliana na aina zote za ukatili, ili kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news